Thursday, April 19, 2018

WAFANYABIASHARA MKOANI SIMIYU WAUNGA MKONO SERIKALI UJENZI WA SHULE YA SEKONDARI YA MKOA

Wafanyabiashara wa Mkoa wa Simiyu wamekubali kuunga mkono Serikali katika Ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Mkoa wa Simiyu inayotarajiwa kuanza kujengwa mwezi Juni mwaka huu.


Kauli hiyo ilitolewa na Wafanyabiashara hao katika kikao chao na Mkuu wa Mkoa kilichofanyika  jana Mjini Bariadi, ambacho kilifanyika kwa lengo la kuzungumzia fursa za biashara na uwekezaji zilizopo mkoani humo, changamoto zinazowakabili na utatuzi wake.

Awali akifungua kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amesema Serikali mkoani humo imekusudia kuwa na shule kubwa itakayoweza kuchukua wanafunzi 1000 ambayo itakayopatikana kwa kujenga upya shule ya Sekondari Simiyu (Kidato cha kwanza hadi cha Nne), ambapo aliahidi kuwa ofisi yake itatoa fedha kiasi na akawaomba wafanyabiasha wazawa kuchangia Ujenzi wa shule hiyo kwa ajili ya maendeleo ya Mkoa.

Amesema  pamoja na kujenga upya Shule ya Sekondari Simiyu, katika shule hiyo kutajengwa mabweni kwa ajili ya wanafunzi wa kike ili wanafunzi wote wa kike wasome wakiwa wanafunzi wa bweni(boarding).

Ameongeza kuwa shule hiyo itakuwa ikichukua wanafunzi watakaofanya vizuri kutoka katika wilaya nyingine ili waandaliwe vema na kuimarisha shule za Kidato cha Tano na Sita na kuwa katika uwezo wa kushindana na wenzao kutoka mikoa mingine.

Aidha, amesema mara baada ya kukamilisha kuimarisha Shule ya Sekondari ya Simiyu Mkoa huo umedhamiria kuwa na Shule ya Sekondari ya Wasichana Simiyu na Shule ya Sekondari ya Wavulana Simiyu,  ambazo zitapatikana kwa Kujenga Upya au  kubadili zilizopo kwa kibali maalumu cha Wizara yenye dhamana na Elimu, ili kuwa na shule mbili za mkoa moja ya wasichana na nyingine ya wavulana.

"Hatuwezi kuwa Makao Makuu ya Mkoa ambayo elimu yote inaishia Shule za Kata, ni lazima tutengeneze shule ambayo watoto wetu wakifanya vizuri katika wilaya zetu wanakuja kusoma hapa; hatuwaweza kushindana na kufanya mambo yote mazuri tuliyojadili hapa ya viwanda na mengine kama hatutaelimisha watu wetu" alisema.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Mkoa wa Simiyu Bw. Njalu Silanga amesema Wafanyabiashara wako tayari kuunga mkono juhudi za Serikali katika ujenzi wa Shule ya Mkoa jambo ambalo litakuwa mwendelezo wa kile kilichowahi kufanyika miaka iliyopita ambapo wafanyabiashara hao walijenga shule ya Sekondari Biashara na kuikabidhi kwa Serikali.

“Sisi wana Simiyu tunapenda maendeleo, tumewahi kukusanywa kama hivi leo tukakubaliana tukajenga Shule ya Sekondari Biashara tukaikabidhi Serikali, pia wapo watu hapa kwenye maeneo yao wamejenga madarasa tena ya viwango wakaikabidhi Serikali, kujenga Shule ya Sekondari ya Mkoa inawezekana” alisema  Njalu.

Wakati huo huo wafanyabiashara hao wameahidi kuwashirikisha Wafanyabiashara wengine ambao ni wazaliwa wa Mkoa wa Simiyu wanaofanya biashara zao katika mikoa mingine ili washirikiane katika kufanikisha Ujenzi wa Shule ya Sekondari Mkoa wa Simiyu.
Baadhi ya Wafanyabiashara wa Mkoa wa Simiyu, wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(hayupo pichani) katika kikao chao na Mkuu huyo wa Mkoa kilichofanyika jana Mjini Bariadi.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Mkoa wa Simiyu ambaye pia ni Mbunge wa Itilima Mhe. Njalu Silanga akizungumza katika kikao cha Wafanyabiashara wa Mkoa huo na Mkuu wa Mkoa huo katika Kikao kilichofanyika jana Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na Wafanyabiashara wa Mkoa huo katika kikao kilichofanyika Mjini Bariadi.
Baadhi ya Wafanyabiashara wa Mkoa wa Simiyu, wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(hayupo pichani) katika kikao chao na Mkuu huyo wa Mkoa kilichofanyika jana Mjini Bariadi.





0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!