Saturday, January 20, 2018

WAKUU WA IDARA ELIMU WAKATAKIWA KUSAIDIA JAMII KUONDOKANA NA MILA ZILIZOPITWA NA WAKATI

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka ametoa wito kwa Wakuu wa Idara za Elimu Msingi na Sekondari Halmashauri za Wilaya kuisadia jamii kuondokana na mila zilizopitwa na wakati.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu ametoa wito huo katika tathimini ya elimu iliyofanyika katika Shule ya Msingi Lukungu Wilayani Busega.
  
Ni kikao cha tathimini ya elimu Mkoa wa SIMIYU kilichowakutanisha  maafisa elimu na wakuu wa idara wa Halmashauri SITA chenye lengo la kufanya  taathimini ya kitaaluma na mikakati ya ufaulu wa mitihani ijayo ya kitaifa.

Akizungumza kwenye kikao hicho Mkoa wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka anasema tathimini ya matokeo ya elimu ilenge kuangalia changamoto zinazowakabili walimu sambamba na kuleta mabadiliko katika jamii.

Amesema jukumu lililombele yao ni kuhakikisha wanaibadilisha jamii ya Simiyu ili iondokane na mila potofu zilizopitwa na wakati ikiwemo ya kuwaadhibu walimu hadharani  kwa kuwatandika viboko almaarufu dagashida.

Kuhusu  Wilaya ya MEATU kufanya vibaya katika mitihani ya kitaifa ya darasa la saba na darasa la nne 2017 amewataka kuhakikisha wanabadilika ili kuuwezesha mkoa wa simiyu kuingia kumi bora kitaifa.

‘Meatu punguzeni kuwa mkia mnatuaibisha jitihidini muondoke huko alisema Mtaka.

Kwa upande wake Afisa Elimu wa Mkoa wa Simiyu, Julius Nestory  amesema pamoja na changamoto zilizopo katika sekta elimu lakini ufaulu umekuwa  ukiongezeka .

Aidha amesema wametekeleza agizo la mkuu wa mkoa la kulima zao la pamba katika shule za msingi na sekondari za serikali  ambapo jumla ya hekari  1,500  na hekari 230 za mahindi  ili kuwawezesha wanafunzi kupata chakula cha mchana .
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka akizungumza na Maafisa Elimu wa Halmashauri  za Mkoa huo (hawapo pichani) katika  tathimini ya elimu iliyofanyika katika Shule ya Msingi Lukungu Wilayani Busega.

Afisa Elimu Mkoa wa Simiyu,Mwl. Julius Nestory Maafisa Elimu wa Halmashauri  za Mkoa huo (hawapo pichani) katika  tathimini ya elimu iliyofanyika katika Shule ya Msingi Lukungu Wilayani Busega. 
Baadhi ya Maafisa Elimu wa Halmashauri za Mkoa wa Simiyu wakimsikilizaMkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka(hayupo pichani) katika tathmini ya Elimu iliyofanyika Wilayani Busega.
Baadhi ya Maafisa Elimu wa Halmashauri za Mkoa wa Simiyu wakimsikilizaMkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka(hayupo pichani) katika  tathmini ya Elimu iliyofanyika Wilayani Busega.


WANUNUZI WA PAMBA WASIO WAAMINIFU WATAJWA KUWA CHANZO CHA WAKULIMA KUCHANGANYA PAMBA NA MAJI

Viongozi na wanachama wa Vyama vya Ushirika wa Mazao -AMCOS Mkoani SIMIYU wamesema chanzo cha wakulima wa Pamba kuchanganya mchanga na mafuta ya kenge kwa madai ya kuongeza uzito katika zao hilo kinatokana na baadhi ya wanunuzi wasio waaminifu  kuwaibia kupitia mizani.

Hayo wameyasema katika majadiliano ya namna ya uendeshaji vya Vyama vya Ushirika na uanzishwaji wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa SIMIYU mjadala ulioandaliwa ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini.

Kikao baina ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka na viongozi na wanachama wa Vyama vya Ushirika wa Mazao -AMCOS chenye lengo la kujadili changamoto zinazowakabili wakulima na uanzishwaji wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa SIMIYU.

Katika mjadala huo wadau hao wamesema udangangifu katika mizani ya kupima uzito wa Pamba umechangia kwa kiasi kikubwa  wakulima kutumia mbinu mbadala za kuongeza uzito

Moses Masalu Mwenyekiti wa chama cha ushirika mhango halmashauri ya mji wa bariadi amesema kuwepo kwa wizi wa pamba katika mizani za kupimia uzito kumesababisha wakulima wengi kutumia mbinu mbadala za kuongeza uzito ili kufidia machungu ya kuibiwa pamba yao na makarani wanapoenda kuuza pamba.

