Monday, August 20, 2018

WANANCHI SIMIYU WAHIMIZWA KUWEKEZA KWENYE UJENZI WA MIUNDOMBINU YA ELIMU

Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Kabeho amewahimiza wananchi wa wilaya ya Maswa mkoani Simiyu kuwekeza katika miundombinu ya elimu ili kukabiliana na msongamano wa wanafunzi  unaotokana na utekelezaji wa Sera ya Elimu  bila malipo.

Kabeho ametoa wito huo katika kijiji cha Jija wakati akizindua mradi wa Maji  na vyumba  viwili vya madarasa katika Shule ya Sekondari Jija, wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru wilayani humo Agosti 19, 2018 .

Amesema kutokana na utekelezaji wa sera ya Elimu bila malipo kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi wanaoandikishwa darasa la awali, darasa la kwanza wanaojiunga na kidato cha kwanza, hivyo wananchi wawekeze katika ujenzi wa madarasa na  miundombinu mingine ya elimu ili wanafunzi waweze kusoma katika mazingira mazuri.

Katika hatua nyingine Kabeho amewataka Watumishi wa Umma kuacha kufanya kazi kwa mazoea badala yake wafanye kazi kwa kwa weledi na ufanisi mkubwa wakiizingatia sheria, kanuni na taratibu.

“Mhe. Rais anaposema HAPA KAZI TU anamaanisha fanya kazi kwa bidii,  zingatia sheria, taratibu na kanuni, wapo watumishi wanafanya kazi pale tu palipo na maslahi mahali ambapo hapana maslahi hamwajibiki, achaneni na kufanya kazi kwa mazoea fanyeni kazi kwa kujituma na kwa ufanisi” alisema

Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi Mashimba Ndaki akizungumza kwa niaba wa wananchi ameishukuru Serikali kwa namna inavyoendelea kuwaletea wananchi maendeleo,  ambapo ameshukuru kwa kupelekea miradi hiyo ya maji na elimu katika Kijiji cha Jija ,huku akisisitiza wazazi kutowakatisha masomo watoto wao hususani wa kike
.
Mwenge wa Uhuru ukiwa Wilayani Maswa  umepitia miradi yenye thamani ya milioni 516, kutoka sekta ya Elimu, Afya, Maji, Maendeleo ya Jamii (Vikundi vya vijana na wanawake)

Mbio za mwenge mkoani SIMIYU zimehitimishwa Agosti 19  baada ya kuanza kukimbizwa Agosti 14 ukitokea mkoani Singida na unatarajiwa kukabidhiwa mkoani Shinyanga Agosti 2018.
MWISHO

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018, Ndg. Charles Kabeho akifungua vyumba viwili vya madasa katika Shule ya Sekondari Jija wilayani Maswa, Agosti 19, 2018, wakati Mwenge wa Uhuru ukiwa katika mbio zake wilayani humo
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru  2018, Ndg. Charles Kabeho akishuhudia jiwe la Ufunguzi wa Madarasa mawili aliyofungua katika Shule ya Sekondari Jija wilayani Maswa, Agosti 19, 2018 likisomwa, wakati Mwenge wa Uhuru ukiwa katika mbio zake wilayani humo.
Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Dkt. Seif Shekalaghe akisalimiana na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru  2018, Ndg. Charles Kabeho mara baada ya kukabidhiwa rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Tano Mwera(hayupo pichani), Agosti 19, 2018. 
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018, Ndg. Charles Kabeho akimtwisha ndoo mkazi wa Jija mara baada ya kuzindua mradi wa maji wa Jija wilayani Maswa Agosti 19, wakati Mwenge wa Uhuru ukiwa katika mbio zake wilayani humo.
Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Dkt. Seif Shekalaghe akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkimbiza Mwenge Kitaifa Dominik Rweyemamu Njunwa, mara baada ya makabidhiano kati ya Wilaya ya Busega na Maswa yaliyofanyika Kijiji cha Jija kukamilika, Agosti 19, 2018.
Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Dkt. Seif Shekalaghe(kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Tano Mwera wakitakiana heri mara baada ya kukamilika kwa makabidhiano ya mwenge wa Uhuru baina yao, yaliyofanyika katik a Kijiji cha Jija Wilayani Maswa Agosti 19,2018.
Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Dkt. Seif Shekalaghe(kushoto) na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018, Ndg. Charles Kabeho wakiteta jambo mara baada ya madarasa mawili katika Shule ya Sekondari Jija kufunguliwa na kiongozi huyo Agosti 19, 2018, wakati Mwenge wa Uhuru ukiwa katika mbio zake wilayani humo

