Serikali ya CHINA
imeahidi kushirikiana na Mkoa wa Simiyu katika uwekezaji hususani katika maeneo ya viwanda. Kilimo na
uvuvi ili kutimiza azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli ya kuwa na Tanzania ya
Viwanda.
Hayo yamesemwa na
Balozi Mshauri wa China nchini, Bw.Zhang Biao wakati alipofanya ziara yake
mkoani Simiyu na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Mkoa wa Simiyu na wadau wa
maendeleo mkoani humo.
Balozi Zhang amesema
endapo Serikali itatengeneza mazingira
wezeshi kwa kujenga miundombinu kwa ajili ya uwekezaji, Makampuni kutoka China
yatakuwa tayari kuwekeza mkoani Simiyu.
“ Mkoa wa Simiyu una
maliasili nyingi na kwa kuwa mmeonyesha utayari Makampuni ya China yatakuja
kuwekeza kwa kasi, Serikali isaidie kuwezesha huduma za maji na umeme
zinapatikana na miundombibu ya kusafirisha malighafi kupelekeka viwandani na
kupeleka bidhaa zetu zitakazozalishwa sokoni”, alisema Balozi Zhang.
Akitoa shukrani kwa
niaba ya Serikali Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony. J. Mtaka amesema
Serikali iko tayari kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji na kuhakikisha miundombinu muhimu kama maji na
umeme inapatikana kwa ajili ya kuwezesha uwekezaji na akamuomba Balozi Zhang kuunganisha Mkoa wa Simiyu na
Makampuni ya China yaliyo tayari kuwekeza.
“ Mkoa wa Simiyu una
fursa nyingi sana za uwekezaji katika eneo la viwanda vya nguo na nyuzi kwa
kuwa unazalisha karibu asilimia 60 ya pamba ya nchini, lakini pia mkoa wetu ni wa
tatu kwa kuwa na ng’ombe wengi kwa hiyo bado kuna fursa ya uwekezaji katika
mazao ya ufugaji wa ng’ombe kama nyama, ngozi na maziwa” , alisema Mtaka.
Aidha, Mtaka alisema
kupitia sehemu ya Ziwa Viktoria mkoa una fursa ya uwekezaji katika kilimo cha
umwagiliaji ambacho alieleza kinaweza kusaidia kuinua uchumi wa wakazi wa wilaya
ya Busega na Mkoa wa Simiyu kwa ujumla, ambapo Serikali inaandaa mpango wa kuwa
na zao moja kwa wilaya moja (one product one district) ili kila wilaya iwe na zao au shughuli moja
inayowaingizia watu wake kipato.
Hii ni mara ya kwanza
kwa Balozi Mshauri wa China nchini kufika mkoani Simiyu ambapo Balozi Zhang ameahidi
kuendeleza urafiki wa nchi ya Tanzania na China ambao ulianza tangu enzi za
Rais wa awamu ya kwanza Hayati Julius K. Nyerere na kuhakikisha uhusiano kati
ya nchi hizi mbili unawanufaisha wananchi wa pande zote mbili.
0 comments:
Post a Comment