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga amesema kuchelewa kuanza kwa msimu wa pamba kunachangia kushuka kwa bei soko la dunia kutokana na kugongana na mataifa mengine katika msimu na hivyo kupendekeza kuanza april badala ya mei na juni.

Kwa upande wake Kaimu Mrajisi Masoko na Uwekezaji Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini, EDMUND MASSAWE amesema nia ya serikali ya kuimarisha ushirika nchini ni kuviwezesha vyama vikuu kununua mazao ya wakulima.

Akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka amewasisitiza viongozi wa  vyama hivyo kuwa waadilifu .

Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa SIMIYU kinatarajiwa kuundwa April mwaka huu kabla ya kuanza msimu wa ununuzi.


Baadhi ya viongozi na wanachama wa Vyama vya Ushirika wa Mazao -AMCOS wakimsikilza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka(hayupo pichani) katika kikao cha kujadili changamoto zinazowakabili wakulima na uanzishwaji wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa SIMIYU
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na viongozi na wanachama wa Vyama vya Ushirika wa Mazao -AMCOS (hawapo pichani)katika kikao cha kujadili changamoto zinazowakabili wakulima na uanzishwaji wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa SIMIYU.




Monday, January 8, 2018

RC MTAKA AMTAKA MKANDARASI KUKAMILISHA MRADI WA MAJI WA LAMADI KABLA YA SEPTEMBA 2019

Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka amemwagiza Mkandarasi wa Kampuni ya China ya CCECC  inayotekeleza mradi wa maji LAMADI kuukamilisha kabla ya mwezi Septemba 2019.

MTAKA ametoa agizo hilo baada ya kuukagua mradi huo unaoanzia katika kijiji cha KARAGO hadi LAMADI wilayani BUSEGA na hadi kukamilika kwake unatarajiwa kunufaisha zaidi ya kaya elfu tano za kata ya Lamadi.

 “Matarajio ya Serikali utekelezaji wa Mradi  huu umalizike kabla ya Septemba 2019 ili uweze kukidhi mahitaji ya watu wa Lamadi na utumike vizuri na viongozi wa CCM watakaoomba ridhaa ya kuwatumikia wananchi katika Serikali za Mitaa mwakani kundi utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa vitendo” alisema Mtaka.

Mbunge wa Jimbo la Busega Dkt Raphael Chegeni pamoja na wananchi wa Lamadi wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Magufuli kwa kutekeleza ahadi ya kuwapelekea  maji wa   mradi wa maji ambao utawasaidia kupata huduma ya maji safi na salama iliyo ya uhakika.

Mradi huo unaotekelezwa kwa miezi 24 unatarajiwa kugharimu jumla ya shilingi Bilioni TISA
.
Katika hatua nyingine akiwa katika Mkutano wa Hadhara katika kijiji cha LAMADI Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka ametangaza kuwa biashara zifanyike kwa saa 24 katika Eneo (centre) la Lamadi Wilayani Busega.

“Eneo la Barabara Kuu ya Musoma Mwanza kutoka Benki ya Azania Tawi la Lamadi mpaka eneo la mwisho pale kwenye  daraja letu, hili litakuwa eneo mahususi la kufanya biashara saa 24”  alisisitiza Mtaka.

Amewataka wakazi wa Lamadi kuitumia kwa faida barabara Kuu ya Musoma-Mwanza na kituo(centre) kikubwa kinachoyakutanisha magari yaendayo mikoani na nchi jirani kwa kufanya biashara saa kama ilivyo kwa maeneo kama hayo katika mikoa mingine,


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(wa pili kushoto) akitoa maelekezo kwa Mhandisi Mshauri wa Mradi  wa Maji wa Lamadi wakati alipotembelea mradi huo jana, wilayani Busega.
Mhandisi Mshauri wa Mradi wa Maji Lamadi, Baraka Alphayo(kulia) kutoka Kampuni ya EGIS EAU CONSULT akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (wa pili kushoto) na viongozi wengine wakati Mkuu huyo wa Mkoa alipotembelea mradi huo jana wilayani Busega.
Mhandisi Mshauri wa Mradi wa Maji Lamadi , Baraka Alphayo(kushoto) kutoka Kampuni ya EGIS EAU CONSULT akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(kulia) wakati alipotembelea mradi huo jana wilayani Busega(kattikati) Mbunge wa Busega, mhe.Dkt.Raphael Chegeni.
Mhandisi Mshauri wa Mradi wa Maji Lamadi , Baraka Alphayo kutoka Kampuni ya EGIS EAU CONSULT akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (kushoto)wakati alipotembelea Ofisi zitakazotumiwa na Mamlaka ya Maji Lamadi jana wilayani Busega,(kulia)Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe.Tano Mwera.



