Sunday, March 26, 2017

SULUHU YA MGOGORO WA MWEKEZAJI MWIBA HOLDINGS NA WANANCHI MEATU YAPATIKANA

Hatimaye suluhu ya mgogoro baina ya mwekezaji wa kampuni ya  MWIBA Holdings na wananchi wa vijiji saba vinavyounda Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) ya Makao wilayani Meatu,  juu ya utata wa mkataba wa kumiliki ardhi, uanzishwaji wa ranchi ,mahusiano mabovu  na kusogezwa  kwa alama za mipaka katika makazi ya wananchi  imepatikana

Suluhu hiyo imepatikana baada ya kufanyika kikao cha pamoja wilayani Meatu kati ya Kamati ya Siasa ya CCM, Viongozi na Watendaji wa Serikali (Wilaya ya Meatu na Mkoa wa Simiyu), Mwakilishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Watendaji wa Kampuni ya MWIBA Holdings na Viongozi wa Vijiji vinavyounda Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Makao, ambacho kimeongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka

 Pande zote mbili (Mwekezaji na wananchi) zimekubaliana kuondoa kesi inayohusu mgogoro huo kwa Msuluhishi Jaji Mstaafu Thomas Mihayo na kurejea tena katika meza ya  maridhiano ili kujadili namna ya kuondoa tofauti na dosari zote zilizoonekana awali.

Mtaka ameipongeza Kampuni ya MWIBA Holdings kurejea katika meza ya mariadhiano na wananchi na ameagiza kufanyika mabadiliko katika Menejimenti ya Kampuni hiyo  kwa kuwa baadhi ya watendaji wametajwa kuwa chanzo cha   migogoro  ambayo imekuwa ikiwanufaisha wao wenyewe  huku ikichochea uhasama kati ya kampuni hiyo na wananchi

“....Nawaeleza Wakurugenzi, baadhi ya wasaidizi wenu wanawachafua sana, wanatengeneza migogoro na wananchi wetu kwa manufaa yao wenyewe; mkitaka kufanya kazi na sisi chukueni hatua kwa watumishi wenu, tunataka wawekezaji lakini hatuko tayari kuona wananchi wananyanyaswa kwa namna yoyote ile” alisema Mtaka.

Naye Mbunge wa Jimbo la Meatu Salum Khamis amesema  nia yake ni kuona wananchi hawabugudhiwi hivyo akatoa rai kuwa maridhiano yatakayofanyika kati ya pande hizo mbili yafanyike kwa umakini sana ili makubaliano yatakayofikiwa yalinde haki za wakazi wa Meatu na yasiwe chanzo cha migogoro.

Wakati huo huo baadhi ya wananchi wamesema mipaka waliyoshiriki kuweka wakati wa uanzishwaji wa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) ya Makao, ilitolewa kinyemela na watumishi wakiwemo viongozi wa Jumuiya hiyo kwa kushirikiana na mwekezaji huyo na kusogeza  nyuma alama hizo kwa kilomita 10 kutoka eneo la hifadhi kuelekea eneo la makazi ya wananchi

Wananachi hao wamesema kuwa mipaka ambayo imekuwa ikileta migogoro ni mpaka ulioko katika kijiji cha Bulongoja kwenye bikoni namba 314, ambapo walisema kuwa bikoni hiyo iliondolewa na kusogezwa nyuma zaidi ya kilometa 10 kutoka ndani ya hifadhi kuelekea kwenye makazi yao.

Akitoa ufafanuzi wa suala hilo, Katibu Tawala Mkoa, Ndg.Jumanne Sagini amesema atatuma timu ya wataalam Ngazi ya Mkoa ambao watashirikiana na wataalam wa wilaya ya Meatu watakaokwenda kuhakiki mipaka hiyo  kwa kuzingatia ramani na kuirejesha ilipokuwa, huku akisisitiza wataalam hao kuzingatia weledi.

Kwa upande wake Mkurugenzi kutoka Kampuni ya Mwiba Holdings Company  Abdulkadir Mohamed  amekubali kumaliza mgogoro huo na kufanya mabadiliko ya menejimenti yake  ili waweze  kufanya uwekezaji wa utalii na mazingira kwa uhuru.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Mhe.Dkt.Titus Kamani amewaasa viongozi na watendaji  wa Serikali mkoani humo kutekeleza wajibu wao katika kuwaletea wananchi maendeleo na wasiruhusu kwa namna yoyote migogoro ikachukua nafasi kubwa kuliko maendeleo ya wananchi.