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Dkt. Fredrick Sagamiko(kushoto)  akisalimiana na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru  2018, Ndg. Charles Kabeho mara baada ya kukabidhiwa rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Tano Mwera(hayupo pichani) kwa Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt. Seif Shekalaghe, Agosti 19, 2018.
 Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru  2018, Ndg. Charles Kabeho na Viongozi wa Wilaya ya Maswa wakisikiliza taarifa ya ujenzi wa Nyumba ya Mtumishi katika Kituo cha Afya cha Malampaka, kabla ya Kiongoi huyo kukagua na kufungua jengo hilo Agosti 19, 2018,  wakati Mwenge wa Uhuru ukiwa katika mbio zake wilayani humo.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru  2018, Ndg. Charles Kabeho akifuatilia nyaraka mbalimbali zinazoonesha uthibitisho wa fedha za Halmashauri ya Wilaya ya Maswa zilizotolewa kama mkopo kwa vikundi vya Vijana na Wanawake, kabla ya kukagua kazi za Vikundi hivyo, wakati Mwenge wa Uhuru ukiwa katika mbio zake wilayani humo Agosti 19, 2018.


Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru  2018, Ndg. Charles Kabeho akizungumza na viongozi wa Wilaya ya Maswa, kabla ya kuzindua Mradi wa Maji wa Kijiji cha Jija wakati Mwenge wa Uhuru ukiwa katika mbio zake wilayani humo Agosti 19, 2018.Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Dkt. Seif Shekalaghe(kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Tano Mwera wakitakiana heri mara baada ya kukamilika kwa makabidhiano ya mwenge wa Uhuru baina yao, yaliyofanyika katik a Kijiji cha Jija Wilayani Maswa Agosti 19,2018.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru  2018, Ndg. Charles Kabeho akizungumza na viongozi wa Wilaya ya Maswa, wakati Mwenge wa Uhuru ulipopita katika Mradi wa Jengo la Bweni ukiwa katika mbio zake wilayani humo Agosti 19, 2018.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru  2018, Ndg. Charles Kabeho akisalimiana na Wajasiriamali kutoka katika Vikundi vya wakina mama na vijana, wakati alipopita na kuona kazi zao, wakati Mwenge wa Uhuru ukiwa katika mbio zake wilayani humo Agosti 19, 2018.
Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Dkt. Seif Shekalaghe(kulia), akikiri kupokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Tano Mwera katika makabidhaiano yaliyofanyika katika Kijiji cha Jija wilayani Maswa, wakati Mwenge wa Uhuru ukiwa katika mbio zake wilayani humo Agosti 19, 2018.
Vijana wa Wilaya ya Maswa wakimvisha skafu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru  2018, Ndg. Charles Kabeho mara baada ya kuwasili wilayani humo akitokea wilayani Busega, tayari kwa kuanza mbio za  Mwenge wa Uhuru wilayani humo Agosti 19, 2018.
Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Tano Mwera akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Dkt. Seif Shekalaghe(kulia), Mwenge wa Uhuru tayari kwa kuanza kuukimbiza katika Wilaya ya Maswa, Agosti 19, 2018. 

Saturday, August 18, 2018

VIONGOZI WATAKIWA KUWAKUMBUSHA WAZAZI KUCHANGIA CHAKULA SHULENI NA KUNUNUA SARE ZA WATOTO WAOViongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu wametakiwa kuwakumbusha wazazi na walezi kuwanunulia watoto wao sare za shule na kuchangia chakula mashuleni ili watoto wao waweze kusoma kwa utuivu na umakini wanapokuwa shuleni  na  kuzuia utoro .

