Na
Stella Kalinga (Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu)
Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka amewataka
viongozi wa kata na vijiji kuwabaini wanufaika wa Mpango wa kunusuru kaya TASAF
III(PSSN) wanaojihusisha na ulevi na kuwaondoa katika orodha ya wanufaika wa
mpango huo.
Mtaka ametoa agizo hilo
wakati alipozungumza na wananchi wa kijiji cha Mwamgoba wilayani Busega katika
zoezi la uhawilishaji fedha za TASAF III PSSN, ambapo jumla ya shilingi
2,976,000 zimegawiwa kwa wanufaika 82 kijijini hapo.
Mtaka amesema lengo la
mpango wa TASAF III ni kuwatoa watanzania katika hali ya umaskini kwa kuwapa
ruzuku itakayowasadia kupata huduma muhimu ikiwa ni pamoja huduma za afya,
kuwasaidia watoto wao waweze kwenda shule lakini baadhi ya wanufaika wamekuwa
wakitumia fedha hizo kulewa badala ya kuanzisha miradi midogo midogo kama
ufugaji wa kuku, mbuzi na kondoo pamoja na kilimo ili miradi hiyo iwasaidie
kuwaongezea kipato.
“Hatuwezi kuleta fedha tukifikiri zitawasaidia kujikwamua katika
Umaskini lakini mnashinda baa na vilabuni kulewa , wengine mnaongeza wake,
tukiwabaini mtaondolewa kwenye huu mpango” , alisema Mtaka.
Mtaka amewataka
wanufaika hao kujishugulisha na kilimo na ufugaji na kuondokana na dhana ya kuwa watakuwa wanufaika wa mpango huo siku
zote, ambapo alieleza azma ya Serikali
ya awamu ya tano ya kuwatoa wananchi katika umaskini na kuwaondolea changamoto
mbalimbali kama kutoa elimu ya bila malipo na kuanzisha Mfuko wa Huduma ya Afya
Watanzania wasio na uwezo waweze kupata matibabu kwa gharama nafuu na akatoa wito kwa wanufaika hao kujiunga na
Mfuko wa Huduma ya Afya ya Jamii (CHF)ambao utawasaidia wao wenyewe pamoja na
wategemezi wao kupata huduma za Afya katika Vituo vya kutolea huduma za Afya.
Aidha, ametoa wito kwa
wazazi kuwakumbusha watoto wao wajibu wa kuwatunza kwa sababu kumekuwa na
baadhi ya wazee ambao wametambuliwa kuwa ni maskini, wakati wana watoto wenye
nguvu na uwezo wa kuwasaidia lakini hawatimizi wajibu wao kuwatunza kwa kuwapa
mahitaji muhimu.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa
fedha hizo Bibi. Christina Robert ambaye ni mnufaika wa mpango wa TASAF amesema
mpango huo umemsaidia kuondokana na kuishi katika nyumba ya nyasi na matope na
kumuwezesha kujenga nyumba ya matofali na bati.
“Naishukuru TASAF maana
imenisaidia sana, ruzuku niliyopewa mara ya kwanza ilinisaidia kutibiwa nilipofanyiwa
upasuaji, mara ya pili nilitumia tena kwenye matibabu, mara ya tatu nilinunua
kuku na bata, mara ya nne nikanunua bati
nikajenga nyumba ya vyumba viwili”, alisema Christina.
Pamoja na kusisitiza
juu ya matumizi sahihi ya fedha za ruzuku za TASAF Mtaka amewataka wananchi wa
Busega na Mkoa wa Simiyu kwa ujumla kuongeza juhudi katika kilimo cha mazao ya
mikunde kwa kuwa tayari Serikali ya India imekubali kununua zaidi ya tani
milioni sita ya choroko, dengu na mbaazi kutoka Tanzania, hivyo wakati utekelezaji wa makubaliano hayo
utakapoanza wananchi walime kwa wingi mazao hayo kwa kuwa kutakuwa na soko la
uhakika.
Jumla ya kaya 4260 zilibainishwa
katika vijiji 41 vya wilaya ya Busega ambapo kaya 53 ziliondolewa katika mpango
wa TASAF III PSSN baada ya uhakiki na kubaini kuwa hazikukidhi vigezo.
|
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu , Mhe.
