Tuesday, February 28, 2017

SIMIYU YAZINDUA RASMI MRADI WA KUPIMA NA KUTIBU WAATHIRIKA WA VVU

Na Stella Kalinga
Mkoa wa Simiyu leo umezindua mradi wa Kupima na Kutibu (Test and Treat) Wale watakaobainika kuwa na Virusi vya Ukimwi bila kujali wingi wa CD4.

Mradi huo ambao unaendeshwa na Shirika lisilo la Kiserikali la CUAMM umezinduliwa leo na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi ambaye amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka katika Ukumbi wa Kanisa Katoliki Mjini Bariadi na kushuhudiwa na viongozi wa serikali, viongozi wa dini, wataalam wa Afya ngazi ya Mkoa na wilaya na wadau wa Afya kutoka mashirika mbalimbali yasiyo ya Kiserikali.

Akisoma Hotuba ya Uzinduzi wa Mradi huo kwa Niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga ametoa wito kwa wananchi Mkoani humo  kujitokeza kwa wingi kupima na kujua hali zao, na kwa wale watakaobainika kuwa na maambukizi kuanza dawa mara moja kama wataalamu watakavyoelekeza.

Akitoa shukrani kwa Shirika la CUAMM amesema Serikali ya Mkoa iko tayari kuhamasisha na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika idara ya Afya kwa kutoa ushirikiano kwa wawekezaji watakaofuata sheria, uwekezaji wenye tija  na kusisitiza kuwa wadau watakaotaka kushirikiana na Mkoa huo katika maeneo tofauti ilikiwemo eneo la mapambano dhidi ya UKIMWI kujadiliana kwanza ili kuzingatia vipaumbele vya Mkoa.

 Aidha, ameuagiza  uongozi wa idara ya afya Mkoa kuhakikisha mipango ya wadau wote wanaofanya kazi na Mkoa wa Simiyu  inaingizwa katika mipango ya Idara hiyo (Comprehensive Regional Health plan/CCHP) ili kujua mchango wa wadau hao na kutokubali mipango isiyo na tija kwa wananchi.

“Mtakumbuka kuwa jukumu la kudhibiti UKIMWI si la Serikali peke yake bali ni la jamii kwa ujumla wakiwepo wadau mbalimbali, tukishirikiana kwa pamoja tunaweza kufikia malengo ya sifuri tatu, yaani maambukizi mapya sifuri, unyanyapaa kwa waathirika wa VVU sifuri na Vifo vitokanavyo na UKIMWI sifuri” amesema.

Akitoa taarifa ya mradi wa Pima na Kutibu(Test and Treat) ambao unatekelezwa katika Mikoa ya Simiyu na Shinyanga, Mwakilishi wa Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Shinyanga, Liberatus Sangu, Paroko wa Parokia ya Bariadi Padre Kizito Nyanga Victor, amesema Mradi huu unatarajiwa kutoa ushauri nasaha na kupima  ,jumla ya wakazi 300,000 Simiyu  sambamba na utoaji wa matibabu ya watoto wadogo  20,000  ikiwa ni moja ya  mkakati wa kupunguza kasi ya   maambukizi ya  asilimia 3.1 kimkoa.

Kizito amesema kuwa  makusudio ya mradi huo ni kuweka vituo vya upimaji ,kuimarisha  maabara na vitendanishi ,kupima usugu wa VVU ,wingi wa VVU  katika mwili ambapo wao kama Kanisa kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali wanaungana na Serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI.

Kwa upande wake Professa Samuel Kaluvya kutoka Chuo Kikuu cha Tiba  Bugando, ambaye ndiye Mshauri Mkuu wa Mradi  huu amesema kuwa Malengo ya   Shirika la Ukimwi Dunia katika nchi zote asilimia 90 ya watu  wanaoishi naVVU waweze kutambulika kwa kupimwa na kuweza kuunganishwa na mfumo wa kutoa dawa na asilimia 90 ya watu  wanaotumia dawa za kufubaza VVU wahakikishe wanatumia dawa hizo  ipasavyo kwa maisha yao yote .

