Friday, July 29, 2016

WAKURUGENZI MKOANI SIMIYU WAAGIZWA KUTENGA BAJETI ZA MAAFISA KILIMO



Na Stella Kalinga (Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu)
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony J. Mtaka amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote mkoani humo kutenga bajeti kwa ajili ya kuwawezesha Maafisa kilimo wa Vijiji,Kata na Wilaya kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Mtaka ametoa agizo hilo wakati alipokuwa akizungumza na Viongozi na Maafisa Kilimo katika kikao kilichofanyika Mjini Bariadi ambacho kilihudhuriwa na Wakuu wa wilaya,Wenyeviti wa Halmashauri,Wakurugenzi na Makatibu Tawala Wilaya kutoka  katika wilaya zote tano za mkoa huo.

Mtaka amesema Maafisa Kilimo wanapaswa kuwezeshwa kwa kupewa vyombo vya usafiri kama pikipiki na magari pamoja na mafuta, ili waweze kuwafikia wakulima katika maeneo yao kwa ajili ya kuwapa ushauri wa kitaalam kila wanapowahitaji katika kuendeleza kilimo bora na chenye tija.

“Mwaka huu kilimo kwa mkoa wetu ni  kipaumbele cha pili na Halmashauri za Mkoa huu zinategemea kilimo kwa takribani asilimia 90 ya mapato yake ya ndani, ipo haja  kuwawezesha maafisa kilimo kwa kuwa wana mchango kubwa katika mapato ya Halmashauri. Ningependa kuona mwaka 2016/2017 hadhi ya Maafisa Kilimo inapanda, Wakurugenzi muwathamini hawa wataalam ndiyo wanaowasaidia kupata hayo mapato katika pamba, choroko, dengu, mpunga na mazao mengine”, alisema Mtaka.

Aidha, kufuatia makubaliano kati ya Serikali ya  Tanzania na India yaliyofanywa hivi karibuni kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.John Pombe Magufuli na Waziri Mkuu wa India juu ya biashara ya mazao ya jamii ya mikunde kama choroko, dengu na mbaazi takribani tani milioni sita, Mtaka amesema Mkoa wa Simiyu unayo fursa kubwa ya  kuzalisha mazao haya kwa takribani asilimia 60 kama ilivyo katika zao la pamba, kwa kuwa kuna ardhi yenye rutuba na wananchi wanalima mazao hayo. 

Katika kufikia azma hiyo, Mtaka amewataka Maafisa kilimo kutumia muda huu kufanya tafiti katika vituo mbalimbali vya utafiti  juu ya mbegu bora, kabla ya msimu wa mazao ya mikunde haujaanza ili wakati utakapofika uzalishaji wa mazao hayo ufanyike kitaalam na kuongeza uzalishaji kuliko ilivyo sasa.

Wakati huo huo Mtaka amewaagiza viongozi na Maafisa Kilimo kutoka katika wilaya zote kuwa na mashamba ya mifano ambayo yatatumika kama mashamba darasa kwa wananchi ili wananchi wajifunze kutoka kwao kwa kuwaonesha kuwa maelezo wanayoyatoa yanatekelezeka. 

Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Uchumi na Uzalishaji katika Sekretarieti ya Mkoa wa Simiyu, Bw. Joseph Nandrie ametoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Simiyu kulima mazao yanayostahimili ukame kama mihogo na mtama ili kukabiliana na baa la njaa.

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga akikiri kupokea maelekezo ya Mkuu wa Mkoa amewataka Maafisa Kilimo kuandaa mipango kazi kwa ajili ya utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na kuyawasilisha kwa viongozi wao wa wilaya ili yaanze kutekelezwa.

Jumla ya Maafisa kilimo 203 kutoka katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Busega, Itilima, Maswa , Meatu na Halmashauri ya Mji  Bariadi wameshiriki katika kikao hiki ambacho kililenga kutoa mwelekeo wa Sekta ya Kilimo kama kipaumbele cha Pili Mkoani Simiyu kwa mwaka 2016/2017.


)- Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony J. Mtaka akizungumza na Viongozi na Maafisa Kilimo wa mkoa huo(hawapo pichani) katika kikao kilichofanyika mjini Bariadi kwa lengo la kujadili mwelekeo wa sekta ya kilimo kama kipaumbele cha pili Mkoani Simiyu kwa mwaka huu, (kushoto) Kaimu Katibu Tawala Mkoa, Bw. Donatus A. Weginah (Picha na Ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Simiyu)
Viongozi na Maafisa kilimo wa Mkoa wa Simiyu, wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Anthony J. Mtaka (hayupo pichani) katika kikao kilichofanyika mjini Bariadi kwa lengo la kujadili mwelekeo wa sekta ya kilimo kama kipaumbele cha pili Mkoani Simiyu kwa mwaka huu(Picha na Ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Simiyu)
)-Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi Mkoa waSimiyu, Ndg. Jeremia Shigala akichangia katika kikao kilichofanyika mjini Bariadi kwa lengo la kujadili mwelekeo wa sekta ya kilimo kama kipaumbele cha pili Mkoani Simiyu kwa mwaka huu (Picha na Ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Simiyu)
Wakuu wa Wilaya wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa(hayupo pichani) katika kikao kilichofanyika mjini Bariadi kwa lengo la kujadili mwelekeo wa sekta ya kilimo kama kipaumbele cha pili Mkoani Simiyu kwa mwaka huu, (kutoka kushoto), Mhe. Tano Mwera (Busega),Mhe. Joseph Chilongani(Meatu), Mhe. Benson Kilangi (Itilima ) na Mhe. Seif Shekalaghe .(Picha na Ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Simiyu)


wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony J. Mtaka (katikati) akizungumza na Viongozi na Maafisa Kilimo wa mkoa huo (hawapo pichani) katika kikao kilichofanyika mjini Bariadi kwa lengo la kujadili mwelekeo wa sekta ya kilimo kama kipaumbele cha pili Mkoani Simiyu kwa mwaka huu, (kushoto) Kaimu Katibu Tawala Mkoa, Bw. Donatus A. Weginah na (kulia) Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga Picha na Ofis ya mkuu wa Mkoa wa Simiyu)










Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!