Mkuu wa Mkoa wa Simiyu
Mhe. Anthony J. Mtaka amewataka Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri
zote kutambua idadi kamili ya wanafunzi katika maeneo yao, ili fedha
zinazoletwa na Serikali kwa ajili ya elimu bila malipo zifanye kazi
iliyokusudiwa.
Mhe. Mtaka amelitoa
agizo hilo katika kikao cha kazi kilichokusudia kutoa tathmini ya elimu na
kutoa dira ya usimamizi na uendeshaji wa elimu katika mkoa, ambacho kiliwahusisha
wadau mbalimbali wa elimu wa Mkoa wa Simiyu kilichofanyika mjini Bariadi, katika
ukumbi wa Shule ya Sekondari Bariadi.
Mhe. Mtaka alisema
baadhi ya walimu wakuu na wakuu wa shule wamekuwa wakitoa takwimu zisizo sahihi
pale zinapohitajika ili waweze kuletewa fedha nyingi za elimu bila malipo kuliko idadi halisi ya
wanafunzi waliopo shuleni.
“Nawaagiza Wakuu wa
Wilaya na Wakurugenzi wote kila mmoja katika eneo lake ahakikishe anatambua idadi
kamili ya wanafunzi kwa kila shule ili kubaini wanafunzi hewa, Wakurugenzi
muwasilishe taarifa hizo katika Kamati za Ulinzi na Usalama za wilaya; katika
taarifa muoneshe hatua mlizochukua dhidi ya wakuu wa shule na walimu wakuu
waliodanganya takwimu za wanafunzi”, alisema Mtaka.
Mtaka alisema kumekuwa
na tatizo la utoro na mdondoko kwa shule za msingi na sekondari katika Mkoa wa
Simiyu ambapo wanafunzi wanaachishwa shule kwa sababu mbalimbali zikiwemo za
kuchunga mifungo na kuozwa kwa wanafunzi
wa kike.
Kufuatia kuwepo kwa tatizo
la utoro Mkuu wa Mkoa aliwataka Wakurugenzi kuwataka walimu wakuu na wakuu wa
shule kutoa maelezo ya kina juu ya matumizi ya fedha za elimu ya bila malipo
kwa wanafunzi watoro.
Aidha, Afisa
Elimu Mkoa, Mwl. Julius Nestory amewaomba Wenyeviti wa Halmashauri na Wabunge
wasaidie katika kusimamia sheria zilizoandaliwa kwa ajili ya kudhibiti suala la
utoro, ikiwa ni namna mojawapo ya
kukabiliana na ujinga kwa jamii ya watu wa Simiyu.
Wakati huo huo Mbunge wa Maswa Mashariki, Mhe. Stanslaus Nyongo amesema katika harakati za kusaidia kuondoa ujinga Mkoani Simiyu, amewaomba wafanyabiashara wa Mkoa wa Simiyu kuwekeza katika elimu ikiwa ni pamoja na kujenga shule na vyuo kwa kuwa sekta binafsi ina mchango mkubwa katika maendeleo ya elimu nchini.
Katika mikakati ya
kuongeza kiwango cha ufaulu, Mhe. Mkuu wa Mkoa aliagiza madarasa ya mitihani
kwa shule za msingi na sekondari yalelewe na viongozi na yatafutiwe utaratibu
wa kuwa na kambi za kitaaluma kama ilivyo kwa upande wa michezo, ambapo
wanafunzi kutoka maeneo tofauti watakutanishwa na kushindanishwa ili kuwajengea
uwezo na kuwaandaa kwa ajili ya mitihani ya kitaifa.
Kiwango cha ufaulu
kwa mwaka 2015 katika Mkoa wa Simiyu kimepanda ikilinganishwa na mwaka 2014 ambapo kwa upande wa darasa la saba ufaulu umepanda kufikia asilimia 61
mwaka 2015 kutoka asilimia 44 mwaka 2014, kidato cha nne asilimia 72.5 kutoka
70 mwaka 2014 na kidato cha sita 2015 ufaulu ulipanda mpaka asilimia 98.2.
0 comments:
Post a Comment