Rai hiyo imetolewa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018, Ndg. Charles Kabeho wakati wa makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru baina ya Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga na Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Tano Mwera yaliyofanyika katika Kijiji cha Mkula wilayani humo.

Kabeho amesema Serikali ya awamu ya tano imefuta ada na michango mbalimbali iliyokuwa kero kwa wananchi ili kila mtoto wa Kitanzania apate haki ya Elimu kuanzia darasa la awali mpaka Kidato cha nne bila malipo , hivyo wazazi na walezi wanapaswa kuwanunulia watoto wao sare za shule pamoja na mahitaji yao mengine ya shule ikiwa ni pamoja na daftari na kalamu.

“ Kwa sasa wazazi hamlipi tena ada wala michango  wajibu wenu ni kununua sare za shule na kununua mahitaji mengine kama kalamu, daftari na mabegi ,Serikali inaendelea kuhamasisha mtimize wajibu wenu, lakini pia namuomba Mkurugenzi awaeleze Walimu wakuu sare za Halmashauri yake ni zipi ili nao wawakumbushe wazazi kwanunulia watoto wao sare hizo” alisema.

Aidha, Kabeho amesema ni vema  wazazi  na walezi wakachangia chakula shuleni ili kuwafanya wanafunzi waweze kusoma kwa utuivu na umakini wanapokuwa shuleni  na  kuzuia utoro .

“Tunaomba pia mtimize wajibu wenu kuchangia chakula shuleni kwa sababu unapotoa chakula shuleni tunapunguza utoro , tunaongeza umakini na ufuatiliaji kwa wanafunzi pale wanapofundishwa, wanafunzi wengi wao wanatoroka pale wanapohisi njaa na wakiondoka baadhi yao hawarudi” alisema Kabeho.

Katika hatua nyingine Mwenge wa Uhuru ukiwa Wilayani Busega na kupitia miradi saba yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 900 katika sekta mbalimbali ikiwemo Afya, Elimu na Viwanda.

Akizungumza mara baada ya kufungua vyumba vitatu vya madarasa na matundu matano ya vyoo katika Shule ya Sekondari Nasa, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018, Ndg. Charles Kabeho ameipongeza Serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya elimu ambayo itasaidia kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.

Akizungumza na Wananchi baada ya kufungua Wodi ya wazazi katika Kituo cha Afya cha Nasa Kabeho amewashukuru wananchi kwa namna wanavyojitolea nguvu kazi katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo katika Kituo hicho cha Afya cha Nasa.

Akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa Wodi hiyo ya wazazi, Katibu wa Afya Wilaya wa Wilaya ya Busega Huruma Temu amesema kuwa wodi hiyo katika kituo cha Afya Nassa hadi kukamilika kwake imegharimu kiasi cha shilingi Milioni 109 ikiwa ni fedha za wafadhili kutoka UNFPA.

Haruna alibainisha kuwa lengo kuu la kujenga wodi hiyo ya wazazi ni kuboresha afya ya uzazi na kupunguza idadi ya vifo vya akinamama na watoto Wilayani Busega.