Jumuiya Hifadhi ya wanyamapori (WMA) Makao inaundwa na vijji saba ambavyo ni Makao, Sapa, Mwangudo, Mbushi, Iramba ndogo, Jinamo na Mwabagimu.

 
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na  Kamati ya Siasa ya CCM, Viongozi na Watendaji wa Serikali (Wilaya ya Meatu na Mkoa wa Simiyu), Watendaji wa  Mwekezaji Kampuni ya MWIBA   Holdings na Viongozi wa Vijiji vinavyounda Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Makao(hawapo pichani) katika kikao cha kutafuta suluhu ya mgogoro wa mwekezaji huyo wananchi wilayani Meatu.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM, Viongozi na Watendaji wa Serikali (Wilaya ya Meatu na Mkoa wa Simiyu) na Viongozi wa Vijiji vinavyounda Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Makao wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (hayupo pichani) katika kikao cha kutafuta suluhu ya mgogoro wa mwekezaji wa Kampuni ya MWIBA Holdings  na wananchi wilayani Meatu.
Watendaji wa Kampuni ya  MWIBA Holdings (waliokaa sehemu ya juu) wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (hayupo pichani) katika kikao kilichofanyika  kutafuta suluhu ya mgogoro wa mwekezaji huyo na wananchi wilayani Meatu.
Mbunge wa Jimbo la Meatu Salum Khamis akizungumza na Kamati ya Siasa ya CCM, Viongozi na Watendaji wa Serikali (Wilaya ya Meatu na Mkoa wa Simiyu), Watendaji wa Kampuni ya MWIBA  na Viongozi wa Vijiji vinavyounda Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Makao(hawapo pichani) katika kikao cha kutafuta suluhu ya mgogoro wa mwekezaji huyo wananchi wilayani Meatu.
Mwenyekiti wa kijiji cha Makao akichangia jambo katika kikao kilichofanyika kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro kati ya Kampuni ya MWIBA Holdings na wananchi wa Makao kilichofanyika Wilayani Meatu.
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini akifafanua jambo katika kikao kilichofanyika wilayani Meatu kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro kati ya Kampuni ya MWIBA Holdings na wananchi wa Makao wilayani humo.

Mkuu wa Wilaya ya Meatu,Mhe.Dkt.Joseph Chilongani akifafanua jambo katika kikao kilichofanyika wilayani humo kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro kati ya Kampuni ya MWIBA Holdings na wananchi wa Makao.


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu,Ndg. Fabian Manoza  akifafanua jambo katika kikao kilichofanyika wilayani humo  kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro kati ya Kampuni ya MWIBA Holdings na wananchi wa Makao
Mwenyekiti wa  CCM Mkoa wa Simiyu, Dkt. Titus Kamani akifafanua jambo katika kikao kilichofanyika wilayani Meatu kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro kati ya Kampuni ya MWIBA na wananchi wa Makao wilayani humo.
Mkurugenzi kutoka Kampuni ya MWIBA Holding, Ndg. Abdulkadir Mohamed akifafanua jambo katika kikao kilichofanyika wilayani humo kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro kati ya Kampuni hiyo na wananchi wa Makao-Meatu.

): Katibu wa CCM Mkoa wa Simiyu, Joyce Masunga akifafanua jambo katika kikao kilichofanyika wilayani Meatu kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro kati ya Kampuni ya MWIBA na wananchi wa Makao wilayani humo, (kulia) Mwenyekiti wa CCM Meatu, Mhe.Juma Mwibuli.
Katibu wa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Makao, Robert Simon akiwasilsha taarfa ya Jumuiya hiyo katika kilichofanyika wilayani Meatu kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro kati ya Kampuni hiyo na wananchi wa Makao-Meatu.
Baadhi ya wananchi wakitoa maelezo ya kusogezwa kinyemela kwa mipaka ya Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Makao tofauti na ile ya awali walioshuhudia ikiwekwa wakati wa uanzishwaji wa jumuiya hiyo, katika kikao ilichofanyika kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro kati ya Kampuni hiyo na wananchi wa Makao-Meatu.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) na Mbunge wa Jimbo la Kisesa wilaya ya Meatu akichangia jambo katika kikao kilichofanyika wilayani humo kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro kati ya Kampuni ya MWIBA na wananchi wa Makao wilayani humo.

