Wakulima wa pamba mkoani Simiyu wameaswa kuacha tabia
ya kuweka maji ,mchanga, na mafuta katika pamba kwa kisingizio cha kuongeza
uzito na wale watakaokaidi watachukuliwa hatua kali
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony
J. Mtaka wakati alipozungumza na Wafanyabiashara wa Pamba pamoja na
Wenyeviti na Wakurugenzi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Simiyu wakati wa
mjadala wa suala la ununuzi wa pamba katika msimu wa mwaka 2016.
Mtaka amesema wakulima wanaoweka maji , mchanga na
mafuta katika pamba wanachangia katika kushusha thamani pamba ya Tanzania
na hivyo kufanya thamani yake kuwa chini katika soko la dunia.
“Mkoa wa Simiyu unazalisha zaidi ya asilimia 60 ya
pamba ya Tanzania kwa hiyo kama pamba hii ikiharibiwa ni wazi kwamba ni pamba
ya Tanzania inaharibiwa,mwaka jana tumeuza zaidi ya kilo milioni 70; kama mkoa
unaozalisha pamba kwa wingi tumejipanga kurejesha heshima ya zao la
pamba” alisema Mtaka.
Aidha, Mtaka amekemea tabia ya wafanyabiashara
kuwaibia wakulima kwa kuchezea mizani na akaagiza atakayebainika achukuliwe
hatua kali.
“Hatutavumlia kuona wafanyabiashara wanaowaibia
wakulima kwa kufanya ujanja ujanja katika mizani tukiwabaini tutawachukulia
hatua kali, na hili limeshaanza kufanyiwa kazi, katika wilaya ya Meatu baadhi
ya wafanyabiashara wameshtakiwa , naupongeza sana uongozi wa wilaya ya Meatu” ,
alisema Mtaka.
Kwa upande wao Wakurugenzi na Wenyeviti wa Halmashauri
wameahidi kutoa ushirikiano kwa wanunuzi na kuwaomba watoe malipo ya awali
(advanced payment) ili kupunguza madeni yasiyoya lazima na kuzifanya
Halmashauri kuendesha baadhi ya shughuli muhimu kupitia ushuru wa pamba.
Wakati huo huo Mtaka amewataka mawakala wa
makampuni yanayojihusisha na ununuzi wa pamba kuwa waaminifu kwa kuacha tabia
ya kukimbia na fedha wanazopewa kwa ajili ya kununua pamba na kuwadanganya
wakulima kwa kuchezea mizani (kuchakachua) pale wanapopima pamba.
“ Mawakala wa makampuni wafanye kazi yao kwa uaminifu
kwa kuwa hiyo ni sehemu ya ajiria kwao, wasilazimishe wafanyabiashara kwenda
kutafuta mawakala Kenya, Uganda au nchi nyingine kwa sababu ya kukosa sifa ya
uaminifu.Wawe waaminifu kwa fedha wanazopewa na kupima kwa mizani ambazo
hazijachakachuliwa” alisema Mtaka.
Msimu wa ununuzi wa pamba mkoani Simiyu umeanza na
Serikali imeagiza wafanyabiashara kununua kilo moja kwa shilingi 1000 na
kuendelea.
0 comments:
Post a Comment