Wednesday, June 1, 2016

MASWA WATEKELEZA AGIZO LA RAIS LA KUTENGENEZA MADAWATI KWA ASILIMIA 75



Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu imetekeleza agizo la Rais John Pombe Magufuli la kutengeneza madawati kwa asilimia 75, ambapo hadi kufikia Mei 31mwaka huu, imetengeneza madawati 19,655 kati ya  26,261 yanayohitajika kwa shule za msingi na meza 10,943 kati ya 9,359 zinazohitajika na viti 10,810 kati ya 9,359 vinavyohitajika na kufanya kuwa na ziada ya meza 1,432 na viti 1,277 kwa shule za sekondari. 

Hayo  yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Rosemary Kirigini wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya utekelezaji wa agizo hilo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony J. Mtaka alipofanya ziara kuona namna agizo hilo linavyotekelezwa wilayani humo.
Mhe. Kirigini alisema wamefikia hatua hiyo kutokana na kuwashirikisha wadau mbalimbali, kunua mbao na  kutumia  mafundi ambao ni wanafunzi wa Chuo cha Ufundi cha Binza, ambao wamekuwa wakitengeneza madawati 500 hadi 1000 kwa siku, kwa gharama ya shilingi 21,625/= kwa dawati moja.

Akipokea taarifa ya wilaya ya Maswa, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu mhe. Anthony J. Mtaka ameupongeza uongozi wa wilaya ya Maswa kwa hatua waliyofikia na ubunifu walioutumia katika kutafuta mbao na kuwatumia mafundi kutoka Chuo cha Ufundi cha Binza, hali iliyosaidia kupunguza gharama na akazitaka wilaya nyingine kutumia uzoefu wa Maswa ili zikamilishe agizo la Mhe. Rais kwa wakati uliopangwa.
“Hiki chuo ni cha Serikali, wakipewa mbao wanatengeneza dawati moja kwa shilingi 21,625 kama alivyotuambia DC,kwa nini wilaya zote za mkoa huu wasione umuhimu wa kuwatumia hawa vijana wa chuo hiki kuwafanyia kazi yao. Watu wanatengeneza dawati moja kwa shilingi 70,000/= sasa si bora tukatumia chuo chetu hiki ili tupunguze gharama na kumuwezesha Mkuu wa chuo akapata fedha zitakazomsaidia kuendesha chuo badala ya kutegemea ruzuku ya serikali?” alisema Mtaka.
  
Aidha, Mtaka amepiga marufuku tabia ya kutumia viti,meza na madawati ya wanafunzi katika shughuli nyingine kama mikutano ya hadhara kwa kuwa kuhamisha madawati au viti kutoka sehemu moja kwenda nyingine kunachangia uharibifu.

Wakati huo huo Mtaka amewataka Maafisa Elimu kuweka mikakati ya kitaaluma ili kuwafanya kuongeza ufaulu kwa wanafunzi ikiwa ni pamoja na kuweka utaratibu wa kufanya mitihani ya majaribio ya mara kwa mara kwa madarasa ya mitihani na kuanzisha na kuzisimamia klabu za masomo mbalimbali mashuleni

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa, Jumanne A. Sagini amesema Halmashauri ione umuhimu wa kupima maeneo yote ya shule ili yatambuliwe yasivamiwe na wananchi kwa kufanya shughuli nyingine kinyume na utaratibu. 

Halmashauri ya Wilaya ya Maswa ina jumla ya shule za Msingi 121 zenye wanafunzi  78,783 na shule za sekondari 40  kati ya hizo 36 ni za Serikali ambazo zina jumla ya wanafunzi 9359. 
Mkuu wa Wilaya ya MaswaMhe. Rosemary Kirigini (kulia) alitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa Mhe. Anthony J. Mtaka (wa pili kulia), kuhusu madawati yaliyotengenezwa katika Chuo cha Ufundi cha Binza wakati wa ziara yake wilayani humo. Wengine ni viongozi wa Mkoa na Wilaya walioshiriki katika ziara hiyo.Picha na Stella A. Kalinga.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (wa tatu kushoto) akizungumza na viongozi wa wilaya ya Maswa (hawapo pichani) kabla ya kufanya ziara ya kukagua utekelezaji wa agizo la Mhe.Rais la utengenezaji wa madawati wilayani humo, (wa pili kushoto) Katibu Tawala Mkoa, Jumanne Sagini na (wa nne kulia) ni Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Rosemary Kirigini. Picha Na Stella A. Kalinga.

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!