Friday, March 24, 2017

RAS Sagini: Viongozi, Watumishi Shirikianeni na Wadau Kuboresha Huduma Za Afya

Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg. Jumanne Sagini  ametoa wito  kwa viongozi na watumishi mkoani humo kushirikiana na wadau mbalimbali wenye nia njema ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika uboreshaji wa huduma za afya kwa wananchi.

Sagini ameyasema hayo leo katika ufunguzi wa kikao cha kuutambulisha Mradi wa USAID Boresha Afya, kilichofanyika katika Ukumbi wa Kanisa Katoliki Mjini Bariadi.

Amesema Simiyu ni miongoni mwa mikoa saba ambayo Mradi wa USAID Boresha Afya utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano (2017-2022), hivyo akawataka viongozi na wataalam kushirikiana na wadau hao kuhakikisha mradi huu unasaidia kubadilisha mfumo wa utoaji huduma za afya katika maeneo yaliyobainishwa.  

Aidha, ameongeza kuwa ujio wa Mradi huu katika Halmashauri zote za Mkoa wa Simiyu uwe ni chachu ya kuhakikisha huduma za Afya zinapatikana kirahisi kwa wananchi wa Mkoa huo.

“Ndugu washiriki nichukue nafasi hii kushukuru mashirika na wadau mbalimbali wanaounga mkono juhudi za Serikali, natoa wito kwa Idara ya Afya Mkoa na wilaya kutoa ushirikiano wa karibu kuhakikisha mradi huu unafanikiwa na unatoa matunda tarajiwa”

Sagini amesema Serikali inafanya juhudi za kukabiliana na viashiria visivyoridhisha katika utoaji huduma za afya ikiwemo kupunguza vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi ambavyo vinafikia 556 kwa kila vizazi hai 100,000 kwa sasa.

“Vifo hivi vinachangiwa na mambo mengi, ikiwemo mahudhurio hafifu ya wajawazito kliniki katika theluthi ya kwanza ya mimba kwa asilimia 24 na wajawazito wanaohudhuria kliniki kwa mahudhurio manne au zaidi kwa asilimia 51” amesema Sagini.

Sagini amesisitiza kuwa mafanikio katika suala la kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi halitatatuliwa na sekta ya Afya pekee bali kwa ushirikiano wa sekta zote za maendeleo.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Simiyu, Dkt.Fredrick Mlekwa amesema Mradi huu umekuja katika wakati muafaka ambao mkoa unafanya jitihada mbalimbali za kukabiliana na vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wadogo chini ya miaka mitano.

Naye Dkt.Joseph Masenga kutoka USAID Boresha Afya amesema mradi huo katika mkoa wa Simiyu utajikita kuunga mkono juhudi za Serikali katika huduma za uzazi wa mpango, Malaria, Huduma za Afya ya Mtoto, huduma za Uzazi, Lishe na maeneo mengine mtambuka ikiwemo jinsia, heshima na ushirikishwaji wa jamii katika huduma za Afya (ngazi ya jamii).

Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa USAID Boresha Afya wa Mkoa wa Simiyu , Dkt. Charles Suka amesema utambulisho wa mradi huo umefanyika kwa viongozi na watendaji wa mkoa huo ili wawe na uelewa wa pamoja ili waweze kutoa mchango katika utengenezaji wa mpango mkakati wa kupunguza vifo vya mama na mtoto na kuweka mpango wa utekelzaji wa  wa mradi kwa miaka mitano.


