Thursday, August 18, 2016

WANANCHI MKOANI SIMIYU WAHIMIZWA KUTUNZA MIRADI YA MAJI



Na Stella Kalinga
Serikali imewataka wananchi kutunza miradi ya maji na miundombinu ya maji kwa ujumla ili waweze kupata huduma endelevu ya maji katika maeneo yao.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe alipotembelea Kisima cha Maji kilichochimbwa kwa Ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Misri, Kilichopo Kijiji cha Nkololo Wilayani Bariadi wakati wa ziara yake Mkoani Simiyu.
Mhe. Kamwelwe amesema Serikali ya Misri kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania  imechimba takribani visima 130 nchi nzima, hivyo wananchi wanapaswa kuunga mkono na kutambua jitihada za Serikali katika kupeleka maji mahali ambapo hapakuwa na huduma za maji na kuwaondolea adha ya kufuata maji mwendo mrefu.
Mhe. Kamwelwe amewataka wananchi wa Nkololo kwa kupitia Jumuiya ya Watumia maji kuhakikisha kuweka utaratibu wa kuchangia huduma ya maji inayotolewa na Kisima hicho ili fedha inayopatikana iwasaidie katika kuboresha mradi huo pale wanapokabiliana na changamoto ndogo ndogo za gharama za uendeshaji wa mradi.
Mwenyekiti wa kijiji cha Nkololo, Bahame Maduhu  amesema Serikali ya kijiji na Wananchi kwa ujumla wamejipanga katika kuhakikisha mradi huo unalindwa na wameshatafuta walinzi ambao wanalinda usiku na mchana, ambapo wamekubaliana kuchangia fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya jenereta ili kulikinga na jua na mvua na alimweleza Mhe. Naibu Waziri kuwa wameshachangia shilingi 1,000,000/=.
“Mradi huu umekuwa msaada sana kwetu, sasa hivi tunapata maji ya uhakika karibu tofauti na zamani wakina mama walikuwa wanafuata maji umbali mrefu halafu maji yenyewe yalikuwa ya chumvi. Maji ya Kisima hiki cha Wamisri hayana chumvi sasa hivi watoto wetu hawataharibika meno tena.”, alisema Maduhu.

Wakati huo huo Mhe. Naibu Waziri amesema Serikali ina mpango wa kujenga mabwawa, kuvuna maji ya mvua na kutengeneza Skimu za Umwagiliaji  ili wananchi walime kilimo cha uhakika na kuwa na uhakika wa kupata mazao ya kutosha badala ya kutegemea maji ya mvua.
“Tunayo maeneo ya kutosha katika nchi hii kwa jili ya kilimo, tuna hekta Milioni 29.4 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji hakuna sababu kabisa katika nchi yetu kuwa na njaa” alisema Kamwelwe.
Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya Mkoa ya Miradi ya Maji na Umwagiliaji, iliyowasilishwa na  Katibu Tawalaa Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini, Mhe.Kamwelwe amesema Wizara ya Maji naUmwagiliaji imetenga jumla ya shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kulipa fidia maeneo yanayofaa kilimo cha umwaagiliaji hususani mabonde ya umwagiliaji, ambayo yakishafidiwa yatalindwa ili yasivamiwe.
Kamwelwe amesema Wizara inaendelea na zoezi la kuanisha maeneo hayo ili kuyatambua na kuyawekea mipaka ambapo alieleza kuwa zoezi hilo litakapokamilika Wizara itazitaarifa Sekretarieti za Mikoa zisaidie katika ulinzi wa maeneo hayo.
Wizara pia imejipanga kuimarisha Tume ya Umwagiliaji ambayo itasaidia usimamizi wa Skimu za umwagiliaji, hadi sasa inahitaji zaidi ya Watalaam 400 kwa nchi nzima.
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji akiwa katika wilaya ya Busega na Bariadi ametembelea miradi mbalimbali ya Maji na Umwagiliaji ikiwemo ya Bwawa la Lutubiga(Busega), Visima vilivyochimbwa na Serikali ya Misri kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania, Chanzo cha Maji na Matanki ya kuhifadhia maji ya Mamlaka ya Maji ya Mji wa Bariadi (BARUWASA.



Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhe. Isack Kamwelwe(kushoto)akizungumza na wakazi wa kijiji cha Nkololo wilayani Bariadi,(baadhi hawapo pichani)  alipotembelea kuona Mradi wa Maji ya Kisima kilichochimbwa na Serikali ya Misri kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kijijini hapo.
Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji ya mji wa Bariadi, Stephen A.Stephen (wa kwanza kulia) akimuonesha Matanki ya kuhifadhia maji ya mamlaka hiyo Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhe. Isack Kamwelwe (wa pili kulia), wakati wa Ziara yake Mkoani Simiyu. .(Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu)
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini (kushoto)akiwasilisha taarifa ya Mkoa juu ya Miradi ya Maji na Umwagiliaji kwa Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhe. Isack Kamwelwe (hayupo pichani), wakati wa Ziara yake Mkoani Simiyu. (Kulia) Katibu Tawala Msaidizi wa Huduma za Maji katika Sekretarieti ya Mkoa wa Simiyu, Mhandisi.Hatari Kapufi.(Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu)

Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Mohammed Said (kushoto) akitoa maelezo juu ya ujenzi wa Tuta la Bwawa la Lutubiga (haliko pichani) kwa Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhe. Isack Kamwelwe(wa tatu kushoto), wakati wa Ziara yake wilayani humo.(Kulia) Katibu Tawala Msaidizi wa Huduma za Maji katika Sekretarieti ya Mkoa wa Simiyu, Mhandisi.Hatari Kapufi.(Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu)
Mhandisi wa Maji wa Sekretarieti ya Mkoa wa Simiyu, Mahobe  Mahuyemba(kulia) akitoa maelezo juu ya kisima kinachotoa Maji kwa Wananchi wa Bariadi Mjini cha Mamlaka ya Maji ya Mji wa Bariadi, kilichopo mjini Bariadi kwa Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhe. Isack Kamwelwe(wa tatu kushoto), wakati wa Ziara yake Mkoani Simiyu.(Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoaw Simiyu) 





0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!