MWENYEKITI, WAJUMBE WA SERIKALI YA KIJIJI LAMADI WASIMAMISHWA KAZI KUPISHA UCHUNGUZI





Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amemsimamisha kazi kwa muda wa mwezi mmoja Mwenyekiti wa Kijiji cha Lamadi Wilayani Busega Mhe.Nzala Hezron pamoja na Wajumbe wa Serikali ya Kijiji hicho, ili kupisha uchunguzi kufuatia tuhuma mbalimbali zinazowakabili.

Uamuzi huo umekuja kufuatia malalamiko yaliyotolewa na wananchi wa Lamadi dhidi ya Mwenyeiti huyo kwa Mkuu Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka katika Mkutano wa hadhara uliofanyika jana Lamadi, kuhusu tuhuma mbalimbali ikiwemo matumizi mabaya ya fedha za michango ya wananchi katika Ujenzi wa Shule ya Sekondari Lukungu pamoja na kutosoma mapato na matumizi ya fedha za michango mbalimbali ya wananchi.

“Ili tuweze kutenda haki ya uchunguzi na ukaguzi tumeona ni busara Mwenyekiti asiwe Ofisini na wajumbe wanaounda Serikali ya Kijiji  wasiwe ofisini ili uchunguzi na ukaguzi wa akaunti uweze kufanyika kwa haki” alisema Mtaka.

Mtaka amesema Mkaguzi wa Ndani kutoka katika Ofisi yake atakayeshirikiana na Mkaguzi wa ndani wa Wilaya ya Busega kufanya ukaguzi katika Akaunti ya Shule kujua namna fedha zilizochangwa na wananchi na zilizotolewa na Halmashauri zilivyofanya kazi ya Ujenzi wa Vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo katika Shule ya Sekondari Lukungu.

Ameongeza kuwa kutokana na malalamilo ya baadhi ya wadau pamoja na wananchi uchunguzi na ukaguzi huo pia utahusisha pia Akaunti ya Kijiji cha Lamadi kwa kuwa Kijiji hicho kina hali nzuri kimapato na kimekuwa kikichangiwa na wadau mbalimbali wa maendeleo, hivyo ni vema ikabainishwa wadau wanaokichangia, wanachangia kitu gani na namna michango hiyo inavyotumika.

Aidha, Mtaka amesema ukaguzi huo pia utafanywa kwenye kamati iliyohusika katika upimaji viwanja katika Mji Mdogo wa Lamadi kwa sababu nayo imekuwa ikilalamikiwa na baadhi ya wananchi kuwa haikuwatendea haki.

Mkuu wa Mkoa huyo amesema uchunguzi na ukaguzi katika maeneo hayo matatu utaanza tarehe 10/01/2018 na taarifa rasmi ya zoezi hilo itatolewa tarehe 10/02/2018 kwa wananchi kupitia Mkutano wa hadhara, itakapobainika kuwa tuhuma zilizotolewa dhidi ya watu hao ni za kweli Serikali itachukua hatua.

Wakati huo huo Mtaka amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega kumuondoa Afisa Mtendaji wa Kata ya Lamadi Bw.Furaha Magese Ng’onela  na kuhakikisha kuwa ifikapo tarehe 10/01/2018 Kijiji cha Lamadi kinapata Mtendaji wa Kijiji kwa kuwa aliyepo sasa anakaimu na Kata ya Lamadi ipangiwe Afisa Mtendaji mwingine.

Vile vile Mtaka ameahidi kuchangia mifuko 100 ya saruji katika Ujenzi wa Shule ya Sekondari Lukungu ambayo sasa imepewe jina lake(Mtaka Sekondari) na wananchi hao, Mkuu wa Wilaya ya Busega,Mhe.Tano Mwera ameahidi kuchangia mifuko 40 na Mbunge wa Jimbo la Busega, Mhe.Dkt.Raphael Chegeni ameahidi kutoa vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya shilingi milioni 10 kufanikisha ujenzi huo.