Mradi wa USAID Boresha Afya Mkoani Simiyu, unatekelezwa kwa ubia wa mashirika ya Jhpiego, Engenderhealth katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na Magharibi ambayo ni Simiyu, Mara,Kagera, Kigoma, Shinyanga, Geita na Mwanza katika kipindi cha miaka mitano(2017-2022).
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg. Jumanne Sagini  akizungumza na Viongozi na Wataalam wa Afya mkoani humo (hawapo pichani) katika ufunguzi wa kikao cha kuutambulisha Mradi wa USAID Boresha Afya, kilichofanyika leo  katika Ukumbi wa Kanisa Katoliki Mjini Bariadi
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dkt.Mageda Kihulya akizungumza na Viongozi na Wataalam wa Afya mkoani humo (hawapo pichani) katika ufunguzi wa kikao cha kuutambulisha Mradi wa USAID Boresha Afya, kilichofanyika leo  katika Ukumbi wa Kanisa Katoliki Mjini Bariadi
Viongozi na Wataalam wa Afya mkoani Simiyu wakimsikiliza Katibu Tawala Mkoa wa Mkoa huo, Ndg. Jumanne Sagini (hayupo pichani)  katika ufunguzi wa kikao cha kuutambulisha Mradi wa USAID Boresha Afya, kilichofanyika leo katika Ukumbi wa Kanisa Katoliki Mjini Bariadi
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg. Jumanne Sagini (wa nne kushoto)  akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi na Wataalam wa Afya mkoani humo baada ya ufunguzi wa kikao cha kuutambulisha Mradi wa USAID Boresha Afya, kilichofanyika leo katika Ukumbi wa Kanisa Katoliki Mjini Bariadi

Wednesday, March 15, 2017

Viongozi na Watendaji Watakiwa kutowabugudhi Wafanyabiashara

Na Stella Kalinga

Serikali imewataka viongozi wa kisiasa pamoja na watendaji wa Serikali kutotumia vibaya madaraka yao kwa kuwanyanyasa na kuwasumbua wafanyabishara hasa wazawa waliowekeza ndani ya nchi.

Kauli hiyo imetolewa leo na Katibu mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda akiwa mkoani Simiyu, wakati wa Mkutano wa Uzinduzi wa Mwongozo wa Uwekezaji wa mkoa pamoja na Tovuti ya Mkoa.

Profesa Mkenda amesema viongozi hao wanatakiwa kuwajengea wafanyabiashara mazingira rafiki yatakayowawezesha kufanya biashara zao kwa amani ili kuweza kukuza uchumi wa Taifa na kuongeza ajira kwa vijana.

Aidha, amewasihi viongozi wote wa Serikali ngazi za Mikoa na wilaya hapa nchini  kujivunia uwepo wa wajasiriamali na wafanyabiashara wakubwa ambao ni wazawa kwani wao ni chachu ya kuongezeka kwa ajira za vijana.

Amesema kuwa si vyema wafanyabishara kutukanwa, kutolewa lugha zisizokuwa sahihi na kuonekana kama wana uadui na Serikali, badala yake watengenezewe mazingira mazuri  ili waweze kulipa kodi na kufuata sheria na taratibu za nchi.

“ Hawa wafanyabishara hasa wazawa na wajasiliamali tuwaone kama wenzetu, ndugu zetu na watu muhimu, kwani wameajiri vijana wetu, wanalipa kodi ili nchi ipate maendeleo, lakini wanatekeleza kauli mbiu ya Rais , Tanzania kuwa nchi ya viwanda, tuwathamni” alisema Adolf.

Mbali na hilo Katibu Mkuu huyo amezitaka Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinatenga maeneo kwa ajili ya wawekezaji wakubwa na wadogo kwa ajili ya kujenga viwanda.

Awali akiongea katika Mkutano huo Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema kuwa ili Tanzania iweze kufanikiwa katika azma yake ya kuwa na viwanda lazima Serikali iwekeze kwanza katika utafiti wa fursa zilizopo.

Mtaka amesema kuwa kuwekeza katika utafiti kutasaidia kutoa uthubutu wa kufanya na kutenda mambo mbalimbali yatakayoifanya nchi kuwa na uchumi wa kati na kuwaletea wananchi maendeleo.

“ Nchi hii tusingelihitaji kuona wakuu wa mikoa kuwa wabobezi katika kila sekta na badala yake wawaache wataalam na watafiti wafanye kazi zao kitaalamu ili kuepuka mvurugano wa shughuli za kimaendeleo ndani ya nchi” amesema Mtaka.

