Na Stella Kalinga
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi,
Mhe. Festo Kiswaga ametoa wito kwa viongozi wa madhehebu ya Dini kutumia nafasi
zao katika kuwahimiza watu wafanye kazi kwa bidii ili kuendeana na Kauli Mbiu ya
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ya HAPA
KAZI TU.
Kiswaga ametoa wito huo
katika ufunguzi wa Mkutano wa Neno la Mungu mjini Bariadi, ulioandaliwa na
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (K.K.K.T) Dayosisi ya Kusini Mashariki ya
Ziwa Victoria kwa kushirikiana na Huduma ya New Life in Christ ya Jijini Dar es
Salaam.
Akitoa salamu za Serikali
kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka, Kiswaga amesema
Viongozi wa dini wana nafasi za kubwa kuwahamasisha waumini kufanya kazi kwa
bidii ili kujiletea maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
“Mhe. Rais wetu John
Pombe Magufuli ameshatoa maelekezo kuwa watu wote wafanye kazi, tena wafanye kazi
kwa nguvu zao zote, katika imani hiyo hiyo Mkuu wa Mkoa wetu anasema ana imani
kubwa kuwa viongozi wa dini wataendelea kuwahimiza waumini wao wafanye kazi.
Ombi lake kwenu Muendelee kumuombea Rais wetu ili aweze kuliongoza Taifa hili
na kutekeleza majukumu yake kwa Amani na Utulivu”
Kiswaga amesema pamoja
na kuwahimiza wananchi kufanya kazi Serikali inatambua mchango mkubwa wa
Viongozi wa dini katika kupunguza Imani potofu, mauaji ya vikongwe, mauaji ya
albino na kutatua migogro ndani ya familia na jamii kwa ujumla, hivyo huchangia
kupunguza vitendo viovu katika jamii.
Wakati huo huo Mkuu
huyo wa Wilaya amewatahadharisha wananchi na wakazi wa Bariadi kutojiingiza
katika masuala ya uvunjifu wa amani ikiwa ni pamoja na kutojichukulia sheria
mikononi kwa kuwaua vikongwe, kujiingiza katika maandamano yasiyo na kibali cha
Serikali na akawataka kutii na kuheshimu sheria za nchi.
Aidha, Kiswaga
amewataka wakazi wa Bariadi na Mkoa wa Simiyu kwa ujumla kufanya usafi katika
maeneo yao ya kazi, biashara na makazi ili kuuweka Mkoa wa Simiyu katika hali
ya Usafi.
Kwa upande wake Askofu wa K.K.K.T Dayosisi ya Kusini Mashariki ya
Ziwa Victoria, Dkt. Emmanuel Makala amesema Kanisa linaunga mkono Juhudi za
Serikali za kuwafanya Watanzania waishi kwa amani kwa kuwapelekea injili, ili waendelee
kuwa na uhuru wa kuabudu.
Mkutano huo wenye kauli
Mbiu ya SIMIYU KWA YESU ulifunguliwa rasmi jana katika Mji wa Bariadi na
utaendelea pia katika vituo vingine 27 katika wilaya zote tano za Mkoa wa
Simiyu hadi tarehe 21/08/2016.
Mwinjilisti Teddy Steven akihubiri katika Mkutano wa Injili Mjini Bariadi( (Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu) |
0 comments:
Post a Comment