MWISHO

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeho akitoa Ujumbe wa Mwenge wa Uhuru mwaka 2018 katika Kijiji cha  Mkula wilayani Busega, wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru wilayani humo, Agosti 18, 2018.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeho akikagua Ujenzi  wa Vyumba vitatu vya madarasa katika Shule ya Sekondari Nasa  wilayani Busega kabla ya kuvifungua, wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru  wilayani humo, Agosti 18, 2018.
 Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeho akiweka jiwe la ufunguzi  wa  Vyumba vitatu vya madarasa katika Shule ya Sekondari Nasa  wilayani Busega , wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru  wilayani humo, Agosti 18, 2018.
Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Tano Mwera(kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga wakikabidhiana Mwengewa Uhuru tayari kwa ajili kuanza mbio zake wilayani Busega Agosti, 2018. 
Mkurugenzi wa Nassa Alovera Proccesors , Bw. Venance Mdunga (wa pili kulia) akitoa maelezo kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeho(wa pili kulia), wakati alipofika kukagua shamba lake ambalo linatoa malighafi ya kutengeneza bidhaa zitokanazo na Alovera.
Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Tano Mwera(kushoto) akisalimiana na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeho, mara baada ya Mwenge wa Uhuru, kufika wilayani Busega, Agosti 17, 2018. 
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeho akiweka Jiwe la Msingi katika Kiwanda cha Kukoboa  Mpunga na kupanga madaraja  kilichopo Lamadi Bariadi, Agosti 17, 2018.
Askari wa FFU na Mkimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa Riziki Hassan Ali wakiondoka na Mwenge wa Uhuru katika Viwanja vya Shule Sekondari Nassa wilayani Busega, wakati ukiwa  katika mbio zake wilayani humo, Agosti 17, 2018
Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Tano Mwera akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka Kwa Mkimbiza  Mwenge Kitaifa Riziki Hassan Ali kutoka Mkoa wa Kusini Unguja, kwa ajili ya kuanza ratiba ya Mbio za Mwenge wa Uhuru wilayani humo, Agosti 18, 2018.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeho akikagua  Wodi ya Mama na Mtoto iliyopo katika Kituo cha Afya cha Nasa wilayani Busega, wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru wilayani humo, Agosti 18, 2018.
 Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeho akizungumza na viongozi na Wananchi mara baada ya kufungua Kituo cha Mafuta cah Masanza Kona, wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru wilayani humo, Agosti 18, 2018. 


Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeyo(katikati) akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Tano Mwera na Mkurugenzi  wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Bw. Anderson Njiginya, wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru wilayani humo, Agosti 18, 2018.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeho akisalimiana na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Mhe. Mickness Mahela, wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru wilayani humo, Agosti 18, 2018.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeho akisalimiana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Bw. Anderson Njiginya wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru wilayani humo, Agosti 18, 2018.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeho akipewa maelezo na Mfanyakazi wa Kiwanda cha Nassa Alovera Proccesors juu ya namna wanavyotengeneza bidhaa mbalimbali na dawa zinazozalishwa   zinazozalishwa.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeho akiangalia mchele ulikobolewa ukiwa katika hatua za mwisho kupangwa na kuwekwa  wenye madaraja, kabla ya kukiwekea kiwanda hicho jiwe la msingi, wakati Mwenge ukiwa katika Mbizo zake wilayani humo Agosti 17, 2018.  .

Friday, August 17, 2018

WANANCHI SIMIYU WASHUKURU SERIKALI KUJENGA DARAJA IKUNGULYABASHASHI, WAKIRI MAWASILIANO USAFIRISHAJI KUIMARIKA


Wananchi wa Vijiji vya Mkuyuni, Ikungulyabashashi, Mwahalaja na Lulayu Kata ya Ikungulyabashashi, wilayani Bariadi Mkoani Simiyu wameishukuru Serikali kwa kukamilisha ujenzi wa Daraja la Ikungulyabashashi na kukiri kuwa kukamilika kwa daraja hilo kutarahisisha na kuimarisha mawasiliano na usafirishaji.

Hayo yamebainishwa na baadhi ya wananchi kutoka katika kata Vijiji hivyo mara baada ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeho kufungua daraja hilo, wakati Mwenge wa Uhuru ukiwa katika mbio zake wilayani Bariadi Agosti 17, 2018.

Wamesema awali kabla ya kukamilika  kwa daraja hilo walikuwa wakipata changamoto ya kusafirisha mazao na mifugo yao  na wakati mwingine kusafiri wao wenyewe hususani kipindi cha masika hivyo kufanya mawasiliano kuwa magumu kati ya pande mbili zinazotenganishwa na daraja hili.
“Kukamilika kwa daraja hili kutaongeza uzalishaji kwa kuwa mawasiliano ya pande zote mbili yatakuwa vizuri tofauti na mwanzo ambapo tulikuwa tunapata shida ya kusafirisha mazao yetu, mifugo  na sisi wenyewe kusafiri kutoka upande mmoja hadi mwingine hasa wakati wa masika” alisema Joshua Yakobo mkazi wa Kilalo.

