Friday, April 19, 2019

DAKTARI BINGWA AWATAHADHARISHA WANANCHI KUTOCHANGANYA DAWA ZA HOSPITALI NA KIENYEJI


Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na maradhi ya moyo  kutoka Wizara ya afya Prof. Harun Nyagori ametoa wito kwa Watanzania kutochanganya dawa za hospitali na kienyeji wakati wa matibabu yao ili kuepuka athari kubwa za kiafya zinazoweza kujitokeza.

Prof Nyagori ameyasema hayo Aprili 18, 2019  wakati akizungumza na  waandishi wa habari  katika Mkutano Mkuu wa chama cha wanataaluma na wajasiriamali wa Kanisa la Waadventista Wasabato(ATAPE),unaofanyika mjini Bariadi.

Amesema kuwa uchanganyaji wa dawa za hospitali na za kienyeji ni hatari kwa afya ya binadamu, hivyo ni vema wagonjwa mbalimbali wa magonjwa ya ndani na maradhi ya moyo kuamua kufanya maamuzi ya matumizi ya dawa upande mmoja ili wasije kujisababishia madhara makubwa zaidi.

“Ni vema wagonjwa wasichanganye dawa za hospitali na za kienyeji, japo dawa nyingi za hospitali zinatengenezwa na Mitishamba lakini utofauti wa dawa za hospitali na dawa za kienyeji ni kwamba wanapotumia dawa za kienyeji wanatumia pasipokujua kiwango cha kemikali zilizopo na aina ya sumu iliyopo kwenye dawa hizo”

“Nimeona wagonjwa wengi wanaochanganya dawa za hospitali na za kienyeji wanapata madhara mbalimbali mwilini, wengine figo zao zimeshindwa kufanya kazi vizuri, wengine maini yameharibika, sukari imezidi kupanda; kwa hiyo nawashauri kama wakiamua kutumia dawa za hospitali watumie hizo na kama wameamua kutumia mitishamba wazitumie hizo tu wasichanganye” alisema Dkt. Nyagori.

Sambamba na hilo Prof Nyagori, pia amesema kuwa katika siku sita za mkutano mkuu wa ATAPE unaoendelea Mkoani Simiyu, ametoa wito kwa wananchi na wakazi wa Simiyu kujitokeza kwa wingi kupima afya zao.

Ameongeza kuwa ndani ya siku mbili ambazo wamekuwa wakitoa huduma hizo za magonjwa ya ndani na maradhi ya moyo, jumla ya wagonjwa 269 walijitokeza kupima afya zao na kati ya hao 103 waligundulika kuwa shinikizo la damu,62 walikuwa na sukari na 140 wenye uzito uliopindukia.

Nao baadhi ya wananchi waliojitokeza kupima afya zao wameshukuru huduma hizo kutoka kwa madaktari bingwa kusogezwa karibu yao kupitia mkutano wa ATAPE huku wakieleza kufurahishwa na huduma hizo kutolewa kwa gharama nafuu.

“Binafsi nimefurahishwa na huduma za madaktari bingwa ambazo nimezipata kupitia mkutano huu wa ATAPE, nimepima na nimeweza kujua afya yangu, kilichonifurahisha zaidi ni kwamba nimetumia shilingi elfu kumi tu kupima shinikizo la damu, sukari na vipimo vingine”alisema Mchungaji Marco Barnabas.

“Huduma zinazotolewa hapa ni nzuri na zinatolewa kwa gharama nafuu kabisa nitoe wito kwa Wanasimiyu kujitokeza kwa wingi kuja kupima afya zao, ili waweze kutambua hali za afya zao na kupata ushauri wa wataalam bingwa” alisema Namkunda Mburuja.

Mkutano Mkuu wa Mkuu wa chama cha wanataaluma na wajasiriamali wa Kanisa la Waadventista Wasabato(ATAPE),unaendelea  mjini Bariadi na unatarajiwa kuhitimishwa Jumapili ya tarehe 21/04/2019; wanataaluma mbalimbali wanaendelea kutoa huduma, huku wajasirimali wakiendelea kuuza bidhaa mbalimbali katika viwanja vya shule ya Sekondari Kusekwa memorial
MWISHO
Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na maradhi ya moyo  kutoka Wizara ya afya, Prof. Harun Nyagori akimhudumia Bi. Eveline Mshanga wakati alipokuwa akitoa huduma za magonjwa ya moyo katika Mkutano wa ATAPE mjini Bariadi.
Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na maradhi ya moyo  kutoka Wizara ya afya, Prof. Harun Nyagori akiwaelezea jambo waandishi wa habari alipozungumza nao wakati akitoa huduma za magonjwa ya moyo katika Mkutano wa ATAPE mjini Bariadi.



0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!