Blog rasmi ya Mkoa wa Simiyu

Friday, April 29, 2022

Mhe. Kafulila Awapongeza Walimu na Wanafunzi Waliofanya Vizuri Katika Mitihani ya Taifa 2021, Aongeza Kiasi cha Zawadi za Ufaulu
















Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. David Kafulila ametumia kiasi cha Tsh.59,040,000/- (Milioni hamsini na tisa na arobaini elfu tu) kama zawadi na motisha kwa walimu, wanafunzi na shule zilizofanya vizuri katika mitihani ya Taifa ya mwaka 2021.

Hafla ya kukabidhi zawadi hizo imefanyika hivi karibuni katika ukumbi wa shule ya Sekondari Kusekwa iliyopo mjini Bariadi.

Zawadi hizo ambazo zilikuwa katika kategoria mbili. Kategoria ya kwanza ilihusisha zawadi kwa Mtihani wa darasa saba ambapo ndani yake kulikuwa na makundi manne ambayo yalipewa zawadi.Kundi la kwanza la zawadi lilienda kwa shule iliyoingia kumi bora kitaifa- katika shule za Serikali ambapo shule ya Msingi Mwanhegele iliyopo Wilayani Maswa imepokea zawadi ya Tsh.2,000,000/- (milioni mbili). 

Kundi la pili la zawadi zimetolewa kwa wanafunzi watano walioingia kumi bora kitaifa ambapo kila mmoja wao alipokea fedha taslim kiasi cha Tsh.1,000,000/-(milioni moja). Kundi la tatu la zawadi zilitolewa kwa walimu wawili waliofanya vizuri zaidi kitaifa katika masomo ya Hisabati, Stadi za Kazi na Maarifa ya Jamii ambapo kila mmoja wao  alipokea zawadi ya fedha taslim kiasi cha Tsh.300,000/-.

Kundi la nne la zawadi zilizotolewa kwa Walimu 36 waliofaulisha masomo yao kwa GPA nzuri zaidi Kimkoa pamoja na Walimu Wakuu wao kwa niaba ya shule zao. Katika kundi zilitolewa zawadi zenye jumla ya Tsh. 4,500,000/= na kufanya thamani ya zawadi zote zilizotolewa kwa ufaulu wa darasa la saba kufikia kiasi cha Tsh. 12,100,000/=(Milioni kumi na mbili na laki moja tu).

Kategoria ya pili ya zawadi zilizotolewa na Mhe.Kafulila zilielekezwa kwa ufaulu wa Mtihani wa kidato cha Nne,ambapo napo kulikuwa na makundi manne yaliyopokea zawadi hizo. Kundi la kwanza la zawadi lilielekezwa kwa kwa Shule iliyoingia Kumi Bora Kitaifa  katika shule za Serikali ambapo shule ya sekondari Ng'hoboko iliyopo Wilayani Meatu ilipokea kiasi cha  Tsh.3,000,000/-. 

Kundi la pili la zawadi zilienda kwa Wanafunzi waliofaulu Mtihani kwa  kupata daraja la kwanza alama 7 (Division One - Point kwa 7 Shule za Serikali),ambapo jumla ya wanafunzi  6 walipokea zawadi ya Tsh. 1,000,000/- kila mmoja. Kundi la tatu la zawadi zilielekezwa kwa Walimu waliofaulisha masomo yao kwa GPA nzuri zaidi ambapo jumla ya walimu 34 pamoja na Wakuu wao wa Shule 34 kwa niaba ya walimu walipokea kiasi cha Tsh. 9,200,000/=. 

Kundi la nne katika kategoria hii, ilikuwa zawadi zilizotolewa kwa waalimu 958 waliofaulisha masomo yao kwa Daraja "A" ambapo kila mmoja wao alipata zawadi ya Tsh. 30,000/- kwa kila A moja na kufanya jumla ya Tsh.28,740,000/-.Jumla ya fedha zilizotumika kutoa zawadi zote kwenye kategoria ya Mitihani ya kidato cha nne ni Tsh. 46,940,000/=

Pamoja na zawadi tajwa hapo juu Mhe. Kafulila ametoa zawadi nyinginezo zikiwemo Vyeti vya Pongezi na Ngao kwa Shule, Kata na Halmashauri zilizofanya vizuri Kimkoa kwa Mtihani wa Darasa la Nne, Darasa la Saba, Kidato cha Pili na Kidato cha Nne pamoja na Vyeti vya Pongezi kwa Wadau mbalimbali wa Elimu kutokana na Mchango wao wakiwemo Waganga wa Tiba Asili na Tiba Mbadala.

Aidha ili kuongeza hamasa kwa walimu katika kuchapa kazi kwa bidii na maarifa Mhe. Kafulila amesema lengo la mwaka huu 2022 ni kupata alama ''A'' 2000 na kila Mwalimu atakayepata A atalipwa kiasi cha Tsh. 50,000/- kwa kila ''A''  badala ya Tsh.30,000/- kama ilivyo sasa. 

Mhe. Kafulila amewapongeza walimu wote wa mkoa wa Simiyu kwa kuchapa kazi licha ya changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo zikiwemo ukosefu wa nyumba za walimu na miundombinu isiyo rafiki.Mwisho.

Tuesday, March 15, 2022

MKANDARASI APEWA SIKU 7 KABLA MKATABA KUVUNJWA

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. David Kafulila ametoa siku saba kwa Kampuni ya Daska Company Ltd, kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa Barabara ya Byuna/Nkindwabiye/ Halawa barabara yenye  urefu wa 14.9km. Thamani ya mradi/mkataba huo ni Tsh.139.993 mln.