Kwa upande wake Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Masuala Kiuchumi na Kijamii (ESRF) Dk Gratian Bamwenda, amesema kukamilika kwa utafiti huo ambao umetoa mwongozo wa uwekezaji mkoani Simiyu kutatoa fursa kwa wananchi na wafanyabishara kutambua fursa na kuwekeza.


Mwongozo wa Uwekezaji Mkoani Simiyu ambao umezinduliwa rasmi leo ni matokeo ya Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Masuala Kiuchumi na Kijamii (ESRF) katika halmashauri zote sita za mkoa wa Simiyu chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa(UNDP); umebainisha takribani fursa 26 za uwekezaji katika sekta zote muhimu mkoani humo.
Katibu mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda(wa pili kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(wa pili kulia) wakionesha Mwongozo wa Uwekezaji Mkoani Simiyu kwa wadau wa Maendeleo wa Mkoa huo mara baada ya uzinduzi uliofanyika Machi, 15, Mjini Bariadi.
Katibu mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka wakiwa wameshika nakala za Mwongozo wa Uwekezaji ikiwa ni maandalizi ya kufanya uzinduzi wa mwongozo huo Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(katika) akizungumza jambo na Katibu mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda(kuhoto) na Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa kiuchumi na Kijamii(ESRF),Dkt.Tausi Kida (kulia)wakati wa Mkutano wa Uzinduzi wa Mwongozo wa Uwekezaji Mkoani Simiyu uliotokana na Utafiti wa Taasisi hiyo.
Katibu mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda akizungumza na Viongozi, watendaji na wadau wa maendeleo wa Mkoa wa Simiyu (hawapo pichani) wakati wa Mkutano wa Uzinduzi wa Mwongozo wa Uwekezaji Mkoani humo.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa kiuchumi na Kijamii(ESRF),Dkt.Tausi Kida akizungumza na Viongozi, watendaji na wadau wa maendeleo wa Mkoa wa Simiyu (hawapo pichani) wakati wa Mkutano wa Uzinduzi wa Mwongozo wa Uwekezaji Mkoani humo.
Mbunge wa Jimbo la Itilima ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Mkoani Simiyu, Mhe.Njalu Silanga akichangia jambo katika mkutano wa Uzinduzi wa Mwongozo wa Uwekezaji Mkoani Simiyu Uliofanyika leo Mjini Bariadi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Dkt. Fredrick Sagamiko akichangia jambo katika mkutano wa Uzinduzi wa Mwongozo wa Uwekezaji Mkoani Simiyu Uliofanyika Mjini Bariadi.
 Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, Mhe. Mashimba Ndaki akichangia jambo katika mkutano wa Uzinduzi wa Mwongozo wa Uwekezaji Mkoani Simiyu Uliofanyika Mjini Bariadi.

Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa(UNDP) Hawa Dabo akizungumza na Viongozi, watendaji na wadau wa maendeleo wa Mkoa wa Simiyu ( baadhi hawapo pichani) wakati wa Mkutano wa Uzinduzi wa Mwongozo wa Uwekezaji Mkoani humo.
Kaimu Afisa TEHAMA wa Sekretarieti ya Mkoa, Bw.Edgar Mdemu(kushoto)  akimuonesha  Katibu mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda(wa pili kushoto) na viongozi wengine Tovuti ya Mkoa wa Simiyu, inayotambulika kwa anuani ya www.simiyu.go.tz kabla ya kuizindua leo Mjini Bariadi.
Baadhi ya Viongozi wakimsikiliza Katibu mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda( hayupo pichani) katika mkutano wa Uzinduzi wa Mwongozo wa Uwekezaji Mkoani Simiyu Uliofanyika Mjini Bariadi.
Baadhi ya wadau wa maendeleo wa Mkoa wa Simiyu wakimsikiliza Katibu mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda( hayupo pichani) katika mkutano wa Uzinduzi wa Mwongozo wa Uwekezaji Mkoani Simiyu Uliofanyika Mjini Bariadi.
Katibu mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda ( wa nne kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Mkoa wa Simiyuna baadhi ya wadau wa maendeo wa mkoa huo mara baada ya uzinduzi wa Mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa huo Mjini Bariadi.

