Na
Stella Kalinga
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi,Teknolojia
na Mafunzo ya Ufundi Mhandisi Stella Manyanya amemsimamisha kazi aliyekuwa Mkuu
wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Bunamhala kilichopo Halmashauri ya Mji wa
Bariadi Mkoani Simiyu Bw. Ramadhani Said, kutokana na utendaji usioridhisha na
kumteua Bi. Levina Mrema kushikilia wadhifa huo kwa muda, wakati taratibu
zingine zikiendelea.
Mhandisi Manyanya
amechukua uamuzi huo alipopokea taarifa baada ya kutembelea chuo hicho alipokuwa
katika ziara yake Mkoani Simiyu, ambapo amesema hajaridhishwa na utendaji kazi katika chuo hicho kikongwe kilichofunguliwa
rasmi mwaka 1978 ambacho kwa sasa kina
watumishi 10 wanaolipwa mshahara na Serikali kwa kuwahudumia wanafunzi 8 tu.
“Nimepata taarifa kuwa kuna wakati chuo hiki
hakina wanafunzi kabisa lakini watumishi mpo na mnaendelea kulipwa mshahara na
Serikali, kwa nini vyuo vingine vina wanafunzi hiki cha kwenu hakina wanafunzi?Wewe kama Mkuu wa
Chuo umefanya jitihada gani kuhakikisha chuo kinakuwa na wanafunzi wa kutosha?
Maana chuo siyo majengo tu”, alisema Manyanya.
Manyanya amesema
amemteua Levina Mrema kuwa Kaimu Mkuu wa Chuo hiki, kwa kipindi cha matazamio
kwa miezi sita ili atumie uzoefu wake kuja na mawazo mapya akishirikiana na
uongozi wa Mkoa na wilaya kukifanya chuo kinarudi katika hadhi yake.
Akitoa taarifa kwa
Naibu Waziri, aliyekuwa Mkuu wa Chuo hicho Ramadhani Said amesema amefanya
jitihada za kukitangaza chuo lakini wanafunzi wanapofika chuoni wanaondoka
baada ya kukutana na changamoto ya miundombinu chakavu ya majengo,ukosefu wa
vifaa vya kujifunzia na kufundishia na ukosefu wa umeme.
Katika kukabiliana na
changamoto ya miundombinu ya chuo, Naibu Waziri amemuagiza Mkurugenzi wa VETA Taifa
kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa bweni , vitanda na kuweka umeme katika
chuo hicho, ambapo aliahidi kutoa shilingi milioni tano za kuanzia kufanya
ukarabati ili wanafunzi wasome katika mazingira mazuri.
Mhandisi Manyanya
amemtaka Mkuu wa Chuo aliyeteuliwa kuweka mikakati ya kukitangaza chuo ili
kitambulike ndani ya Mkoa na nje ya mkoa wa Simiyu ili vijana wapate ujuzi
utakaowasaidia kujikwamua kutoka katika umaskini.
Pamoja na jitihada
alizozionesha Naibu Waziri, Bi. Mrema ameomba Serikali itenge fedha za kutosha katika bajeti ya mwaka wa fedha
ujao ili kufanya ukarabati wa majengo yote, kununua vifaa vya kujifunzia na
kufundishia, kutengeneza barabara ili kuweka mazingira yatakayowashawishi
wanafunzi kujiunga katika chuo hicho.
Kwa upande wake Mkuu wa
Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka ameahidi kusimamia na kuhakikisha chuo hicho
kinakuwa na manufaa kwa Mkoa wa Simiyu na Taifa kwa ujumla ili kiwasaidie
Watanzania hususani vijana kupata elimu na ujuzi wa masuala mbalimbali ukiwemo
ujasiriamali, ushonaji, ufundi uashi, ufundi seremara na mafunzo mengine.
Kabla ya kuteuliwa kuwa
Kaimu Mkuu wa Chuo, Bi. Levina Mrema alikuwa Mhasibu katika chuo hicho.
0 comments:
Post a Comment