Na Stella Kalinga
Serikali
Mkoani Simiyu imetoa wito kwa wananchi na
wadau mbalimbali Mkoani humo kutoa ushirikiano kwa wataalam wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo
ya Ukimwi(Tanzania HIV Impact Survey-THIS) ili takwimu zitakazopatikana ziendane na hali halisi ya mkoa.
Wito
huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mhe.Festo Kiswaga wakati
akisoma hotuba kwa Niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka leo mjini Bariadi , katika mkutano wa wadau wa
Utafiti huo unaotarajiwa kufanyika mwezi Machi mwaka huu Mkoani humo.
Amesema
kwa kuwa utafiti huo unafanyika katika ngazi ya kaya kwa kuzingatia sampuli
iliyopendekezwa na Wataalam ambapo amesisitiza elimu itolewe kwa familia zitakazochaguliwa
kupimwa ili ziwe tayari kupima na kupokea majibu.
“Mtakubaliana
nami kwamba sera na mipango bora hutegemea upatikanaji wa takwimu sahihi na
bora , hivyo nitoe wito kwa wadau wote wa mkoa wetu kutoa ushirikiano wa karibu
kwa watafiti ili kufanikisha zoezi hili muhimu kwa Taifa letu” alisema.
Akitoa
ufafanuzi wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi Mkoani Simiyu, Bibi.Mihayo
Bupamba kutoka Shirika lisilo la
Kiserikali la ICAP amesema utafiti utafanyika katika ngazi ya kaya kupitia
sampuli (baadhi ya kaya) zilizochaguliwa kwenye maeneo tisa (09) kutoka wilaya
zote mkoani humo, ambapo amesisitiza kuwa utafiti huo utahusisha upimaji wa
hiari wa Virusi vya Ukimwi, Homa ya Ini na Kaswende baada ya watafiti
kuzungumza na walengwa.
Bupamba
amesema utafiti huu unalenga kukusanya
taarifa za maambukizi mapya ya VVU, kiwango cha VVU mwilini kwa wanaoishi na
VVU, wastani wa maambukizi ya VVU kwa watu wa rika zote,wingi wa chembechembe
za kinga mwilini (CD4 T-cell count), viashiria vya usugu wa dawa,na kiwango cha
maambukizi ya kaswende na homa ya ini kwa watu wenye umri wa miaka 15 na zaidi.
Ameongeza
kuwa utafiti huo pia unatarajia kukusanya taarifa za upatikanaji na utumiaji wa
huduma zitolewazo katika kudhibiti maambukizi ya VVU na UKIMWI na viashiria vya
tabia hatarishi zinazochangia maambukizi ya VVU ambayo kwa mujibu wa tafiti zilizopita
inaonekana kupungua kutoka asilimia 7 mwaka 2013 mpaka asilimia 5.1 mwaka 2011.
“
Utafiti wa awamu hii ni wa tofauti na tafizi zilizofanyika miaka ya nyuma,
unahusisha watu wa rika zote katika kaya zilizochaguliwa... na wote wataopima
watapewa matokeo yao papo hapo”alisema
Bupamba
amesema kupitia utafiti huo kaya/ familia zitatambua hali zao kiafya na wale
watakaokutwa na maambukizi wataanzishiwa huduma za matibabu,kusisitiza kuwa pia
Serikali itapata takwimu zitakazotumika kupanga sera na mipango mbalimbali kwa
manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Wakizungumza
katika mkutano huo Wawakilishi wa Madhehebu ya Dini Sheikh wa Mkoa wa Simiyu,
Mahamoud Kalokola na Mchungaji wa Kanisa la AICT, Josephati Magori wamesema viongozi
wa dini watatoa ushirikiano kwa watafiti katika kuwahamasiha wananchi na
wakawataka watafiti hao kuwashirikisha
viongozi wa dini hususani katika ngazi ya Kata na Vijiji au Mitaa kila watakapofanya
utafiti.
Naye
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu,
Ndg.Jumanne Sagini amewahakikishia wataalam na watafiti wote kuwa Serikali na
Watendaji mkoani humo itatoa ushirikiano wa dhati kila watakapohitajika.
Utafiti
wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi ambao umeshaanza kutekelezwa kwa baadhi ya
mikoa utatekelezwa nchi nzima katika
maeneo 525 utazifikia kaya 16,000 wananchi
42, 000 ambapo kati ya hao watoto ni 8,000.
Mkutano
wa wadau wa utafiti huo umewahusisha viongozi wa Serikali ngazi ya mkoa na
Wilaya, watendaji wakiwepo waratibu wa ukimwi Mkoa na Wilaya, watakwimu,
maafisa maendeleo ya jamii, viongozi wa
madhehebu ya dini wadau wengine kutoka mashirika yasiyo ya Kiserikali.
0 comments:
Post a Comment