Monday, March 13, 2017

TAARIFA KWA UMMA

 

                               TAARIFA KWA UMMA
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka anawaalika wananchi na wadau wote wa maendeleo katika Uzinduzi wa Mwongozo wa Uwekezaji mkoani Simiyu utakaofanyika tarehe 15 Machi 2017, katika Ukumbi wa Kanisa Katoliki Mjini Bariadi kuanzia saa 3:00 asubuhi.

Mgeni rasmi katika uzinduzi huo ni Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Prof. Adolf Mkenda

Mwongozo wa uwekezaji Mkoani SIMIYU unabainisha fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo Mkoani humo na utaongoza uandaaji na utekelezaji wa Mipango ya Maendeleo ya Mkoa na Halmashauri zake.

Aidha, Mwongozo unakusudia kutekeleza azma ya Serikali ya Tanzania ya Viwanda  kama ilivyofafanuliwa katika Mpango wa pili wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano (2016/2017 – 2020/2021) na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.

Pamoja na mambo mengine mpango huu unabainisha taarifa mahususi kwa makampuni na watu binafsi kutoka ndani na nje nchi, wenye nia ya kuwekeza  katika maeneo yenye rasilimali nyingi ambazo hazijaanza kutumika (untapped resources) ili kukuza uwezo wa uzalishaji katika sekta zote muhimu Mkoani Simiyu.

Mwongozo huu ni matokeo ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF) Januari - Februari 2017, katika Halmashauri zote za Mkoa wa Simiyu (Bariadi Vijijini, Bariadi Mjini, Busega, Itilima,Maswa na Meatu) kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP)

Imetolewa na:
Stella A. Kalinga
Afisa Habari Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Simiyu
13 Machi, 2017.



Friday, March 3, 2017

DC BARIADI:ASKARI WANAOJIHUSISHA NA UJANGILI WACHUKULIWE HATUA

Na Stella Kalinga
Serikali Mkoani Simiyu imetoa wito kwa Taasisi zinazoshughulika na Ulinzi na Hifadhi ya Wanyamapori kuwachukulia hatua askari Wanyamapori wanaojihusisha kwa namna moja ama nyingine  na vitendo vya Ujangili.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Festo Kiswaga ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bariadi katika Maadhimisho ya Siku ya Wanyamapori duniani, yaliyofanyika Mjini Bariadi, ambayo yameenda sambamba na zoezi la upandaji miti katika Hospitali Teule ya Mkoa(Somanda).

Kiswaga amesema baadhi ya askari wanyamapori wamekuwa wakivujisha siri za kukabiliana na majangili hali inayosababisha Serikali kupata hasara kutokana na ujangili kuongezeka na hivyo ameshauri askari hao kuchukuliwa hatua bila kuonewa haya.

 “Upo udhaifu kwa baadhi ya  walinzi na askari ambao tumewapa dhamana ya kulinda wanyamapori, nitoe tu wito kwamba viongozi waandamizi wa taasisi hizi kwa maana ya TANAPA, Vikosi vya kuzuia Ujangili, itakapotokea kiongozi au askari  yeyote ana mahusianao na hawa amabao ni majangili achukuliwe hatua” amesema.

Ameongeza kuwa pamoja na Serikali kuwawezesha askari wanyamapori kwa silaha za kivita ili kupambana na majangili,  upo umuhimu wa kuwaongezea mafunzo na kuona namna ya kuongeza vikosi vya Intelejensia vitakavyosaidia kuwakamata majangili kabla hawajafanya uharibifu katika hifadhi.

Aidha, Kiswaga ameomba Mashirika yasiyo ya Kiserikali kusaidia vikundi na taasisi zinazijitolea kuelimisha jamii kuondokana na ujangili ili elimu hii iwafikie wananchi wote  kwa ajili ya kuwasaidia kuona umuhimu wa kulinda wanyamapori kwa manufaa yao na Taifa wa ujumla.

Vile vile Kiswaga amewashauri wakazi wa Mkoa wa Simiyu kutumia vizuri fursa ya kuwa karibu na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa kujenga hoteli za kitalii, kufanya kazi za sanaa zitazonunuliwa na watalii pamoja na kuanzisha vilabu vya kupinga masuala ya ujangili kwa ajili ya kujiletea maendeleo yao na ya mkoa kwa ujumla.