Kwa upande wake Mwenyekiti  wa Kijiji cha Lamadi, Mhe.Nzala Hezron amesema kuhusu  suala la ujenzi wa Shule yeye pamoja na Serikali yake ya Kijiji haikushirikishwa kikamilifu na Kamati ya Maendeleo ya Kata(WADC).

Naye Mhe.Chegeni amemhakikishia Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka kuwa michango ya viongozi, wadau wa mendeleo na wananchi wa Lamadi inayotolewa sasa itatumika kama ilivyokusudiwa na ikiwa kuna atakayebainika kutumia tofauti na utararibu atachukuliwa hatua.

Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe.Tano mwera ametoa wito kwa wananchi wa Lamadi kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuchangia shilingi 10,000 kwa kaya ili kufikia Februari 15, 2018 vyumba vinne vya madarasa viwe vimekamilika katika Shule ya Sekondari Lukungu(imebadilishiwa jina na wananchi na kuitwa Mtaka Sekondari), ambayo hadi sasa ina madarasa manne na matundu ya vyoo 16 yanayoendelea kukamilishwa ili wanafunzi waanze masomo.

Nao wananchi wa Vijiji vinavyounda Kata ya Lamadi wamesema wamejipanga kuhakikisha vyumba vya madarasa vinajengwa na kukamilika  katika shule hiyo kabla ya Februari 15, 2018 ambapo kila Kitongoji kimejipanga kuanza na ujenzi wa chumba kimoja cha darasa na vitongoji vyenye watu wachache vitaungana viwili kujenga chumba kimoja cha darasa, ambapo  kamati za ujenzi zitachaguliwa na wananchi wenyewe.


Mwenyekiti wa Kijiji cha Lamadi Wilayani Busega, Mhe. Nzala Hezron akizungumza na wananchi katika Mkutano wa Hadhara ulioitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka kwa lengo la kusikiliza kero mbalimbali za wananchi na kuzitolea  ufumbuzi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu akizungumza na wananchi wa Kata ya Lamadi katika mkutano wa Hadhara uliofanyika Lamadi wiayani Busega.
Diwani wa Kata ya Lamadi Mhe.Bija Laurent Bija akizungumza na wananchi wa kata hiyo  katika Mkutano wa Hadhara ulioitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka kwa lengo la kusikiliza kero mbalimbali za wananchi na kuzitolea  ufumbuzi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (kushoto) na Mbunge wa Jimbo la Busega Mhe.Dkt. Raphael Chegeni wakifurahia jambo wakiwa kwenye Mkutano wa Hadhara uliofanyika katika Kata ya Lamadi wilayani Busega.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Maka(kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe.Tano Mwera wakiwa kwenye Mkutano wa Hadhara uliofanyika katika Kata ya Lamadi wilayani Busega.  
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Simiyu, Boniventure Mushongi akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Lamadi wilayani Busega.

Ngolo Masunga mkazi wa Kijiji cha Lamadi akiwasilisha malalamiko yake kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(hayupo pichani) katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Lamadi wilayani Busega.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Lamadi Bw.Furaha Magese Ng’onela akifafanua jambo katika Mkutano wa Hadhara uliofanyika katika Kata hiyo wilayani Busega.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Ndg.Anderson Njiginya akifafanua jambo katika Mkutano wa Hadhara uliofanyika katika Kata ya Lamadi wilayani humo.

RC MTAKA AKUTANA NA BALOZI WA CHINA HAPA NCHINI, AAHIDI MENGI KWA MKOA WA SIMIYU






Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amekutana na Balozi wa China Nchini Tanzania Mhe.Wang Ke.

Balozi Wang amefurahishwa na utekelezaji wa Mpango wa Simiyu  wa One Product One Distict-(Wilaya Moja Bidhaa Moja) Maana China kwa sasa wanatekeleza One Belt One Road.

Aidha, ametoa vyerehani 50 kwa Mabinti wa Simiyu ikiwa ni kuunga Mkono juhudi za viwanda vidogovidogo mkoani Simiyu.

Balozi huyo pia amekubali kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kujenga bweni moja la watoto wa kike na  amesema yupo tayari kusaidia ujenzi wa Maktaba ndani ya mkoa

Wakati huo huo amesema atasaidia kompyuta kuunga mkono juhudi za Mkoa kwenye Maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(ICT) na kusaidia mkoa kupata jimbo rafiki nchini china pamoja na baadhi ya maafisa wa Simiyu kwenda China kupata uzoefu.