 “Tunaishukuru sana Serikali kukamilisha Daraja hili ambalo litarahisisha sana mawasiliano sasa hivi wakazi wa vijiji vya Kata ya Ikunguyabashashi watakuwa wanavuka katika daraja hilo kwenda kufanya biashara katika minada ya Dutwa, Nyakabindi na Bariadi Mjini” alisema Benjamin Malala.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018, Ndg. Charles Kabeho alikagua ujenzi wa daraja hilo na kuridhishwa hatimaye akaupongeza Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi kwa kujenga daraja hilo kwa kuzingatia viwango.

Akisoma taarifa ya Ujenzi wa Daraja hilo Meneja wa Wakala wa Barabara Mijini naVijijini(TARURA), Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Mhandisi. Nyamagulula Masatu amesema daraja la Ikungulyabashashi lenye urefu wa mita 16.8, upana wa mita 6.6 linajengwa kwa ufadhili wa Department For International Developments (DFID) kwa usimamizi wa TARURA.

Ameongeza kuwa ujenzi wa daraja hili utagharimu jumla ya shilingi 345,293,434/= huku akibainisha kuwa faida kuu ya mradi huu ni kurahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo kutoka mashambani kwa wakulima kwenda kwenye masoko.

Mwenge wa Uhuru ukiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi umepita katika miradi minne yenye thamani ya shilingi milioni 568 ikiwemo mradi wa maji wa Kasoli na Shule ya Msingi Otto Busese ambayo imejengwa kwa ufadhili wa Kiwanda cha kuchambua pamba cha Alliance Ginnery Limited kiilichopo Kasoli Bariadi.

Meneja Mkuu wa Kiwanda cha Kuchambua Pamba cha Aliance Ginnery, Bw. Boaz Ogola amesema kuwa Kampuni yake inatambua kuwa nayo ni sehemu ya jamii, hivyo imeamua kushirikiana na jamii katika kuchangia maendeleo ya huduma za jamii katika elimu, afya na maji.

“Tumeshirikiana na jamii katika kuimarisha huduma za jamii,  Kasoli tumechimba kisima cha maji, tumejenga madarasa mawili na matundu matano ya vyoo katika kila shule inayotuzunguka, tumejenga Bweni la watoto wa kike katika shule ya Sekondari Mwamlapa na tunaendelea kushirikiana na jamii kuhakikisha kuwa tunaunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha elimu” amesema Ogola.