“Tofauti na hapo mkataba uvunjwe na taratibu zifuatwe kupata kampuni nyingine.Sina na sijawahi kuwa na subira kwa wakandarasi wababaishaji. Nitoe wito Wakandarasi wote mkae mguu sawa. Nitafuta kazi zote zinazosuasua ili kubaki na wakandarasi wenye uwezo wa kutekeleza kazi kwa mujibu wa mikataba wanayosaini".Amesema Kafulila.

Kafulila ametoa maelekezo hayo kwa Meneja wa Mkoa wa  Mamlaka ya Barabara vijijini( TARURA) wakati wa ziara yake leo Machi14, 2022 wilaya ya Bariadi. Mwisho.









Thursday, March 10, 2022

Katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, TUGHE-Simiyu Yatoa Msaada Kituo cha Afya Ikindilo.


























Sherehe ya siku wa Wanawake duniani, huadhimishwa kila tarehe nane ya mwezi wa tatu. Katika kuadhimisha sherehe hizo, 2022, kama ilivyo ada Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE-Simiyu), waliamua kufanya matendo ya huruma Wilayani Itilima ambapo ndipo sherehe za siku ya mwanamke kimkoa zimefanyika.

Akiwakaribisha wilayani Itilima Mkurugenzi wa Wilaya ya Itilima, Bi. Elizabeth Gumbo amesema ‘’ninafuraha kubwa niwakaribishe sana Wilaya ya Itilima, Pongezi sana  Kwa Mwenyekiti na katibu wa TUGHE Bi. Elizabeth na  Catherine. Niwaombee baraka za mwenyezi Mungu,niwatie moyo wanawake wenzangu,sisi tunaweza, na tumejionea wazi kabisa kutoka kwa Mama yetu, Rais wetu ambaye ni mwanamama Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwani, kwa Wilaya ya  Itilima tu ametupatia fedha ambazo zimewezesha ujenzi wa vyumba 82 vya madarasa. Hivyo wakina mama sote tuwe na moyo wa kumuunga mkono Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan, tupambane wenyewe, kila mmoja katika nafasi aliyopewa akaonyeshe uwezo wake. Wakina mama tuendelee kuwashauri kina mama wengine, binti zetu, familia, watoto na Taifa letu, kwani wakina mama ni jeshi kubwa’’.

Akielezea sababu za TUGHE-Simiyu, kuchagua eneo hilo na kufanya matendo ya huruma, Mwenyekiti kamati za Wanawake TUGHE Mkoa wa Simiyu,Bi.Elizabeth Nangali Gelege   amesema “ tumeamua kufanya haya matendo ya huruma katika kituo cha afya cha Ikindilo baada ya kufahamishwa na Mganga Mkuu wilaya ya Itilima Dkt. Anorld Musiba, kuwa kituo cha afya Ikindilo kina mahitaji. Tumekuja na mashuka, mama Samia Suluhu Hassan  ameleta  majengo, sisi tumeleta sabuni pamoja na mashuka vyote vikiwa na thamani ya Tsh. Milioni moja. 

Akizungumzia kauli mbiu ya mwaka huu ya siku ya wanawake duniani, ambayo inasema:“Kizazi cha Haki na Usawa Kwa Maendeleo, Tujitokeze Kuhesabiwa’’. Bi. Geleje amesema Kauli mbiu hii inaonyesha wazi kwamba huu ni mwaka wa sensa, hivyo wanawake tujitokeze kuhesabiwa.Kila mwanamke atumie kipaji chake kuhakikisha watu wa familia yake wanahesabiwa na kuendeleza nchi.

Akizungumzia msaada huo Katibu wa TUGHE Mkoa wa Simiyu Bi.Catherine Nyingi amesema katika kuonyesha mshikamano,sisi TUGHE tuna kawaida ya kufanya matendo ya huruma na kurudisha huduma katika jamii.Kama ambavyo tumefanya leo katika kituo hiki cha afya cha Ikindilo.

Akitoa taarifa kuhusu kituo cha afya Ikindilo, Mganga mfawidhi Kituo cha afya Ikindilo Dkt. Elizabeth Malunde amesema Kituo cha afya Ikindilo  ni kimoja kati ya vituo 3 vya afya Wilayani itilima. Kituo hiki kimepanda kutoka daraja namba mbili na sasa kipo namba tatu. 

Kituo cha afya Ikindilo kinatoa huduma mbalimbali kama vile chanjo cha UVIKO,Kliniki ya HIV, tuanafanya tohara kwa watoto wa kiume, tunahudumia wangonjwa wa nje na ndani, poa tunatoa huduma za mama na mtoto. Mwaka jana mwezi wa saba tulifungiwa mfumo wa GhoTomis, hivyo malipo yoye ya huduma za afya yanafanyika kwa kutumia mfumo. Upatikanaji wa Dawa ni  100%, upatikanaji wa damu 100% pia tuna duka la Dawa. 

Pamoja na mafaniko tajwa hapo juu bado tunakabiliwa na  mbalimbali.Changamoto kubwa tuliyo nayo ni kuwa hatuna eneo ila tupo kwenye mchakato wa kutafuta eneo . Pia tuna changamoto ya nyumba za watumishi kwani tuna Nyumba 6 tu na hivyo kufanya watumishi wengine kuishi katika maeneo ya mbali, uchakavu wa majengo, tuna changamoto ya jengo la kulaza wagonjwa- OPD, Changamoto ya watumishi, kituo hakina uzio na hivyo kufanya wanyama kuingia  ndani ya eneo la kituo cha afya,pia hatuna wodi ya kulaza watoto wachanga.Mwisho.

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!