Sambamba na hilo amesisitiza wananchi kuendelea kupanda miti ili kukabiliana na hali ya jangwa na mabadiliko ya Tabia nchi na kuiomba Taasisi ya RAFIKI Wildlife Foundation kuona namna ya kuongeza idadi ya miti katika maadhimisho yajayo.

Naye Mkuu wa Kanda ya Serengeti kutoka Kikosi cha Kuzui Ujangili, Ndg. Said Hassan Mkeni amesema Maadhimisho ya Siku ya wanyamapori imeenda sambamba na upandaji miti kwa sababu miti ni chakula cha wanyamapori, vile vile inasaidia kupata mvua na kuhifadhi mazingira.


Kauli mbiu ya Siku ya Wanyamapori Duniani Mwaka 2017 ambayo yamefanyika Mkoani Simiyu kwa Ufadhili wa Shirika lisilo la Kiserikali la RAFIKI Wildlife Foundation ni “ SIKILIZA SAUTI YA VIJANA KWA UHIFADHI” 
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Simiyu ambaye pia Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mhe Festo Kiswaga akipanda mti katika Hospitali ya Mkoa wa Simiyu(Somanda), katika maadhimisho ya Siku ya Wanyamapori iliyofanyika Mjini Bariadi.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mhe Festo Kiswaga akizungumza na Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ,Hospitali ya Mkoa  na wananchi, katika maadhimisho ya Siku ya Wanyamapori yaliyofanyika Mjini Bariadi.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Mhandisi.Hatari Kapufi akizungumza na Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ,Hospitali ya Mkoa  na wananchi, katika maadhimisho ya Siku ya Wanyamapori yaliyofanyika Mjini Bariadi.
Mkuu wa Kanda ya Serengeti kutoka Kikosi cha Kuzui Ujangili, Ndg. Said Hassan Mkeni akizungumza na Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ,Hospitali ya Mkoa  na wananchi, katika maadhimisho ya Siku ya Wanyamapori yaliyofanyika Mjini Bariadi.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Simiyu ambaye pia Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mhe Festo Kiswaga akisaini Kitabu cha Wageni katika Hospitali ya Mkoa wa Simiyu(Somanda), wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanyamapori iliyofanyika Mjini Bariadi.
Baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Hospitali ya Mkoa wakipanda mti katika Hospitali ya Mkoa wa Simiyu(Somanda), katika maadhimisho ya Siku ya Wanyamapori iliyofanyika Mjini Bariadi.
Baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Hospitali ya Mkoa wakipanda mti katika Hospitali ya Mkoa wa Simiyu(Somanda), katika maadhimisho ya Siku ya Wanyamapori iliyofanyika Mjini Bariadi.

Wednesday, March 1, 2017

WANANCHI WAOMBWA KUTOA USHIRIKIANO KWA WATAFITI VIASHIRIA NA MATOKEO YA UKIMWI

Na Stella Kalinga
Serikali Mkoani Simiyu  imetoa wito kwa wananchi na wadau mbalimbali Mkoani humo kutoa ushirikiano kwa  wataalam wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi(Tanzania HIV Impact Survey-THIS)  ili takwimu zitakazopatikana  ziendane na hali halisi ya mkoa.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mhe.Festo Kiswaga  wakati  akisoma hotuba kwa Niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka  leo mjini Bariadi , katika mkutano wa wadau wa Utafiti huo unaotarajiwa kufanyika mwezi Machi mwaka huu Mkoani humo.

Amesema kwa kuwa utafiti huo unafanyika katika ngazi ya kaya kwa kuzingatia sampuli iliyopendekezwa na Wataalam   ambapo  amesisitiza elimu itolewe kwa familia zitakazochaguliwa kupimwa ili ziwe tayari kupima na kupokea majibu.

“Mtakubaliana nami kwamba sera na mipango bora hutegemea upatikanaji wa takwimu sahihi na bora , hivyo nitoe wito kwa wadau wote wa mkoa wetu kutoa ushirikiano wa karibu kwa watafiti ili kufanikisha zoezi hili muhimu kwa Taifa letu” alisema.

