Serikali imewataka viongozi wa kisiasa pamoja na watendaji wa Serikali
kutotumia vibaya madaraka yao kwa kuwanyanyasa na kuwasumbua wafanyabishara
hasa wazawa waliowekeza ndani ya nchi.
Kauli hiyo imetolewa leo na Katibu mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na
Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda akiwa mkoani Simiyu, wakati wa Mkutano wa
Uzinduzi wa Mwongozo wa Uwekezaji wa mkoa pamoja na Tovuti ya Mkoa.
Profesa Mkenda amesema viongozi hao wanatakiwa kuwajengea wafanyabiashara
mazingira rafiki yatakayowawezesha kufanya biashara zao kwa amani ili kuweza
kukuza uchumi wa Taifa na kuongeza ajira kwa vijana.
Aidha, amewasihi viongozi wote wa Serikali ngazi za Mikoa na wilaya hapa nchini kujivunia
uwepo wa wajasiriamali na wafanyabiashara wakubwa ambao ni wazawa kwani wao ni
chachu ya kuongezeka kwa ajira za vijana.
Amesema kuwa si vyema wafanyabishara kutukanwa, kutolewa lugha zisizokuwa
sahihi na kuonekana kama wana uadui na Serikali, badala yake watengenezewe
mazingira mazuri ili waweze kulipa kodi na
kufuata sheria na taratibu za nchi.
“ Hawa wafanyabishara hasa wazawa na wajasiliamali tuwaone kama wenzetu,
ndugu zetu na watu muhimu, kwani wameajiri vijana wetu, wanalipa kodi ili nchi
ipate maendeleo, lakini wanatekeleza kauli mbiu ya Rais , Tanzania kuwa nchi ya
viwanda, tuwathamni” alisema Adolf.
Mbali na hilo Katibu Mkuu huyo amezitaka Halmashauri zote nchini
kuhakikisha zinatenga maeneo kwa ajili ya wawekezaji wakubwa na wadogo kwa
ajili ya kujenga viwanda.
Awali akiongea katika Mkutano huo Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony
Mtaka amesema kuwa ili Tanzania iweze kufanikiwa katika azma yake ya kuwa na
viwanda lazima Serikali iwekeze kwanza katika utafiti wa fursa zilizopo.
Mtaka amesema kuwa kuwekeza katika utafiti kutasaidia kutoa uthubutu wa
kufanya na kutenda mambo mbalimbali yatakayoifanya nchi kuwa na uchumi wa kati
na kuwaletea wananchi maendeleo.
“ Nchi hii tusingelihitaji kuona wakuu wa mikoa kuwa wabobezi katika kila
sekta na badala yake wawaache wataalam na watafiti wafanye kazi zao kitaalamu
ili kuepuka mvurugano wa shughuli za kimaendeleo ndani ya nchi” amesema Mtaka.
Kwa upande wake Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Masuala Kiuchumi na Kijamii
(ESRF) Dk Gratian Bamwenda, amesema kukamilika kwa utafiti huo ambao umetoa
mwongozo wa uwekezaji mkoani Simiyu kutatoa fursa kwa wananchi na
wafanyabishara kutambua fursa na kuwekeza.
Mwongozo wa Uwekezaji Mkoani Simiyu ambao umezinduliwa rasmi leo ni matokeo
ya Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Masuala Kiuchumi na Kijamii (ESRF)
katika halmashauri zote sita za mkoa wa Simiyu chini ya ufadhili wa Shirika la
Maendeleo la Umoja wa Mataifa(UNDP); umebainisha takribani fursa 26 za
uwekezaji katika sekta zote muhimu mkoani humo.
Mwakilishi wa Shirika la
Maendeleo la Umoja wa Mataifa(UNDP) Hawa Dabo akizungumza na Viongozi,
watendaji na wadau wa maendeleo wa Mkoa wa Simiyu ( baadhi hawapo pichani) wakati
wa Mkutano wa Uzinduzi wa Mwongozo wa Uwekezaji Mkoani humo.
Kaimu Afisa TEHAMA wa
Sekretarieti ya Mkoa, Bw.Edgar Mdemu(kushoto) akimuonesha Katibu mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na
Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda(wa pili kushoto) na viongozi wengine Tovuti ya Mkoa
wa Simiyu, inayotambulika kwa anuani ya www.simiyu.go.tz
kabla ya kuizindua leo Mjini Bariadi.
Baadhi ya Viongozi
wakimsikiliza Katibu mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf
Mkenda( hayupo pichani) katika mkutano wa Uzinduzi wa Mwongozo wa Uwekezaji
Mkoani Simiyu Uliofanyika Mjini Bariadi.
Baadhi ya wadau wa
maendeleo wa Mkoa wa Simiyu wakimsikiliza Katibu mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara
na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda( hayupo pichani) katika mkutano wa Uzinduzi wa
Mwongozo wa Uwekezaji Mkoani Simiyu Uliofanyika Mjini Bariadi.
Katibu mkuu Wizara ya Viwanda,
Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda ( wa nne kushoto) akiwa katika picha
ya pamoja na viongozi wa Mkoa wa Simiyuna baadhi ya wadau wa maendeo wa mkoa huo mara
baada ya uzinduzi wa Mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa huo Mjini Bariadi.
0 comments:
Post a Comment