Vilevile ameuchagua Mkoa wa Simiyu kuwa mkoa wake wa Kipaumbele katika maeneo mengi ya miradi ya Kilimo,mifugo na uvuvi.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(kushoto) akiwa na Balozi wa China hapa Nchini, Mhe.Wang Ke ofisini kwake jijini Dar es Salaam ambapo walizungumza mambo mengi kuhusu maendeleo ya Mkoa wa Simiyu














Thursday, January 4, 2018

ANGELINA MABULA: HALMASHAURI ZITUMIE WATAALAM WAKE KUPIMA MAENEO ILI KUWAPUNGUZIA ADHA WANANCHI

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe.Angelina Mabula amezitaka Halmashauri mkoani Simiyu kutumia Wataalam wake kupima maeneo ili wananchi waweze kupata hati miliki ya maeneo yao na kupunguza adha mbalimbali hususani migogoro.

Mhe.Mabula ameyasema hayo wakati wa ziara yake Mkoani Simiyu iliyokuwa na lengo la kukagua jengo litakalotumika kama Ofisi ya Kanda ya Ardhi ya Simiyu na kufuatilia utekelezaji wa maelekezo aliyotoa wakati wa ziara yake mwezi Agosti mwaka jana Mjini Bariadi.

Amesema ikiwa kuna Halmashauri inahitaji kupima viwanja na mashamba na ina watumishi wachache katika Idara ya Ardhi ufanyike utaratibu wa kuomba watumishi kutoka katika halmashauri nyingine ili waweze kuungana na kuweka kambi katika Halmashauri husika wafanye kazi ya kuwahudumia wananchi wengi kwa wakati mmoja.

“ Hatuna wataalam wa kutosha kuweza kupima viwanja vingi kwa wakati mmoja katika Halmashauri, lakini tunao wataalam katika Mkoa husika ambao tulishasema kama kuna uhitaji wa kupima maeneo katika Halmashauri moja wataalam wote ndani ya mkoa wakusanywe waweke kambi hapo mpaka hiyo kazi iishe , wakimaliza wanahamia wilaya nyingine” alisisitiza Mabula.

Ameongeza kuwa Halmashauri yoyote itakapoona ina uhitaji wa watalaam kutoka Ofisi ya Kanda kwa ajili ya kuongeza nguvu katika zoezi la upimaji, Ofisi hiyo ipo tayari kufanya kazi na Halmashauri yoyote itakayoomba.

Aidha, amezitaka Halmashauri mkoani Simiyu kupima maeneo yote ya Mjini pamoja na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda na uwekezaji.

Kwa upande wake Kaimu Kamishna wa Kanda ya Ardhi ya Simiyu, Ndg. Makwasa Biswalo ametoa wito kwa Watalaam mkoani humo kuona namna ya kutenga eneo la mipango miji katika eneo lililopitiwa na barabara ya lami ya  kilomita 70 kutoka Bariadi mpaka Lamadi(kilomita kadhaa kwenye kila upande wa barabara) ambalo ni eneo zuri kwa ajili ya uwekezaji.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amesema ameshazungumza na Watendaji wa Halmashauri zinazopitiwa na barabara hiyo ya Bariadi-Lamadi(KM 70) kuwa,  waone  namna Halmashauri hizo zinavyoweza kumiliki maeneo hayo walau kilomita moja kushoto na kulia kwa barabara hiyo.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo na Makazi, Mhe. Angelina Mabula(wa tatu kushoto) akiangalia baadhi ya hati za kimila zilizoandaliwa kwa ajili wananchi wa Wilaya ya Bariadi katika Ofisi ya Idara ya Ardhi ya Halmashauri hiyo, wakati wa ziara yake Mkoani Simiyu.


Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo na Makazi, Mhe. Angelina Mabula akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Simiyu wakati wa ziara yake Mkoani humo, (kushoto) Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka.
 Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (kushoto) akizungumza na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo na Makazi, Mhe. Angelina Mabula alipokuwa Mkoani humo kwa ziara ya siku moja.


