Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka ametoa ufafanuzi wa agizo la kufanya
mabadiliko ya Walimu wakuu, Wakuu wa Shule na Waratibu Elimu Kata mkoani humo, ambalo Serikali ya Mkoa ililitoa tarehe 17
Agosti ,2016 katika kikao ambacho alipokea Vishikwambi (tablets) 637 kutoka EQUIP Tanzania
(Mpango wa Kuinua Ubora wa Elimu Nchini) kwa ajili ya Walimu wakuu na Waratibu wa Elimu
Kata
Mkuu huyo wa
Mkoa ametoa ufafanuzi huo kufuatia kuwepo kwa taarifa za upotoshaji wa agizo
hilo kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.,
kuwa Mkuu wa Mkoa ametangaza kuwavua madaraka Walimu wakuu, Wakuu wa Shule na
Waratibu Elimu Kata wote wa Mkoa huo; hali iliyopelekea baadhi ya Walimu wakuu
na Waratibu kukosa ari ya kufanya kazi, kwa
kigezo cha kusubiri kuvuliwa madaraka.
Mtaka amesema Mkoa
ulipokea taarifa za takwimu za wanafunzi hewa, vyumba vya madarasa, idadi ya
walimu na idadi ya madawati, baada ya kupokea taarifa hizo ulionekana utofauti
mkubwa wa takwimu hizo ndipo Serikali mkoani humo, ikaahidi kupitia mapungufu
ya udanganyifu wa takwimu hizo kwa kila shule na kuchukua hatua ikiwa ni pamoja
na kuwawajibisha Walimu wakuu na Wakuu wa Shule waliodanganya idadi ya
wanafunzi.
Aidha, Mtaka amesema
Mkoa wa Simiyu umepata bahati ya kuwa na Mradi wa EQUIP Tanzania ambao umewawezesha
waratibu kupata pikipiki na posho, walimu wakuu wamepewa vishikwambi kwaa jili
ya utunzaji wa takwimu, hivyo Serikali inao wajibu wa kuangalia mahitaji ya
Mkoa katika elimu ambapo alielekeza yafanyike mabadiliko ya Walimu wakuu
Msingi, Sekondari na Waratibu wa mkoa mzima.
“Nililisema
mwanzo na leo nalirudia tutafanya mabadiliko makubwa kwa Wakuu wa Shule za
Msingi, Sekondari na Waratibu Elimu kata kwa kujiridhisha na maendeleo ya shule
zetu, idadi ya walimu waliopo,idadi ya wanafunzi, kiwango cha ufaulu wa
wanafunzi na mazingira ya shule ; lakini tutatoa upendeleo kwa shule 10 bora
katika kila wilaya kwa Mitihani ya Kitaifa ya Darasa la IV, VII Kidato cha II
na IV , hiki ni kipimo kimojawapo cha walimu wa kuendelea nao. Nasisitiza hakuna
mtu atakayeonewa wala kufedheheshwa”, alisema Mtaka.
Mtaka amesema azma ya
Serikali ni kuibua vipaji vipya vya viongozi wa Elimu katika ngazi ya Wilaya
ambapo alisema ameshaagiza Maafisa Elimu wa Wilaya kuwasilisha taarifa ya
walimu waliojiendeleza katika ngazi shahada ya kwanza na shahada ya uzamili ili
watakaokuwa na sifa waweze kuteuliwa katika nafasi za Walimu wakuu, Wakuu wa
Shule na Waratibu Elimu Kata ambao watafanyiwa upekuzi (vetting) na Vyombo vya
Ulinzi na Usalama.
Sanjari na hilo ,
Mkuu huyo wa Mkoa amesema Walimu wakuu na Wakuu wa shule wa zamani ni tofauti
na wale wa sasa, kwa kuwa sasa hivi
wamekuwa maafisa masuuli wa shule zao ambapo wanapokea fedha za Elimu bila
malipo kupitia akaunti za shule zao, hivyo ni lazima wapatikane watu waadilifu,
wenye sifa na uwezo wa kuongoza shule na kusimamia fedha za Serikali.
Akichangia
katika kikao hicho Afisa Elimu (Msingi) Wilaya
ya Meatu, George Lowasa ameshauri Uchambuzi wa watu watakaoteuliwa ufanyike katika
umakini mkubwa ili wapatikane watendaji wazuri na kuhusu utoaji wa takwimu sahihi
alishauri kuwe na utaratibu wa kuziboresha kila (robo) baada ya miezi mitatu
ili kuwa na takwimu sahihi pale zinapohitajika.
Kwa upande wake
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini amesema Uteuzi huo utazingatia
sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya uteuzi ambapo hakuna mtu atakayeonewa au
atakayependelewa.
Wakati huo huo Mkuu
wa Mkoa amesema atawachukulia hatua Maafisa wale wanaolalamikiwa na walimu kwa
kuwatolea lugha mbaya kila wanapotoa
huduma kwa walimu hao katika Halmashauri za Mkoa huo.
Naye Katibu wa
CWT Mkoa wa Simiyu, Said Mselema akitoa mcango wake katika kikao hicho ameshauri baada ya mabadiliko ya wakuu wa shule na
Waratibu wa Elimu Kata kufanyika wale ambao wataonekana hawana sifa za
kuendelea kushika nafasi hizo waondolewe kwa staha kwa kufauata taratibu, ambapo aliomba Serikali
ngazi ya Wilaya na Mkoa ikishirikishe chama hicho katika masuala yote muhimu ya
kuendeleza sekta ya Elimu, kwa kuwa wanamsaidia mwajiri katika usimamizi wa
utendaji kwa walimu.
Kikao hicho cha wadau kilichofanyika mjini Bariadi na kimewahusisha Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa, Maafisa Elimu kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Simiyu pamoja na Wenyeviti na Makatibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) ngazi ya Mkoa na Wilaya.
Kikao hicho cha wadau kilichofanyika mjini Bariadi na kimewahusisha Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa, Maafisa Elimu kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Simiyu pamoja na Wenyeviti na Makatibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) ngazi ya Mkoa na Wilaya.
0 comments:
Post a Comment