Anthon Mtaka akimkabidhi fedha Bw. Methesela Mrobi wakati wa zoezi la
uhawilishaji fedha za ruzuku kwa wanufaika wa Mpango wa kunusuru kaya maskini
TASAF III ,katika kijiji cha Mwamgoba, Wilaya ya Busega Mkoani humoi. (Picha na
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.)
|
|
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu , Mhe.
Anthony Mtaka akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Mwamgoba wilayani Busega
(hawapo pichani) kabla ya zoezi la uhawilishaji fedha za ruzuku kwa wanufaika
wa Mpango wa kunusuru kaya maskini TASAF III kijijini hapo, kutoka kulia Katibu
Tawala Wilaya Busega , Sebastiani Masanja, Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Tano
Mwera na Katibu Tawala Mkoa, Jumanne Sagini (Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu)
|
|
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bw.
Jumanne Sagini akifafanua jambo kwa wakazi wa Kijiji cha Mwamgoba wilayani
Busega (hawapo pichani) kabla ya zoezi la uhawilishaji fedha za ruzuku kwa
wanufaika wa Mpango wa kunusuru kaya maskini TASAF III kijijini hapo, Wilayani
Busega Mkoani humo. (Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu)
|
|
Baadhi ya wanufaika wa Mpango wa
kunusuru kaya maskini TASAF III katika kijiji cha Mwamgoba Wilayani Busega,
wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (hayupo pichani),
alipozungumza nao kabla ya zoezi la uhawilishaji wa fedha za ruzuku kwa ajili
ya mpango huo. (Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu)
|
|
Bw. Methesela Mrobi akimuonesha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu na
viongozi wengine wa Mkoa na Wilaya(hawapo pichani) Bwawa dogo alilochimba kwa
kutumia fedha za ruzuku za Mpango wa kunusuru kaya maskini TASAF III, ambalo
analitumia kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.(Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
wa Simiyu)
|
|
Mkuu wa Wilaya ya Busega , Mhe.
Tano Mwera (katikati) na Katibu Tawala Wilaya ya Busega, Bw. Sebastian Masanja
(kulia) wakizungumza jambo kabla ya zoezi la uhawilishaji fedha za ruzuku kwa
wanufaika wa Mpango wa kunusuru kaya maskini TASAF III kijiji cha Mwamgoba,
Wilayani Busega (kushoto) Katibu Tawala
Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini.(Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu)
|
|
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu , Mhe.
Anthony Mtaka akiwa na Viongozi wengine wa Mkoa na Wilaya ya Busega wakitoka kukagua shamba la miwa la Bw. Methesela Mrobi ambalo analima kwa kumwagilia maji kutoka katika bwawa dogo alilochimba kwa kutumia fedha za ruzuku ya Mpango wa kunusuru kaya maskini TASAF awamu ya III ,katika kijiji cha Mwamgoba, Wilaya ya Busega Mkoani humo. (Picha na
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.)
|
|
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu , Mhe.
Anthony Mtaka akisaini kitabu cha wageni katika Shule ya Msingi Mwamgoba alipotembelea shule hiyo kabla ya kufanya zoezi la
uhawilishaji fedha za ruzuku kwa wanufaika wa Mpango wa kunusuru kaya maskini
TASAF III ,katika kijiji cha Mwamgoba, Wilaya ya Busega Mkoani humo. (Picha na
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.)\
|
|
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu , Bw. Jumanne Sagini akisaini kitabu cha wageni katika Shule ya Msingi Mwamgoba alipotembelea shule hiyo kabla ya kufanya zoezi la
uhawilishaji fedha za ruzuku kwa wanufaika wa Mpango wa kunusuru kaya maskini
TASAF III ,katika kijiji cha Mwamgoba, Wilaya ya Busega Mkoani humo. (Picha na
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.) | |
|
Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Mipango na Uratibu, Bw. Donatus Weginah(kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (kulia) wakimsikiliza mwalimu Mkuu wa Shule ya Mwamgoba (hayupo pichani) wakati Mkuu huyo wa Mkoa alipotembelea shule hiyo kabla ya kufanya zoezi la
uhawilishaji fedha za ruzuku kwa wanufaika wa Mpango wa kunusuru kaya maskini
TASAF III ,katika kijiji cha Mwamgoba, Wilaya ya Busega Mkoani humo. (Picha na
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.) |
0 comments:
Post a Comment