Serikali imesema itawachukulia hatua kali Wafanyabiashara wa pamba watakaochezea mizani kwa lengo la kuwaibia wananchi pale wanaponunua pamba.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mhe. Charles Tizeba wakati wa ziara yake ya siku moja Mkoani Simiyu ,alipotembelea kituo cha kununulia pamba cha N.G.S ,katika kijiji cha Luguru wilayani Itilima.
Waziri Tizeba alisema
Serikali haitavumilia vitendo vya unyonyaji dhidi ya mkulima kwa kuwa inafanya
kila jitihada kuwasaidia wakulima wa pamba ili waone umuhimu
wa zao hilo na kuhakikisha wanazalisha pamba bora.
Aidha, Waziri Tizeba ameitaka Bodi ya Pamba kuwachukulia wakulima wote watakaobainika kuuza pamba iliyochafuliwa kwa kuwekwa maji, mchanga na mafuta kwa kuwa wanaharibu ubora wa pamba na hivyo kuchangia kushusha thamani ya pamba ya Tanzania katika soko la dunia.
“Sheria ni msumeno
unakata kote, Serikali itawachukulia hatua wafanyabiashara wa pamba wanaochezea
mizani na ninyi wananchi mnaoweka maji,mafuta na mchanga kwenye pamba muache, mkiendelea
mtachukuliwa hatua kwa sababu mnasababisha pamba yetu inashuka thamani katika
soko la Dunia”, alisema Tizeba
Kwa upande wake Mkuu wa
mkoa wa Simyu, Anthony J. Mtaka amesema Serikali imekusudia kutatua kero za
wakulima wa pamba na kuwakikishia
mazingira mazuri ya uzalishaji ikiwa ni pamoja na wakulima kupata mbegu bora,
dawa na kuhakikisha wanauza pamba kwa bei nzuri.
“Kwa muda mrefu mmekuwa
mkilima pamba na kupata mavuno yasiyoridhisha mpaka mkakata tamaa na kuanza
kulima mazao mengine, tunataka pamba kama zao kuu la biashara mkoani Simiyu
lizalishwe kwa wingi na katika ubora”, alisema Mtaka wakati alipozungumza na
wananchi wa Luguru.
Sanjari na hilo Waziri,
Tizeba ametoa wito wa wakulima kuwatumia Maafisa ugani waliopo katika maeneo
yao ili wapate ushauri wa kitaalam juu ya kanuni bora za kilimo katika zao la
pamba na mazao mengine wanayolima.
Akiwasilisha taarifa ya
Mkoa kwa Waziri wa Kilimo,Mifugo na Uvuvi, Katibu Tawala Mkoa, Bw. Jumanne A. Sagini
alisema Mkoa wa Simiyu una jumla ya Maafisa Ugani 261 waliopangwa kwenye kata
na vijiji na wasimamiwa kikamilifu katika kutimiza majukumu yao ikiwa ni pamoja
na kutoa ushauri wa kitaalam kwa
wakulima.
Waziri Tizeba pia aliwahamasisha wananchi wa
Mkoa wa Simiyu kulima kwa wingi dengu, choroko na mbaazi kwa sababu Serikali ya
India kupitia kwa Waziri Mkuu wake imesema inahitaji kati ya tani milioni sita hadi
nane za choroko, dengu na mbaazi.
Mkoa wa Simiyu
unategemea Kilimo kwa asilimia kubwa ambapo sekta ya kilimo inachangia
takribani asilimia 75 ya pato la Mkoa na zao kuu la biashara ni pamba.
0 comments:
Post a Comment