 Kaimu Kamishna wa Ardhi Kanda ya Simiyu,Ndg.Makwasa Biswalo akifafanua jambo wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo na Makazi, Mhe. Angelina Mabula Mkoani Simiyu,(kulia) Afisa Ardhi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Bi.Grace Mgombera.
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu,Ndg.Jumanne Sagini akifafanua jambo wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo na Makazi, Mhe. Angelina Mabula Mkoani Simiyu.
Mkuu wa Idara ya Ardhi  na Maliasili katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Ndg.Mazengo Sabaya akifafanua jambo wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo na Makazi, Mhe. Angelina Mabula Mkoani Simiyu.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Ndg.Abdallah Malela akifafanua jambo wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya  Makazi, Mhe. Angelina Mabula Mkoani Simiyu.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe.Angelina Mabula(kulia) akitoa maelekezo kwa baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Simiyu baada ya kukagua Jengo la Ofisi linalotarajiwa kutumika kama Ofisi ya muda ya Kanda ya Ardhi Simiyu, wakati wa ziara yake Mkoani humo.
Baadhi ya viongozi na wataalam wa Mkoa wa Simiyu wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe.Angelina Mabula (hayupo pichani) wakati wa ziara yake Mkoani humo.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe.Angelina Mabula(kulia) pamoja na baadhi ya viongozi na Watalaam wa Mkoa wa Simiyu akitoka katika  Jengo  linalotarajiwa kutumika kama Ofisi ya muda ya Kanda ya Ardhi Simiyu, wakati wa ziara yake Mkoani humo, (kushoto) Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga.

Wednesday, January 3, 2018

WAZIRI MWIJAGE: NJIA NZURI YA KUFIKIA UCHUMI WA KATI NI UCHUMI WA VIWANDA

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage amesema njia nzuri ya kufikia Uchumi wa Kati ifikapo mwaka 2025 ni kupitia Uchumi wa Viwanda jumuishi.

Waziri Mwijage ameyasema hayo alipozungumza na wadau wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Mkoa wa Simiyu wakati wa ziara yake Mkoani humo, ambapo alisisitiza juu ya Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda ulio imara, shindani na endelevu, utakaozingatia mambo muhimu matatu ambayo ni soko, malighafi na teknolojia.

Amesema lengo la  Serikali ni kuhamasisha ujenzi wa Uchumi wa Viwanda Jumuishi ambao unawahusisha watu wengi kupitia viwanda vidogo na vya kati,vitakavyotumia malighafi zitakozozalishwa hapa nchini vilivyopo katika maeneo mbalimbali nchini,  ukiwepo mkoa wa Simiyu ambao umeonekana kufanya vizuri katika eneo hilo.

“Safari ya Simiyu imeanza vizuri na lengo la safari ni kuhamasisha Watanzania kujenga uchumi wa viwanda jumuishi, viwanda ambayo malighafi yake inazalishwa  na wananchi wenyewe, vitatoa ajira kwa wananchi walio wengi, vitatumia malighafi asilia na kutoa mazao yenye matumizi makubwa” alisema Mwijage.

Waziri Mwijage amepongeza juhudi zinazofanywa na Mkoa wa Simiyu katika Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda kupitia Falsafa ya “Wilaya Moja Bidhaa Moja Kiwanda Kimoja” ambapo sasa umejipanga kuelekea kwenye “Kijiji Kimoja Bidhaa Moja”.

Ameongeza kuwa mwaka 2018/2019 Serikali kupitia Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo(SIDO) litawasaidia wananchi kupata mafunzo ya ujasiriamali, uzalishaji na uchakataji, ambapo ameuhakikishia Viongozi wa Mkoa wa Simiyu kuwa Ujenzi wa Ofisi ya SIDO ya Mkoa huo eneo la Isanga Mjini Bariadi utakamilika kabla ya kuanza kwa vikao vya Bunge la Bajeti mwaka  2018, kwa kuwa fedha za ujenzi zipo.

Sanjali na hilo Waziri Mwijage amewataka Maafisa Ushirika kuwahamasisha wananchi kujiunga katika vikundi ili waweze kukopeshwa mitaji ya kuanzisha viwanda vidogo na Serikali pamoja na Taasisi nyingine za Kifedha kwa kuwa ni rahisi zaidi vikudi kufikiwa kuliko mtu mmoja mmoja.

Wakati huo huo Mwijage amewataka watendaji wote wa Serikali kuondoa vikwazo na kuacha urasimu unaoweza kuwakwamisha wawekezaji katika maeneo mbalimbali hapa nchini ili kuweza kuufikia Uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Akiwasilisha tarifa ya Mkoa, Katibu Tawala Mkoa Simiyu, Ndg. Jumanne Sagini amesema ili kuandaa mazingira mazuri yatakayowawezesha wawekezaji kuvutiwa na kuwekeza mkoani humo, wametenga maeneo ya uwekezaji na madawati ya uwekezaji kwa kila Halmashauri na timu mahsusi ya Mkoa ya kuanzisha na kuendeleza dhana ya Simiyu ya Viwanda inayoongozwa na Katibu Tawala Mkoa.

Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Mkoa wa Simiyu, Njalu Silanga amesema wako tayari kuunga mkono juhudi za Serikali kwa vitendo katika Ujenzi wa Viwanda vidogo na vya kati na akaomba Meneja wa SIDO Mkoa atembelee viwanda vilivyopo ili aweze kutoa ushauri juu kuboresha uendeshaji wa viwanda hivyo katika tija.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amesema kupitia SIDO mkoa huo unaweza kufikia Uchumi wa Kati. “Tungehitaji kuwa ni Mkoa ambao value addition(kuongeza thamani) itafanyika kupitia SIDO, mahali ambapo mtu mwenye milioni tatu wakiungana kikundi cha walima alizeti wanaprocess(wanachaka) wenyewe mafuta” alisema Mtaka.

Pamoja na kuzungumza na wadau wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Mkoa wa Simiyu, Waziri Mwijage alifungua Jengo la muda la Ofisi ya SIDO Mkoa wa Simiyu lililopo Mtaa wa Malambo Mjini Bariadi na kukagua eneo la ujenzi wa Ofisi mpya ya SIDO itakayojengwa na SUMA JKT, ambayo inatarajiwa kukamilika kabla ya kuanza kwa vikao vya Bunge la Bajeti mwaka  2018.



Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe.Charles Mwijage akifungua ofisi za Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) iliyoko Mtaa wa Malambo mjini Bariadi wakati wa ziara yake jana Mkoani Simiyu.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe.Charles Mwijage akitoa maelekezo kwa Meneja wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo(SIDO) Mkoa wa Simiyu, Ndg.Athanas Moshi  mara baada ya kufungua Ofisi ya muda ya Shirika hilo Mkoani humo, iliyoko Mtaa wa Malambo mjini Bariadi wakati wa ziara yake jana Mkoani Simiyu.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe.Charles Mwijage(mwenye skafu) akitoa maelekezo kwa Meneja wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo(SIDO) Mkoa wa Simiyu, Ndg.Athanas Moshi (kushoto) mara baada ya kufungua Ofisi ya muda ya Shirika hilo Mkoani humo, iliyoko Mtaa wa Malambo mjini Bariadi wakati wa ziara yake jana Mkoani Simiyu.
Katibu Tawala Mkoa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini akiwasilisha taarifa ya Mkoa kwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe.Charles Mwijage(hayupo pichani) wakati wa ziara yake Mkoani humo jana(kulia) Mkurugenzi Mkuu wa SIDO Tanzania, Profesa. Sylvester Mpanduji.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe.Charles Mwijage akizungumza na wadau mara baada ya kutembelea eneo itakapojengwa Ofisi Mpya ya SIDO Isanga Mjini Bariadi, wakati wa ziara yake mkoani Simiyu.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe.Charles Mwijage akivishwa skafu na vijana wa Skauti wa Mjini Bariadi mara baada ya kuwasili mahali ilipo Ofisi ya Muda ya SIDO Mtaa wa Malambo Mjini Bariadi.
Waziri wa  Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe.Charles Mwijage(kulia) akisaini Kitabu cha wageni katika Ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Simiyu mara baada ya kufika hapo wakati wa ziara yake Mkoani humo (kushoto) ni Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka.
Paroko wa Parokia ya Mtakatifu John Mjini Bariadi, Padre.Kizito Nyanga akichangia hoja katika kikao cha Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe.Charles Mwijage na wadau mkoani Simiyu.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Mkoani Simiyu na Mbunge wa Jimbo la Itilima,Mhe.Njalu Silanga akichangia hoja katika kikao cha Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe..Charles Mwijage na wadau mkoani Simiyu.
Baadhi ya wadau wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mkoa wa Simiyu wakimsikiliza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe.Charles Mwijage (hayupo picha) katika kikao maalum kati yake na wadau hao wakati wa Ziara yake Mkoani humo.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga akichangia hoja katika kikao cha Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe.Charles Mwijage na wadau mkoani Simiyu.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe.Charles Mwijage (wa sita kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi na wadau wa viwanda Mkoa wa Simiyu wakati wa ziara yake mkoani humo.

WIZARA YA ELIMU YATOA VITABU 16985 KWA SHULE ZA SEKONDARI SIMIYU

Wizara ya Elimu pamoja na wadau wengine wa Elimu wametoa vitabu 16,985 kwa shule za Sekondari za Mkoa wa Simiyu kwa ajili ya  matayarisho ya awali ya kuwaandaa wanafunzi wa kidato cha kwanza na elimu ya sekondari (baseline course).