Mradi wa Pima na Kutibu (Test and Treat) Mkoani Simiyu utaanza kutekelezwa katika vituo viwili vya kutolea huduma za Afya  Mwamapalala (wilayani Itilima) na Songambele (wilayani Bariadi) na baadaye vituo nane na hatimaye utatekelezwa katika wilaya zote.
Mwakilishi wa mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka, Mhe.Festo Kiswaga akizindua alama inayotambulisha Mradi wa Pima na Kutibu VVU (Test and Treat) uliozinduliwa leo Mjini Bariadi.
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka, Mhe.Festo Kiswaga akizungumza na viongozi, wataalam wa Afya na wadau mbalimbali wa afya kabla ya Uzinduzi wa Pima na Kutibu VVU (Test and Treat) Mjini Bariadi, ambao unatekelezwa na Shirika la CUAMM kwa kushirikiana na Serikali.

Mwakilishi wa Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Shinyanga, Liberatus Sangu, Paroko wa Parokia ya Bariadi Padre Kizito Nyanga Victor akizungumza na viongozi, wataalam wa Afya na wadau mbalimbali wa afya kabla ya Uzinduzi wa Mradi wa Pima na Kutibu VVU (Test and Treat) Mjini Bariadi, ambao unatekelezwa na Shirika la CUAMM kwa kushirikiana na Serikali.
Mwakilishi wa Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Shinyanga, Liberatus Sangu, Paroko wa Parokia ya Bariadi Padre Kizito Nyanga Victor akizungumza na viongozi, wataalam wa Afya na wadau mbalimbali wa afya kabla ya Uzinduzi wa Mradi wa Pima na Kutibu VVU (Test and Treat) Mjini Bariadi, ambao unatekelezwa na Shirika la CUAMM kwa kushirikiana na Serikali.
Meneja wa Mradi wa Pima na Kutibu VVU(Test and Treat)   Dkt.Arianna Bortolani kutoka Shirika la CUAMM  akitoa maelezo kwa Mkuu wa Wilaya ya Bariadi juu ya alama inayotumika kutambulisha mradi huo mara baada ya kufanya uzinduzi.
Baadhi ya Wajumbe wa Timu ya Usimamizi wa Idara ya Afya Mkoa (Regional Health Management Team RHMT) wakimsikiliza Mwakilishi wa mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka, Mhe.Festo Kiswaga kabla ya Uzinduzi wa Pima na Kutibu VVU (Test and Treat) Mjini Bariadi
Baadhi ya Wajumbe wa Timu ya Usimamizi wa Idara ya Afya Mkoa (Regional Health Management Team RHMT) wakimsikiliza Mwakilishi wa mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka, Mhe.Festo Kiswaga kabla ya Uzinduzi wa Pima na Kutibu VVU (Test and Treat) Mjini Bariadi.
Mratibu wa Mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI Mkoa wa Simiyu Dkt.Khamis Kulemba akiwasilisha mada ya hali ya maambukizi ya VVU kimkoa  kwa wadau malimbali wa afya katika kikao cha Pima na Kutibu VVU(Test and Treat).
Mganga Mkuu wa Mkoa, Dkt.Mageda Kihulya (wa pili kushoto) akizungumza katika kikao cha uzinduzi wa Mradi wa Pima na Kutibu VVU (Test and Treat) Mjini Bariadi,  (kushoto) Professa Samuel Kaluvya kutoka Chuo Kikuu cha Tiba  Bugando, ambaye ndiye Mshauri Mkuu wa Mradi  huo

Thursday, February 23, 2017

RAIS SHEIN ATIMIZA AHADI YA KUTOA VIFAA KUKAMILISHA UJENZI WA MSIKITI MKUU BARIADI

Na Stella Kalinga

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Ali Mohamed Shein ametimiza ahadi ya kutoa sadaka ya vifaa vya ujenzi wa Msikiti wa MASJID RAUDHAL  mjini Bariadi, ambao ni Msikiti mkuu Simiyu.

Rais Shein alitoa ahadi hiyo mwezi Oktoba 2016 wakati alipokuwa Mkoani Simiyu kuwaongoza Watanzania katika Maadhimisho ya Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru, Wiki ya Vijana na Kumbukumbu ya Kifo cha Baba wa Taifa Mwl.Nyerere.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo,Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka amemshukuru Mhe.Rais Shein na kubainisha kuwa ujio wake mwaka jana umeleta mafanikio makubwa kwa mkoa na kujenga uhusiano mazuri kati ya Mkoa wa Simiyu na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mtaka amesema ujio wa Dkt Shein mkoani Simiyu umefungua milango ya ushirikiano wa kibiashara kati na Zanzibar, ambapo alimtuma Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mhe.Riziki Pembe Juma mwezi Desemba mwaka jana kuja kuona Chaki za Maswa na sasa Mkoa huo unauza chaki Zanzibar.

