Wednesday, August 31, 2016

SERIKALI MKOANI SIMIYU KUFANYA MABADILIKO YA WATENDAJI ELIMU NGAZI YA SHULE NA KATA

Na Stella Kalinga
 Serikali Mkoani Simiyu imekusudia kufanya mabadiliko kwa Wakuu wa Shule , Walimu Wakuu na Waratibu wa Elimu Kata katika Halmashauri zote mkoani humo, kwa kuzingatia sifa za kujiendeleza kielimu, uwezo kiutendaji  na uadilifu.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Anthony John Mtaka katika kikao alichofanya leo Ofisini kwake na Maafisa Elimu, Vifaa na Takwimu na Maafisa Elimu Vielelezo kutoka katika Halmashauri zote za Mkoa huo.
Mtaka amesema ameamua kufanya kikao na Wataalam hao ili kupata mchango wao katika suala la uwepo wa mkanganyiko wa takwimu mbalimbali za elimu hususani takwimu za wanafunzi kwa Walimu wakuu na Maafisa Elimu ambazo zimekuwa zikitofautiana kila zinapohitajika kwa nyakati tofauti.
“Ofisi hiyo hiyo ya Afisa  Elimu inatoa Idadi ya Wanafunzi wanaoletewa ruzuku ya elimu bila malipo ( kabla ya uhakiki)  nyingine, idadi ya wanafunzi baada ya uhakiki  nyingine na idadi ya wanafunzi wanaochangiwa fedha za Michezo (UMISETA) kwa Elimu ya Sekondari ni nyingine na anayeleta taarifa zote ni  huyo huyo, hatuwezi kuwa na watu ambao kila wanapotoa takwimu hatuziamini mpaka zihakikiwe”alisema Mtaka. 
Kufuatia uwepo wa mkanganyiko na mabadiliko ya mara kwa mara ya takwimu hizo katika idara ya elimu, Mkuu wa Mkoa huyo amesema kwa kuwa Elimu ni kipaumbele cha kwanza cha Mkoa; ipo haja ya kufanya mabadiliko kwa Walimu wakuu, Wakuu wa shule na Waratibu wa Elimu kata ili wapatikane watu wenye sifa watakaosimamia shule na fedha za Serikali kwa uadilifu pasipo kufanya udanganyifu katika takwimu.
Mtaka amesema Walimu Wakuu na Waratibu Elimu Kata wa Mkoa wa Simiyu wamewezeshwa ikiwa ni pamoja na kupewa mafunzo na vitendea kazi kama vishikwambi kwa ajili ya utunzaji wa takwimu, pikipiki na fedha ya mafuta hivyo wanapaswa kuwa mfano kwa kuwajibika na kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu. 
Aidha, Mtaka amesema kama taarifa za udanganyifu katika idara ya Elimu zitaendelea Wataalamu wa Vifaa, Takimu na Vielelezo katika Halmashauri watakuwa hawafanyi kazi yao sawa sawa, hivyo aliwataka Wakurugenzi wa Halmashauri kutambua nafasi ya wataalamu hao na kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ili wawe na taarifa sahihi za idara ya elimu.
Akitoa mchango wake katika kikao hicho Afisa Elimu Vifaa na Takwimu wa Wilaya ya Busega, Mathayo  Maingu amesema moja ya sababu ya uwepo wa mkanganyiko wa takwimu ni uzembe kwa baadhi ya Walimu wakuu na Wakuu wa Shule katika suala la utunzaji wa takwimu hali inayopelekea kutoa takwimu zisizo sahihi.
Kwa upande wake Afisa Elimu Vifaa na Takwimu wa Wilaya ya Itilima Ayubu Mbilinyi amesema ili kukabiliana na udanganyifu katika takwimu Watendaji katika Idara ya Elimu wanapaswa kuimarisha mfumo wa usimamizi wa nyaraka mbalimbali za usajili, mahudhurio ya wanafunzi mashuleni na kuwa na mfumo sahihi wa kutambua idadi ya wanafunzi katika nyakati zote.
Naye Afisa Elimu Vielelezo wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Charles Martini amesema hali ya udanganyifu wa takwimu imekuwa ikisababishwa na Maafisa Elimu, Vifaa na Takwimu na Maafisa Elimu Vielelezo kutowezeshwa na Waajiri wao kwenda kuhakiki takwimu mbalimbali za kielimu zinazowasilishwa.
Kwa Mujibu Mkuu Mkoa wa Simiyu mkanganyiko umeonekana katika takwimu za wanafunzi wa Elimu ya Sekondari kwa Mkoa mzima  zilizowasilishwa ambapo  idadi ya wanafunzi wanaoletewa ruzuku ya elimu bila malipo kwa mwezi Januari hadi Julai 2016 ni 41,616 ambayo ni tofauti na idadi ya wanafunzi  baada ya uhakiki Agosti 2016 ya  39,283 na wanafunzi waliochangiwa fedha za UMISETA mwaka 2016 ni ambayo ni  41,492.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony John Mtaka akizungumza Maafisa Elimu, Vifaa na Takwimu na Maafisa Elimu Vielelezo ( hawapo pichani) kutoka katika Halmashauri zote za Mkoa huo, katika kikao kilichofanyika leo Mjini Bariadi ofisini kwake



Afisa Elimu, Takwimu Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, Ayubu Mbilinyi (wa pili kulia) akichangia katika kikao cha Mkuu wa Mkoa na Maafisa Elimu, Vifaa na Takwimu na Maafisa Elimu Vielelezo kutoka katika Halmashauri zote za Mkoa huo, kilichofanyika Mjini Bariadi.



Baadhi ya Maafisa Elimu, Vifaa na Takwimu na Maafisa Elimu Vielelezo  kutoka katika Halmashauri zote za Mkoa huo wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony John Mtaka (hayupo pichani) katika kikao kilichofanyika leo Mjini Bariadi ofisini kwake.



Baadhi ya Maafisa Elimu, Vifaa na Takwimu na Maafisa Elimu Vielelezo  kutoka katika Halmashauri zote za Mkoa huo wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony John Mtaka (hayupo pichani) katika kikao kilichofanyika leo Mjini Bariadi ofisini kwake.


Afisa Elimu, Takwimu (Msingi) Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, Anthony Patrick (kushoto) akichangia katika kikao cha Mkuu wa Mkoa na Maafisa Elimu, Vifaa na Takwimu na Maafisa Elimu Vielelezo kutoka katika Halmashauri zote za Mkoa huo, kilichofanyika Mjini Bariadi, Ofisini kwa Mkuu wa Mkoa.





Afisa Elimu, Takwimu Sekondari) Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Elias Mbiji (aliyesimama) akichangia katika kikao cha Mkuu wa Mkoa na Maafisa Elimu, Vifaa na Takwimu na Maafisa Elimu Vielelezo kutoka katika Halmashauri zote za Mkoa huo, kilichofanyika Mjini Bariadi, Ofisini kwa Mkuu wa Mkoa.






Afisa Elimu, Takwimu (Sekondari) Halmashauri ya Mji Bariadi , Revocatus Ladislaus akichangia katika kikao cha Mkuu wa Mkoa na Maafisa Elimu, Vifaa na Takwimu na Maafisa Elimu Vielelezo kutoka katika Halmashauri zote za Mkoa huo, kilichofanyika Mjini Bariadi, Ofisini kwa Mkuu wa Mkoa.





Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!