Akikabidhi vitabu hivyo kwa Maafisa Elimu wa Halmashauri zote sita za Mkoa wa Simiyu, Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka amesema vitabu hivyo ni msaada mkubwa kwa Mkoa huo,  vikitumiwa vizuri  na walimu wenye nia ya kufanya mapinduzi ya elimu na kuwasaidia wanafunzi kujua maana halisi ya vitabu hivyo vitasaidia  Mkoa wa Simiyu kufikia malengo ya kiushindani katika Elimu.

Ameongeza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata vitabu pamoja na mahitaji mengine ikiwa ni pamoja na madawati, walimu, vyumba vya madarasa vinavyotolesheleza hivyo akasisitiza vitabu hivyo vikatumike kwa kusoma ili viwasaidie.

“Vitabu hivi mtakapogawiwa mkavitumie kwa ajili ya kusoma visiwe mapambo na kama mwanafunzi hujui uliza, jibidiishe kujua kitabu hicho kinahusu nini na kama hujaelewa muulize mwalimu ili kesho kwenye mtihani ufaulu kama wenzako wananvyofaulu” alisema Mtaka.

Aidha, Mtaka amewataka Maafisa Elimu mkoani humo kuzungumza na walimu kabla ya kugawa vitabu hivyo ili vitakapogawiwa katika shule vigawiwe katika utaratibu mzuri utakowawezesha walimu kuwasadia wanafunzi kuvitumia kwa manufaa.

Akitoa taarifa juu mapokezi ya vikao hivyo Katibu Tawala Mkoa amesema Mkoa huo umepokea jumla ya vitabu 16,000 kwa ajili ya wanafunzi na vitabu 985 kwa ajili walimu(kiongozi cha mwalimu).

Akizungumza kwa niaba ya Maafisa Elimu Sekondari mkoani humo,  Afisa Elimu Sekondari wa Halmahauri ya Mji Bariadi Mwl. Esthom Makyara amesema vitabu hivyo ni msingi mzuri kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza na Maafisa Elimu hao wanapaswa  kuwaelekezaWakuu wa shule kutofungia vitabu hivyo  stoo badala yake wanafunzi wapewe ili wavisome.

Naye Kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Simiyu, Ndg.Charles Maganga amesema Maafisa Elimu Sekondari wahakikishe vitabu hivyo vinagawiwa kwa wakuu wa shule kabla ya shule kufunguliwa Januari 08, 2018, ili wanafunzi wa kidato cha kwanza wanapoanza masomo wavikute shuleni.

Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Bariadi walioshuhudia zoezi la ugawaji wa vitabu hivyo kimkoa wamesema, vitabu hivyo vitawasaidia wenzao wa kidato cha kwanza kujenga msingi  mzuri wa maarifa ya jumla na lugha ya Kiingereza.


Vitabu hivi vimetolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Msaada wa Watu wa Marekani(UKAID) kupitia Mpango wa Taifa waKuinua Ubora wa Elimu hapa nchini EQUIP-T.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(kushoto) akikabidhi vitabu vya matayarisho ya awali ya kuwaandaa wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa elimu ya sekondari (baseline course), kwa Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Mji Bariadi, Mwl. Esthom Makyara vilivyotolewa na wadau wa Elimu, wakati wa zoezi la ugawaji wa vitabu hivyo lililofanyika kimkoa Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na Maafisa Elimu Sekondari na baaadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari Bariadi(hawapo pichani), kabla ya kukabidhi vitabu vya matayarisho ya awali ya kuwaandaa wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa elimu ya sekondari (baseline course), kwa maafisa elimu wilaya vilivyotolewa na wadau mbaimbali wa Elimu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(kushoto) akikabidhi vitabu vya matayarisho ya awali ya kuwaandaa wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa elimu ya sekondari (baseline course), kwa Afisa Elimu (Sekondari) wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Mwl. Jumanne Yasini vilivyotolewa na wadau wa Elimu, wakati wa zoezi la ugawaji wa vitabu hivyo lililofanyika kimkoa Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(kushoto) akikabidhi vitabu vya matayarisho ya awali ya kuwaandaa wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa elimu ya sekondari (baseline course), kwa Afisa Elimu (Sekondari) wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Mwl. Joseph Mashauri vilivyotolewa na wadau wa Elimu, wakati wa zoezi la ugawaji wa vitabu hivyo lililofanyika kimkoa Mjini Bariadi.

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!