 Aidha, ameongeza kwa kupitia ujio wake alimtuma Waziri wa Biashara,Viwanda na Masoko, Balozi Amina Salum Ali kuona fursa za biashara na sasa wananchi wa Simiyu wamehakikishiwa soko la Mchele na mazao ya mikunde Zanzibar kupitia makubaliano yatakayowekwa kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mkoa wa Simiyu.

"Dkt.Shein Akiwa Simiyu amefanya ya kimwili na ya kiroho sisi kama Mkoa tutakuwa mashahidi wa kazi na utumishi wake;kupitia yeye tumefanya biashara Zanzibar, kupitia yeye Msikiti wetu unajengwa kwa sadaka yake na kupitia yeye tumefungua milango mipana ya ushirikiano" alisema.

 Amesema Serikali ya Mkoa iko tayari kushirikiana na BAKWATA katika kuhakikisha mapungufu yatakayojitokeza yanatatuliwa ili Msikiti wa Kisasa na Ofisi za kisasa za BAKWATA zinajengwa ambazo zitaendana na hadhi ya makao makuu ya Mkoa.

Akitoa shukrani kwa niaba ya viongozi na waumin wa Kiislamu Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mahamoud Kalokola amesema anamshukuru Rais Shein kwa sadaka yake hiyo ambayo ina thawabu kubwa kwa Mwenyezi Mungu.

"Tunamshukuru sana Mhe.Rais Shein kwa sadaka yake na tunamwomba Mwenyezi Mungu amuongezee pale alipotoa, maana Quran inasema ajengaye msikiti anajijengea nyumba peponi" alisema.

Vile vile Sheikh Kalokola ametoa wito kwa watu wote wenye mapenzi mema kusaidia mahali popote misikiti inapojengwa ili kuwawezesha waumin kupata mahali pa kuswali jambo ambalo litawapa thawabu kwa Mwenyezi Mungu.

Vifaa vilivyotolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Ali Mohammed Shein kama sadaka yake ni saruji,nondo, rangi,mbao n.k ikiwa ni pamoja na fedha taslimu kwa ajili ya malipo ya mafundi na vimewasilishwa kwa niaba yake na Ally Habshy Abdallah, ili kukamilisha msikiti wa MASJID RAUDHAL.

 
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(wa tatu kushoto) na Sheikh Mkuu wa Mkoa huo,Mahamoud Kalokola (wa nne kushoto) na viongozi wengine wa BAKWATA mkoa wakipokea baadhi ya vifaa vya ujenzi vilivyotolewa na Rais wa Zanzibar,Mhe.Dkt.Ali Mohamed Shein kukamilisha ujenzi wa msikiti wa MASJID RAUDHAL mjini Bariadi kutoka kwa mwakilishi wake Ally Habshy Abdallah
Sheikh wa Mkoa wa Simiyu, Mahamoud Kalokola akizungumza na baadhi ya viongozi wa BAKWATA kabla ya kupokea vifaa vya ujenzi vilivyotolewa na Rais wa Zanzibar,Mhe.Dkt.Ali Mohamed Shein ili kukamilisha ujenzi wa msikiti wa MASJID RAUDHAL mjini Bariadi kutoka kwa mwakilishi wake Ally Habshy Abdallah

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na baadhi ya viongozi wa BAKWATA kabla ya kupokea vifaa vya ujenzi vilivyotolewa na Rais wa Zanzibar,Mhe.Dkt.Ali Mohamed Shein ili kukamilisha ujenzi wa msikiti wa MASJID RAUDHAL mjini Bariadi kutoka kwa mwakilishi wake Ally Habshy Abdallah.
Mwalikishi wa Rais wa Zanzibar,Mhe.Dkt.Ali Mohamed Shein Ndg. Ally Habshy Abdallah akizungumza viongozi wa BAKWATA kabla ya kuwasilisha vifaa vya ujenzi alivyovitoa kama sadaka yake ili kukamilisha ujenzi wa msikiti wa MASJID RAUDHAL mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(mwenye koti) akiangalia baadhi ya sehemu za Msikiti wa MASJID RAUDHAL mjini Bariadi unaotarajiwa kukamilika kujengwa baada ya kupokea vifaa kutoka kwa Rais wa Zanzibar,Mhe.Dkt.Ali Mohamed Shein.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na baadhi ya viongozi wa BAKWATA mara baada ya makabidhiano ya vifaa vya ujenzi wa  Msikiti wa MASJID RAUDHAL mjini Bariadi kutoka kwa Rais wa Zanzibar,Mhe.Dkt.Ali Mohamed Shein.

