Viongozi wa dini wametakiwa
kuwahubiria waumini wao kuachana na
imani za kishirikina ikiwa ni pamoja na kuamini katika ramli chonganishi.
Wito huo umetolewa na Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony J. Mtaka wakati alipozungumza na washirika wa
Kanisa la Waadventista Wasabato na wakazi wa Bariadi, wakati wa ufunguzi wa mahubiri yaliyoandaliwa na Kanisa La
Wadventista Wasabato Mtaa wa Ntuzu ambayo yameanza rasmi mapema wiki hii katika
viwanja vya mpira wa mikono, karibu na
Kanisa la Waadventista Wasabato Mjini Bariadi.
Mtaka amesema baadhi ya wananchi wamekuwa wanaamini
katika ramli chonganishi hali inayosababisha baadhi yao kupoteza maisha kwa
sababu ya kukosa tiba sahihi kutokana na wao kuamini katika masuala ya uganga hata
kama magonjwa wanayoumwa yanatibika katika vituo vya kutolea huduma za Afya.
“Nawaomba muwahubirie
sana watu wa Bariadi, kuna watu hapa akiumwa malaria anaamini mpaka akachanjwe chale kwa mganga ndiyo atapona, naamin viongozi wote
hapa mtaona ni jinsi gani hawa watu wanahitaji kusaidiwa”, alisema Mtaka.
Kwa upande wake Mjumbe
wa Kamati ya Maandalizi ya Mahubiri hayo Mchungaji Peter Bahini alisema
Mahubiri hayo yamelenga kuwatoa watu katika vitendo vya uhalifu na vile vinavyoendana na imani za kishirikina
ikiwa ni pamoja na ukataji wa mapanga hasa kwa vikongwe na mauaji ya watu wenye
ulemavu wa ngozi (Albino).
Mchungaji Bahini
alisema mahubiri hayo yamesaidia zaidi ya watu 200 kubadili tabia zao kwa
kuacha maovu ambao wamekukubali kubatizwa.
Wakati huo huo Mkuu wa
Mkoa wa Simiyu amewataka waimbaji wa kwaya ya Kanisa la Waadventista
Wasabato-Kurasini, kuweka malengo ya kuwa na studio ya kurekodi nyimbo ili
warekodi nyimbo zao katika studio yao wenyewe, ambapo aliahidi kuchangia na
kuwashirikisha wadau wengine na wapenzi wa kwaya hiyo kuchangia.
“Ndugu zangu kwaya ya
SDA Kurasani ni kwaya Kongwe mno, mna zaidi ya miaka thelathini, sasa hivi
mlipaswa kuwa na studio yenu wenyewe, hampaswi kuwa miongoni mwa watu wanaoibiwa
kazi zao”, alisema Mtaka.
Aidha, Mtaka alishauri
Uongozi wa Kwaya SDA Kurasini kuanzisha vitu viwili kwanza, ikiwa ni tovuti itakayotumika kutangaza kazi
mbalimbali za kwaya na kufungua akaunti ya benki ambayo itatumika na mashabiki
hao kuichangia michango mbalimbali kwa ajili ya kuiwezesha kwaya katika masuala
mbalimbali.
Sanjari na hilo Mkuu wa
Mkoa alisema amesikitika kuona baadhi ya
shule za madhehebu ya dini zimefanya vibaya katika matokeo ya Mtihani wa Kidato
cha Sita kwa mwaka 2016, ambapo
aliwataka Viongozi wa Madhehebu ya dini kuliangalia kwa upya suala hilo, kulifanyia
kazi na kuweka mikakati ya kufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa ijayo.
Mahubiri yaliyoandaliwa
na Kanisa La Wadventista Wasabato Mtaa wa Ntuzu yaliyofunguliwa na Mhe. Mkuu wa
Mkoa yanatarajiwa kufungwa rasmi Julai 30, 2016.
Mkuu wa Mkoa Mhe. Anthony J. Mtaka (mwenye skafu ya njano kulia) akiimba pamoja na Waimbaji wa Kwaya ya kanisa la Waadventista (Wasabato) ya Kurasini Dar es Salaam mara baada ya kufungua mahubiri yaliyoandaliwa na kanisa hilo mjini Bariadi, mapema wiki hii, (wa pili kulia) Afisa Upelelezi wa Mkoa, Jonathani Shana. (Picha na Stella A. Kalinga) |
0 comments:
Post a Comment