Na
Stella Kalinga
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Anthony Mtaka ameishauri Serikali kufuta utaratibu wa kutoa fedha kwa kaya
maskini zinazotolewa kupitia Mpango wa Kunusuru kaya maskini TASAF III na
badala yake uandaliwe utaratibu wa kuwawezesha wananchi kupata ruzuku ya mbegu
na pembejeo nyingine za kilimo.
Mtaka ametoa ushauri
huo wakati wa zoezi la uhawilishaji wa fedha katika kijiji cha Itinje wilayani
Meatu, ambapo jumla ya shilingi 2,800,000 zilitolewa kwa kaya 77 zinazonufaika
na mpango huo.
Mtaka amesema Serikali
inatumia zaidi ya Bilioni 400 kwa ajili ya Mpango wa TASAF nchi nzima na wakati
huo baadhi ya malengo ya TASAF III yameanza kutekelezwa na Serikali ikiwa ni
pamoja na utoaji wa elimu bila malipo, utoaji wa huduma za afya bure kwa wazee
na Mfuko wa Huduma ya Afya kwa Jamii (CHF) hivyo, malengo ya TASAF yamepungua.
“Hizi shilingi bilioni
1.7 zilizotolewa kwa mwaka mmoja kwa Meatu tu, zingetolewa kama ruzuku kwa
wakulima wa pamba, mngeweza kupata mbegu bure, dawa bure mkalima pamba na mkapata
fedha nyingi kuliko nikiwagawia hizi elfu thelathini, elfu hamsini na watu
wengine humo katikati wanaiba hizo fedha, Nitakuwa kiongozi wa kwanza tena
kijana kupendekeza huko mbele Serikali ifute mpango huu wa TASAF”, alisema
Mtaka.
Mtaka amesema wananchi
wanapaswa kusaidiwa njia sahihi za kutafuta
fedha kwa ajili ya kujikwamua katika umaskini ikiwa ni pamoja na
kujishughulisha na kilimo, ufugaji, ujasiriamali na kupewa fedha ambazo
wanufaika walio wengi hawazitumii kwa
malengo yaliyokusudiwa.
Aidha, Mtaka amesema
watoto watimize wajibu wa kuwatunza wazazi wao kwa kuwa baadhi ya wanufaika wa
mpango wa TASAF III ni wazee waliotelekezwa na watoto wao, hiyo wazee
wawakumbushe watoto wao ili wawasaidie kuwatimizia mahitaji muhimu.
Pamoja na ushauri wake
kwa Serikali Mkuu huyo wa mkoa amewataka wanufaika wa mpango huo kujiandaa na kujipanga namna watavyojipatia mahitaji
yao muhimu endapo mpango huu utasitishwa na akawataka wajikite katika ufugaji
na kilimo cha Pamba na alizeti.
“Nawapa hizi pesa leo
ila nawashauri kila mmoja ajipange, ikitokea TASAF inafutwa leo ajue atapataje
mahitaji yake ya kila siku. Natamani muwe watu mnaopenda kupata nyavu kwa ajili
ya kuvua samaki badala ya kupenda kupewa samaki, hizi pesa zitawalemaza”
Nae Mkuu wa
Wilaya ya Meatu Dkt. Joseph Chilongani amesema uhalisia wa utekelezaji wa
mpango huo wa kunusuru kaya maskini haujakaa vizuri kwani haoni kama
unamuondolea mwananchi umaskini.
Dk Chilongani
ameeleza kuwa ni vema fedha hizo
zitafutiwe utaratibu mzuri wa kuwasaidia wananchi kupitia vikundi
vitakavyojishughulisha na shughuli za kuwaongezea kipato kuliko unavyotekelezwa
kwa sasa.
Mpango
wa kunusuru Kaya Maskini TASAF III Wilayani Meatu unatekelezwa katika jumla ya kaya
5727 zilizoandikishwa katika vijiji 68 kati ya 106 vilivyopo wilayani humo,
ambao kufikia mwezi Agosti 2016, Halmashauri ya Wilaya ya Meatu imeshapokea
jumla ya shilingi 1, 793,421,272.73
0 comments:
Post a Comment