RC MTAKA ASEMA WAKUU WA SHULE HAWATASIMAMISHWA KUTOKANA NA MATOKEO MABAYA PEKEE.

Na Stella Kalinga
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka amesema Serikali mkoani humo haitawasimamisha kazi walimu wakuu na wakuu wa shule kutokana na matokeo mabaya ya shule zao, isipokuwa kwa uthibitisho wa taarifa za wadhibiti ubora wa elimu kuwa hawafai kushika nyadhifa hizo.

Mtaka ameyasema hayo leo ktk ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili ya kuboresha utendaji kwa wajumbe wa kamati za Shule za Msingi mkoani humo ktk ukumbi wa Kanisa Katoliki mjini Bariadi

Amesema suala la matokeo ya mitihani ya kitaifa kuwa mabaya lawama hazipaswi kwenda kwa walimu pekee kwa kuwa wazazi, kamati za shule, walimu na wanafunzi kila mmoja ana wajibu wake.

"Kuna wanafunzi wameshindikana hawawatii walimu, wazazi nao wanatetea ubovu wa watoto wao, halafu wakifeli mwalimu asimamishwe, hii haitawezekana kabisa; kwa nini  kamati za shule zisiwajibishwe" alihoji Mtaka.

Amesema ikiwa taarifa za wadhibiti ubora wa elimu zitaonesha kuwa mwalimu Mkuu au Mkuu wa shule amefanya kazi ktk kiwango kinachomfanya  apoteze sifa za kuwa katika nafasi yake, Wakurugenzi wa Halmashauri ambao ndio mamlaka yao ya nidhamu watawachukulia hatua kwa mujibu wa sheria za utumishi wa Umma.

Ameongeza kuwa Wakurugenzi wa Halmashauri wanapaswa kuwawezesha wadhibiti ubora kupita na kukagua shule zote, ili taarifa zao ziwe kichocheo cha kuchukua hatua kwa walimu wakuu,wakuu wa shule na kamati za shule.

Wakati huo huo Mtaka ameishauri Wizara yenye dhamana na Elimu kuacha utaratibu wa kufanya mabadiliko ya mara kwa mara ya mitaala ya Elimu ili kudhibiti ubora wa elimu hapa nchini.

Kwa upande wake Mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu(ADEM) Ndg.Adam Mnyavanu amesema  mafunzo hayo yatasaidia kutatua changamoto ya wazazi kutotambua nafasi yao katika elimu na kupitia kamati za shule wazazi watatambua wajibu wao katika maendeleo ya elimu.

Vile vile Mnyavanu ametoa wito kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kutenga fedha za kuwawezesha wadhibiti ubora kutekeleza majukumu yao ipasavyo katika bajeti za Halmashauri na kuhakikisha fedha hizo zinatumika kama ilivyokusudiwa kwa lengo la kuinua ubora wa elimu.

Mafunzo kwa wajumbe wa kamati za shule yaliyofadhiliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la EQUIP Tanzania, yamehusisha pia wataalam wa elimu ngazi ya Mkoa na wilaya na yamelenga kuwaelimisha wajumbe hao juu ya muundo wa kamati za shule, majukumu yake, namna wajumbe wanavyopatikana na umuhimu wa kamati hizo katika Maendeleo ya Elimu.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akifungua mafunzo ya kuboresha utendaji wa Wajumbe wa Kamati za Shule za Msingi Mkoani humo ambayo yamefanyika leo Mjini Bariadi .
Baadhi ya Washiriki wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akifungua mafunzo ya kuboresha utendaji wa Wajumbe wa Kamati za Shule za Msingi Mkoani humo ambayo yamefanyika leo Mjini Bariadi .
Mkufunzi kutoka Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu(ADEM) Ndg.Adam Mnyavanu akizungumza na wataalam wa Elimu na wajumbe wa Kamati ya Shule za Msingi katika mafunzo yaliyofanyika Mjini Bariadi.
Mkufunzi kutoka Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu(ADEM) Ndg.Adam Mnyavanu akizungumza na wataalam wa Elimu na wajumbe wa Kamati ya Shule za Msingi katika mafunzo yaliyofanyika Mjini Bariadi.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (wa kwanza kushoto kwa walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa  mafunzo ya kuboresha utendaji wa Wajumbe wa Kamati za Shule za Msingi Mkoani humo ambayo yamefanyika leo Mjini Bariadi