Mwenge wa Uhuru unaendelea na mbio zake mkoani Simiyu ambapo Agosti 18 utakuwa katika Wilaya ya Busega, Agosti 19 utakuwa katika Wilaya ya Maswa na Agosti 20 utakabidhiwa katika Mkoa wa Shinyanga.
MWISHO
Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeho akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Daraja la Ikungulyabashashi wilayani Bariadi mkoani Simiyu, wakati Mwenge wa Uhuru ukiwa katika mbio zake wilayani humo, Agosti 17, 2018.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeho akifungua Daraja la Ikungulyabashashi wilayani Bariadi mkoani Simiyu, wakati Mwenge wa Uhuru ukiwa katika mbio zake wilayani humo, Agosti 17, 2018.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeho akizungumza na Wanafunzi wanachama wa Klabu ya Wapinga Rushwa katika Shule ya Sekondari Nyasosi katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, wakati Mwenge wa Uhuru ukiwa katika mbio zake wilayani humo, Agosti 17, 2018.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeho akiangalia kiatu kilichotengenezwa na Kikundi cha Vijana wa Dutwa wilayani Bariadi Mkoani Simiyu, wakati Mwenge wa Uhuru ukiwa katika mbio zake wilayani humo, Agosti 17, 2018.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeho akimtwisha ndoo ya maji Bi. Joyce Paulo mkazi wa Kijiji cha Kasoli wiayani Bariadi mkoani Simiyu mara baada ya kufungua mradi wa kisima kirefu cha maji Kasoli, wakati Mwenge wa Uhuru ukiwa katika mbio zake wilayani humo, Agosti 17, 2018.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeho na viongozi wengine w Wilaya ya Bariadi wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Festo Kiswaga(kulia) wakishangilia  mara baada ya kiongozi huyo kufungua Shule ya Otto Busese (iliyojengwa kwa ufadhili wa Alliance Ginnery Limited), wakati Mwenge wa Uhuru ukiwa katika mbio zake wilayani humo, Agosti 17, 2018.
Mkimbiza Mwenge Kitaifa mwaka 2018, Ndg Ipyana Alinuswe Mlilo akitoa Ujumbe wa Mwenge wa Uhuru mwaka 2018 katika Shule ya Sekondari Kasoli wiayani Bariadi, wakati Mwenge wa Uhuru ukiwa katika mbio zake wilayani humo, Agosti 17, 2018.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Mhandisi. Wilbert Siogopi akimkaribisha Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeho, kabla ya kukabidhiwa Mwnge wa Uhuru na Mkurugnezi mwenzake wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi , Ndg. Melkizedeck Humbe Agosti 17, 2018.
Mwananchi Clement Mlanda akiwa katika picha ya pamoja na Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeho huku akiwa amaeshika Mwenge wa Uhuru, mara baada ya nyumba yake kufunguliwa na Mwenge wa Uhuru mwaka 2018, Agosti 17, 2018.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Bariadi, Bw. Albert Rutaihwa akisalimiana na Mkimbiza Mwenge Kitaifa mwaka 2018, Ndg Issa Abass Mohamed mara baada ya kukabidhiwa rasmi kutoka Halmashauri ya Mji wa Bariadi kwena Halamshauri ya Wilaya ya Bariadi, wakati Mwenge wa Uhuru ukiwa katika mbio zake wilayani humo, Agosti 17, 2018.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeho akitoa Ujumbe wa Mwenge wa Uhuru mwaka 2018 katikaViwanja vya Shule ya Msingi Ikungulyabashashi wilayani Bariadi, wakati Mwenge wa Uhuru ukiwa katika mbio zake wilayani humo, Agosti 17, 2018.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Mhandisi. Wilbert Siogopi (kushoto) akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Ndg. Melkizedeck Humbe wakati Mwenge wa Uhuru ukiwa katika mbio zake wilayani humo Agosti 17, 2018
Meneja wa Wakala wa Barabara Mijini naVijijini(TARURA), Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Mhandisi. Nyamagalula Masatu akiwa ameshika Mwenge wa Uhuru pamoja na Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeho akitoa Ujumbe wa Mwenge wa Uhuru mwaka 2018, mara baada ya daraja la Ikungulyabashashi kufunguliwa na Mwenge wa Uhuru Agosti 17, 2018.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Mhandisi. Wilbert Siogopi (kulia) akimkabidhi Mwenge wa Uhuru Mkuu wa Wilaya ya Bariadi , Mhe. Festo Kiswaga mara baada ya kuupokea kutoka kwa kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Ndg. Melkizedeck Humbe, ili aweze kuendelea na itifaki, Agosti 17, 2018.

KIWANDA CHA USHONAJI KUAJIRI VIJANA NA WANAWAKE SIMIYU


Kukamilika kwa kiwanda cha ushonaji  katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi kutasaidia kuongeza ajira, ujuzi na vipato vya wananchi wa Simiyu hususani  wanawake na vijana.

Kiwanda hicho kinakadiriwa kujengwa kwa fedha kiasi cha shilingi milioni 85 hadi kukamilika kwake ambapo itatoa pia fursa kwa wakazi wa mji wa Bariadi na Mkoa mzima kwenda kujifunza ushonaji na ubunifu wa mitindo mbalimbali ya nguo ambayo baadae wataweza kujiajiri na kujiongezea kipato.

Akitoa taarifa ya ujenzi wa kiwanda hicho  mbele ya kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018 Ndg. Charles Kabeho  kabla ya kuweka jiwe la msingi kiwanda hicho ,Mhandisi  wa Halmashauri ya Mji Samwel Msolini amesema Halmashauri ilipokea msaada wa vyerehani 50,  kutoka Serikali ya Jamhuri ya China, vyerehani 25 vikiwa vya umeme na vingine 25 ni vya kawaida.