Akitoa ufafanuzi wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi Mkoani Simiyu, Bibi.Mihayo Bupamba  kutoka Shirika lisilo la Kiserikali la ICAP amesema utafiti utafanyika katika ngazi ya kaya kupitia sampuli (baadhi ya kaya) zilizochaguliwa kwenye maeneo tisa (09) kutoka wilaya zote mkoani humo, ambapo amesisitiza kuwa utafiti huo utahusisha upimaji wa hiari wa Virusi vya Ukimwi, Homa ya Ini na Kaswende baada ya watafiti kuzungumza na walengwa.

Bupamba amesema  utafiti huu unalenga kukusanya taarifa za maambukizi mapya ya VVU, kiwango cha VVU mwilini kwa wanaoishi na VVU, wastani wa maambukizi ya VVU kwa watu wa rika zote,wingi wa chembechembe za kinga mwilini (CD4 T-cell count), viashiria vya usugu wa dawa,na kiwango cha maambukizi ya kaswende na homa ya ini kwa watu wenye umri wa miaka 15 na zaidi.

Ameongeza kuwa utafiti huo pia unatarajia kukusanya taarifa za upatikanaji na utumiaji wa huduma zitolewazo katika kudhibiti maambukizi ya VVU na UKIMWI na viashiria vya tabia hatarishi zinazochangia maambukizi ya VVU ambayo kwa mujibu wa tafiti zilizopita inaonekana kupungua kutoka asilimia 7 mwaka 2013 mpaka asilimia 5.1 mwaka 2011.

“ Utafiti wa awamu hii ni wa tofauti na tafizi zilizofanyika miaka ya nyuma, unahusisha watu wa rika zote katika kaya zilizochaguliwa... na wote wataopima watapewa matokeo yao papo hapo”alisema

Bupamba amesema kupitia utafiti huo kaya/ familia zitatambua hali zao kiafya na wale watakaokutwa na maambukizi wataanzishiwa huduma za matibabu,kusisitiza kuwa pia Serikali itapata takwimu zitakazotumika kupanga sera na mipango mbalimbali kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Wakizungumza katika mkutano huo Wawakilishi wa Madhehebu ya Dini Sheikh wa Mkoa wa Simiyu, Mahamoud Kalokola na Mchungaji wa Kanisa la AICT, Josephati Magori wamesema viongozi wa dini watatoa ushirikiano kwa watafiti katika kuwahamasiha wananchi na wakawataka  watafiti hao kuwashirikisha viongozi wa dini hususani katika ngazi ya Kata na Vijiji au Mitaa kila watakapofanya utafiti.

Naye  Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini amewahakikishia wataalam na watafiti wote kuwa Serikali na Watendaji mkoani humo itatoa ushirikiano wa dhati kila watakapohitajika.
Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi ambao umeshaanza kutekelezwa kwa baadhi ya mikoa utatekelezwa  nchi nzima katika maeneo 525 utazifikia  kaya 16,000 wananchi 42, 000 ambapo kati ya hao watoto ni 8,000.

Mkutano wa wadau wa utafiti huo umewahusisha viongozi wa Serikali ngazi ya mkoa na Wilaya, watendaji wakiwepo waratibu wa ukimwi Mkoa na Wilaya, watakwimu, maafisa maendeleo  ya jamii, viongozi wa madhehebu ya dini wadau wengine kutoka mashirika yasiyo ya Kiserikali.

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mhe.Festo Kiswaga(wa pili kulia)  akizungumza na wadau wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi mjini Bariadi leo, kwa Niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu utafiti unatarajiwa kuanza mwezi huu.
Baadhi ya Viongozi na Watendaji wa Serikali,viongozi wa Dini na wadau wengine wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi, wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga katika mkutano uliofanyika leo mjini Bariadi.
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini akizungumza na wadau wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi katika Mkutano uliofanyika leo mjini Bariadi , utafiti ambao unatarajiwa kuanza kufanyika Mkoani Humo mwezi huu.
Mdau wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi  Bibi.Mihayo Bupamba  kutoka Shirika lisilo la Kiserikali la ICAP akiwasilisha mada kwa wadau wa utafiti huo mkoani Simiyu katika mkutano uliofanyika Mjini Bariadi.

Sheikh wa Mkoa wa Simiyu,Mahamoud Kalokola akichangia mada katika mkutano wa wadau w Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi mkoani humo katika mkutano uliofanyika Mjini Bariadi.






Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!