Wednesday, February 22, 2017

WANARIADHA WA KIMATAIFA  KUSHIRIKI MASHINDANO YA KILI -MARATHON
Na Stella Kalinga

Wanariadha wawili wa Kimataifa kutoka katika jimbo la Hanover  Nchini Ujerumani wanatarajia kushiriki  mashindano ya riadha ya Kilimanjaro Marathon yatakayofanyika  Februari 26 mwaka huu, Mkoani Kilimanjaro ikiwa ni moja kati ya ushirikiano baina ya Ujerumani na Tanzania.

Akifungua mafunzo ya siku moja ya makocha na walimu wa michezo  mbalimbali kutoka  mikoa minne ya kanda ya Ziwa ,Rais wa Shirikisho la Riadha Nchini ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka aliwataja wanariadha hao kuwa ni Christin Kulgemeyer na Stephan Immega ambao watakuwa chachu ya kuwatia moyo wanariadha wengine wa  Kitanzania 
.
Mtaka alibainisha kuwa licha ya kushiriki mashindano hayo,wanariadha hao watapata fursa ya kuona Mlima Kilimanjaro ikiwa ni moja kati ya kuitangaza Tanzania na vivutio vyake.

Aidha katika ufunguzi huo Mtaka  aliwataka makocha na viongozi wa michezo mbalimbali kutoka mikoa ya Simiyu,Mwanza,Mara na Shinyanga kuyatumia mafunzo hayo vizuri ili kujenga mtazamo chanya wa kimichezo katika mikoa ya kanda ya Ziwa.

Aliongeza kuwa viongozi hao wanapaswa kutambua kuwa riadha inakuwa ni moja kati ya njia ya kuitangaza nchi kwa Mataifa nyingine ikiwa ni pamoja na kujenga ushirikiano baina ya Mkoa wa Simiyu na jimbo la Hanover Nchini Ujerumani.

“Kupitia wanariadha hawa imekuwa faraja kuona  Tanzania riadha inakuwa ni sehemu ya kuitangaza nchi yetu, kwa sababu hawa wanariadha wametoka Ujerumani kuja kushiriki mashindano ya Kilimanjaro Marathoni mwaka huu 2017, ikiwa ni pamoja na kuwa sehemu ya ushirikiano kati ya Mkoa wa Simiyu na Jimbo la Hanover Ujerumani” alisema

Hata hivyo wanariadha hao wameonyesha kufurahishwa na kuanzishwa kwa ushirikiano wa kimichezo baina ya nchi yao na Mkoa wa Simiyu kwani wanaamini watajifunza mengi kutokana na kubadilishana uzoefu na kuifanya micheczo kuwa na nafasi kubwa Duniani.

Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka akifungua mafunzo ya Makocha na Walimu wa Michezo mbalimbali kutoka Mikoa ya Simiyu, Mwanza, Mara na Shinyanga.
Mwanariadha wa kike Christin Kulgemeyer lutoka Ujerumani anayetarajiwa kushiriki Kilimanjaro Marathon akizungumza na Makocha na Walimu wa Michezo mbalimbali kutoka Mikoa ya Simiyu, Mwanza, Mara na Shinyanga walio katika mafunzo mjini Bariadi.
Mwanariadha wa kiume kutoka Ujerumani Stephan Immega anayetarajiwa kushiriki Kilimanjaro Marathon akizungumza na Makocha na Walimu wa Michezo mbalimbali kutoka Mikoa ya Simiyu, Mwanza, Mara na Shinyanga walio katika mafunzo mjini Bariadi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi inayoshughulikia Michezo Nchini Ujerumani, Lowest Saxon Sports Association (LSB), Ndg .Reinhard Rawe akizungumza Makocha na Walimu wa Michezo mbalimbali kutoka Mikoa ya Simiyu, Mwanza, Mara na Shinyanga walio katika mafunzo mjini Bariadi.
Baadhi ya Makocha na Walimu wa Michezo mbalimbali kutoka Mikoa ya Simiyu, Mwanza, Mara na Shinyanga walio wakimsikiliza Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania, Mhe.Anthony Mtaka (hayupo pichani) wakati akifungua  mafunzo kwa washiriki hao mjini Bariadi.