Ameongeza kuwa baada ya kupokea msaada huo Halmashauri imeamua kuanzisha Kiwanda hicho ili kuviwezesha kutumika na hatimaye Halmashauri ipate mapato, kutoa ajira kwa wananchi na wananchi kupata huduma za mavazi yenye kiwango.
  
“”Lengo la Ujenzi wa Kiwanda cha Ushonaji ni kwa ajili ya kushona nguo kwa mahitaji mbalimbali ikiwa ni pamoja na nguo zinazovaliwa  kwenye sherehe mbalimbali, sare za shule na maeneo ya kazi, mradi huu ukikamilika utaongeza mapato ya Halmashauri, kutoa ajira kwa wananchi na wananchi watapata huduma ya mavazi” alisema Msolini..

Aidha,  akiweka jiwe la msingi katika kiwanda hiki, kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Kabeho amefurahishwa sana na akapongeza Halmashauri kwa kubuni mradi huo ambao amesema utakuwa na manufaa kwa wananchi na Halmashauri.

“Kiwanda hiki  kitawasaidia wajasiriamali wanaojihusisha na masuala ya ushonaji  kupata kipato, kitawasaidia wananchi kujiajiri wenyewe, lakini pia Halmashauri nayo itapata mapato” alisema Charles Kabeho..

Angello Michael mkazi wa mji wa Bariadi alisema kiwanda hicho kitasaidia vijana na wanawake wengi ambao hawana kazi za kufanya na kubadilisha maisha na vipato vyao kwa baadaye.

Katika hatua nyingine Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018 amewapongeza Wananchi na Viongozi katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi kwa namna walivyoshirikiana katika ujenzi wa Miundombinu ya Elimu katika Shule ya msingi Kilulu na akatoa wito wananchi kwenda kujifunza ujenzi wa majengo mazuri yenye kiwango kwa gharama nafuu.

Aidha Mwenge wa Uhuru ukiwa katika Halmashauri Mji wa Bariadi,  pamoja na kuweka Jiwe la Msingi la kiwanda cha ushonaji, umepitia miradi mingine katika Sekta ya Elimu, Afya, Mazingira, Sekta Binafsi  na Ujenzi.

MWISHO
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Kabeyo akiweka jiwe la Msingi la Jengo/Kiwanda cha Ushonaji Mjini Bariadi, wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Agosti 16, 2018. 
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Mhe. Dkt. Joseph Chilongani katika makabidhiano Kijiji cha Gambasingu Wilayani Itilima, Agosti 16, 2018.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga(kulia), Katibu Tawala Mkoa(kushoto) wakiwa pamoja na baadhi ya Wakimbiza Mwenge Kitaifa mwaka 2018 na Paroko wa Parokia ya Mtakatifu John mara baada ya Mwenge wa uhuru kuona msitu wa asili na mradi wa maji.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Kabeyo akifungua mabomba ya maji ili kujiridha kama ni kweli yanatoka, kabla ya Kufungua mradi wa maji wa Gitoya Mjini Bariadi, wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Agosti 16, Bariadi.
Askari wa Kikosi cha Kuzuia Ghasia(FFU) na baadhi ya Wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa, wakielekea eneo la Mradi wa kufungua madarasa matatu katika Shule ya Msingi Kilulu Mjini Bariadi, Agosti 16, 2018.
 Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Kabeyo akizungumza na viongozi na wananchi wa Bariadi Mjini mara baada ya kuweka jiwe la Msingi la Jengo/Kiwanda cha Ushonaji Mjini Bariadi, wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Agosti 16, 2018. 
Mfanyabiashara wa Mjini Bariadi, Bw. John Sabu na akiwa ameshika Mwenge wa Uhuru mara baada ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Kabeyo( wa pili kushoto), kuweka Jiwe la Msingi la Hoteli yake ya SweetDream,(kulia)ni mtoto wao.
 Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Kabeyo akiweka jiwe la Msingi katika Hoteli ya Sweet Dreams ya Mjini Bariadi inayomilikiwa na Mfanyabiashara John Sabu, wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Mjini Bariadi, Agosti 16, 2018. 


Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!