Monday, February 13, 2017

#JUKWAA LA BIASHARA SIMIYU# RC MTAKA AWAKARIBISHA WAWEKEZAJI WAZAWA KUWEKEZA SIMIYU

Na Stella Kalinga
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka ametoa wito kwa Wafanyabiashara wazawa kuwekeza katika mkoa huo na kuwahakikishia kuwa Serikali iko tayari kuwaunga mkono.

Mtaka amesema hayo katika ufunguzi wa Jukwaa la biashara lililofanyika leo mjini Bariadi, ambalo limeandaliwa na Kampuni ya Magazeti ya Serikali(TSN) ikishirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.

Amesema fursa takribani 14 zimetangazwa katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo baada ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Kiuchumi na Kijamii(ESRF) uliopelekea kuandaliwa kwa Rasimu ya mwongozo wa uwekezaji wa mkoa.

"Tunataka kutransform mkoa wa Simiyu na kuufanya kuwa wa tofauti katika kuelekea  kwenye uchumi wa kati, Tungehitaji kujenga mkoa tofauti na watu wengine waje wajifunze; yapo tuliyoanza kutekeleza na yapo yaliyo kwenye pipeline" alisema.

Mtaka amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote mkoani humo, kutoweka urasimu usio wa lazima kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika maeneo yao.

Ameongeza kuwa mkoa wa Simiyu umeanzisha mfumo tofauti wa kushirikisha Sekta binafsi katika utekelezaji wa Sera ya Tanzania ya Viwanda ambapo wameanza kwa Halmashauri kuendesha viwanda vidogo kwa ubia na Vikundi vya Vijana; Wilaya ya Meatu(kiwanda cha kusindika maziwa) na Wilaya ya Maswa (Kiwanda cha kutengeneza Chaki).

Aidha, pamoja na kuwepo kwa viwanda vidogo  Mtaka amesema Serikali mkoani Simiyu imedhamiria kuwa na viwanda vya kati na vikubwa kwa lengo la kuyaongezea thamani mazao ya kilimo na mifugo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, ambaye pia ni Mtaalam wa masuala ya biashara, Profesa Elisante Ole Gabriel amewataka wafanyabiashara kuwa na utamaduni wa kulipa kodi kwa hiari ili biashara zao ziwe endelevu.

Pia Profesa Ole Gabriel ametoa rai kwa wafanyabiashara wa Mkoa wa Simiyu kuzijua vema biashara zao na kufanya biashara hizo kimkakati hususani katika kubuni biashara zinazojibu changamoto za jamii na suala la huduma bora kwa wateja.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA), Ndg.Richard Kayombo ametoa wito kwa wafanyabiashara kutunza kumbukumbu za biashara zao ili walipe kodi kulingana mapato yao ili kuiwezesha serikali kupata kodi/mapato stahiki.

Naye Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali(TSN) ambao ndiyo waandaaji wa Jukwaa la biashara, Dkt. Jim Yonazi amesema wao wanaamini maendeleo ni Habari, hivyo wako tayari kufanya kazi na mkoa wa Simiyu kwa kuwa viongozi wake wanachukia kasi ndogo katika maendeleo.

"Wakati wengine wanaona Simiyu kama mkoa mpya sisi tunaona fursa, tumeamua kupeleka habari za uwekezaji na maendeleo ya mkoa huu sehemu mbalimbali duniani kupitia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na sasa hivi watu zaidi ya 80,000 wanajua nini kinaendelea hapa" alisema.

Jukwaa la biashara mkoani Simiyu limeandaliwa na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) yaani Habari Leo, Daily News na Spoti Leo kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu. Wadau wengine ni Benki ya Maendeleo(TIB), Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA), Benki ya NMB na Baraza la Uwezeshaji wananchi Kiuchumi (NEEC)

Jukwaa hilo limewahusisha viongozi wa Mkoa huo ngazi ya Mkoa na Wilaya, wafanyabiashara na wadau mbalimbali wa Maendeleo wa Mkoa huo.

Pichani ni Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhariri Mhe.Anthony Mtaka, Mhariri Mtendaji wa TSN, Dkt.Jim Yonazi, Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Sanaa, Utamaduni na Michezo, Profesa Elisante Ole Gabriel,Mkurugenzi wa Elimu ya Mlipa Kodi wa TRA Ndg Richard Kayombo, Katibu Tawala Mkoa Simiyu,Ndg.Jumanne Sagini, viongozi wengine wa mkoa huo pamoja na wadau mbalimbali wakiwa katika jukwaa hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na wadau mbalimbali wa maendeleo wa Mkoa huo katika Jukwaa la biashara lililofanyika leo mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka  wa pili kulia na Profesa Elisante Ole Gabriel wa pili kushoto wakiteta jambo katika Jukwaa la Biashara lililofanyika leo Mjini Bariadi, (kushoto) Katibu Tawala mkoa , Ndg.Jumanne Sagini.
Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali(TSN) Dkt. Jim Yonazi  akizungumza na wadau wa maendeleo ya Mkoa wa Simiyu wakati wa jukwaa la Biashara lililofanyika leo Mjini Bariadi.
Mbunge wa Jimbo la Busega Mhe.Raphael Chegeni akichangia jambo katika Jukwaa la Biashara lililofanyika Mjini Bariadi.
Baadhi ya Makatibu Tawala Wasaidizi wakifuatilia uwasilishwaji wa mada mbalimbali katika Jukwaa la Biashara lililofanyika Mjini Bariadi.
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.Jumanne Abdalla Sagini akizungumza na wadau wa Maendeleo ya huo katika Jukwaa la Biashara Mjini Bariadi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa ,Utamaduni na Michezo, Profesa Elisante Ole Gabriel akiwasilisha mada katika Jukwaa la Biashara Mjini Bariadi . 
Baadhi ya Viongozi wakifuatilia uwasilishwaji wa mada mbalimbali katika Jukwaa la Biashara lililofanyika Mjini Bariadi katika Ukumbi wa Kanisa Katoliki.
Kwaya ya Kanisa la AICT Bariadi wakiimba wimbo maalum wakati wa Jukwaa la Biashara katika Ukumbi wa kanisa Katoliki Mjini Bariadi.
Kutoka kulia,(walioketi) Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga, Mkuu wa Wilaya ya Busega, Tano Mwera, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Prof.Elisante Ole Gabriel,  Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka , Mhariri Mtendaji wa TSN, Dkt. Jim Yonazi , Katibu Tawala Mkoa, Jumanne Sagini, Mwakilishi wa Benki ya Maendeleo (TIB) katika picha ya pamoja na washiriki wa  Jukwaa la Biashara  Mjini Bariadi.
Kutoka kulia,(walioketi)  Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga, Mkuu wa Wilaya ya Busega, Tano Mwera, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Prof.Elisante Ole Gabriel,  Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka , Mhariri Mtendaji wa TSN, Dkt. Jim Yonazi , Katibu Tawala Mkoa, Jumanne Sagini, Mwakilishi wa Benki ya Maendeleo (TIB)katika picha ya pamoja na viongozi wa Mkoa wa Simiyu wakati wa Jukwaa la Biashara .
Kutoka kulia,(walioketi)  Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga, Mkuu wa Wilaya ya Busega, Tano Mwera, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Prof.Elisante Ole Gabriel,  Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka , Mhariri Mtendaji wa TSN, Dkt. Jim Yonazi , Katibu Tawala Mkoa, Jumanne Sagini, Mwakilishi wa Benki ya Maendeleo (TIB)katika picha ya pamoja na Wabunge na Wakurugenzi wa Halmashauri wakati wa Jukwaa la Biashara Mjini Braiadi.
Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali(TSN) Dkt. Jim Yonazi akiwatambaulisha baadhi ya watumishi wa Kampuni ya Uchapishaji wa Magazi ya Serikali (TSN) kwa wadau wa Maendeleo y Mkoa wa Simiu wakati wa Jukwaa la Biashara Mkoani humo Mjini Bariadi.

Saturday, February 11, 2017

VIONGOZI WA TAASISI ZA UMMA SIMIYU WAHIMIZWA KUSIMAMIA UTEKELEZAJI WA AGIZO LA MAKAMU WA RAISPI

Na Stella Kalinga

Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu,Ndg.Jumanne Sagini ametoa wito kwa viongozi na Wakuu wa Taasisi za Umma mkoani humo,  kusimamia utekelezaji wa agizo la Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan la kufanya mazoezi ya viungo Jumamosi ya pili ya kila mwezi.

Sagini ametoa wito huo leo katika hotuba yake kwa watumishi wa umma,wanafunzi na wananchi walioshiriki mazoezi ya viungo na michezo mbalimbali katika uwanja wa Halmashauri ya Mji Bariadi ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mhe.Makamu wa Rais.

Amesema Simiyu wamejipanga kutekeleza na akawataka watumishi wa Umma kuheshimu agizo hilo na kutekeleza kama ilivyoelekezwa, badala ya kuamua kushiriki au kutoshiriki. 

"...Niombe wote wanaowasimamia Watumishi wa Umma kuhimiza utaratibu huu wa mazoezi ambao ni agizo la Makamu wa Rais ambalo limeongozana na nyaraka za Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara yenye dhamana na Elimu na Mafunzo ya Ufundi, lakini mara kadhaa hata Wizara ya Afya imekuwa ikisema,  Sisi kama Watumishi wa Umma hatuwezi kuchagua kutekeleza au tusitekeleze" alisema.

Amesema kila mkuu wa Taasisi,Idara,Sehemu anapaswa kuhakikisha watumishi walio chini yake wanashiriki mazoezi ya viungo mwezi ujao(Machi) kwa kuwa  kushindwa kutekeleza Maelekezo ya viongozi pasipo sababu za msingi ni utovu wa nidhamu, ambalo ni kosa kwa mujibu wa Sheria,kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma.

Sagini ameongeza kuwa watumishi ambao hawatashiriki mazoezi ya viungo pasipo sababu za msingi wahojiwe na ikibidi wachukuliwe hatua stahiki kutokana na utoro huo.

Aidha, ametoa rai kuwa watumishi wa umma kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara ili kupambana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza kama shinikizo la damu, kisukari na magonjwa ya moyo kwa kuwa muda mwingi wanakuwa maofisini.

Wakati huo huo Afisa Michezo wa Mkoa wa Simiyu,Ndg.Addo Komba amesema pamoja na kutekeleza agizo la Mhe.Makamu wa Rais, Mkoa una mpango wa kuwakutanisha watumishi wote wa Umma na Wanafunzi mara mbili kwa mwezi kufanya mazoezi ya viungo na michezo mbalimbali.

Sambamba na hilo Komba amesema katika kutambua na kuinua vipaji kwenye michezo, mkoa umepanga kuandaa ligi mwishoni mwa mwezi Februari, 2017 kwa ajili ya wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari kwa michezo mitatu ambayo ni mpira wa miguu, mpira wa pete na Riadha.


Utekelezaji wa Agizo la Makamu wa Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan mkoani Simiyu, unafanyika chini ya kauli mbiu"SIMIYU MPYA, MICHEZO KWA AFYA, AMANI NA MAENDELEO."
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini (mwenye kofia nyeupe) akiwa na baadhi ya watumishi  katika mazoezi ya kutembea kwenye Uwanja wa Halamshauri ya Mji Bariadi, wakati wa utekelezaji wa agizo la Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan la kufanya mazoezi ya Viungo.

 Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini (wa pili kushoto) akishiriki mazoezi ya viungo na  baadhi ya watumishi wa Umma,wanafunzi na wananchi katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji Bariadi.
Baadhi ya Watumishi na wanafunzi wakifanya mazoezi ya viungo  katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji Bariadi leo kutekeleza agizo la Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan.
Timu ya Sekretarieti ya Mkoa ikivuta kamba dhidi ya timu ya Halmashauri ya Mji Bariadi (haipo pichani) katika  Uwanja wa Halmashauri ya Mji Bariadi.
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini akizungumza na Viongozi na watumishi wa Umma, wanafunzi na wananchi walioshiriki mazoezi ya viuongo na michezo mbalimbali mjeni Bariadi ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan.
Baadhi ya vijana wa Bariadi walioshiriki mchezo wa mbio za baiskeli leo mara baada ya viongozi, watumishi wa umma na wanafunzi kumaliza mazoezi ya viungo.
Baadhi ya watumishi wakishiriki mbio za mita 100 wakati wa utekelezaji wa agizo la Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan la kufanya mazoezi ya Viungo na michezo mbalimbali mjini Bariadi.

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!