Na Stella Kalinga
Rais wa Shirikisho la
Riadha Tanzania (RT) ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka
ametoa wito kwa Watanzania kujitokeza katika kumpokea Mwanariadha, Alphonce
Simbu ambaye ameshika nafasi ya tano katika mashindano ya Olimpiki ya Marathoni
yaliyofanyika Jijini Rio de Janeiro nchini
Brazili.
Mtaka amesema hayo
wakati wa mahojiano maalum na Waandishi wa Habari Ofisini kwake juu ya namna
Shirikisho hilo lilivyopokea nafasi ya Mwanariadha huyo katika mashindano ya
Olimpiki ya Marathoni mwaka 2016.
Mtaka amesema
Mwanariadha huyo na wenzake wanatarajiwa kurejea nchini siku ya Alhamisi mchana
tarehe 25 Agosti,2016 katika Uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
Dar es Salaam, ambapo taratibu za mapokezi zinaendelea kufanywa na Kamati Tendaji
ya Shirikisho na akawaomba viongozi katika wizara yenye dhamana na michezo
kuona namna ya kushiriki katika mapokezi ya mwanariadha huyo.
“Hatujapata medali
lakini nafurahi kuona mapokeo ya watu kuona kiu ya kuwa tunafanya vizuri , nafikiri mapokeo
hayo yaendelee. Kitendo cha Alphonce Simbu kuwa miongoni mwa wanariadha bora
watano si jambo dogo, tangu mwaka 1964 Tanzania hatujawahi kupata ushindi
katika riadha, Nawaomba Watanzania tumuunge mkono Alphonce Simbu kwa kuwa
ameliletea heshima Taifa”alisema Mtaka.
Mtaka amesema ushindi
wa Alphonce umetoa mwanga kuwa endapo Serikali itawekeza katika riadha Watanzania
wataweza kufanya vizuri katika mashindano ya Jumuiya ya Madola na Mashindano mengine ya Kimataifa katika siku
zijazo, kwa kuwa kabla ya mashindano ya Olimpiki Shirikisho la riadha
liliwekeza kwa wanariadha ambapo walikaa kambini kwa takribani miezi nane na
shirikisho lilikuwa likiwalipa shilingi 600,000/= kwa kila mmoja.
Aidha, Mtaka ameshukuru
baadhi ya Mashirika ambayo yamejitoa kumsaidia Mwanariadha huyo pamoja na maendeleo
ya Riadha na Shirikisho la Riadha kwa ujumla, yakiwemo TTCL, DSTV na Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania(TCRA) na akasema Viongozi wa Shirikisho la riadha wamedhamiria
kuhakikisha Riadha inailetea heshima Taifa na inawatoa Watanzania Kimasomaso
katika medani ya michezo.
“Mwanariadha huyu
ameitangaza nchi, Olimpiki ina watazamaji wengi duniani ambao jana wametazama yale
mashindano, yule mtangazaji alipomtaja Alphonce Sumbi kuwa namba tano, alisema
anatoka katika nchi ambayo Rais wake Kauli mbiu yake ni HAPA KAZI TU. Ni maneno
ya Kiswahili lakini yametangazwa na Mtangazaji kutoka katika Shirika la
Utangazaji la Kimataifa, ni faraja kubwa hii ni brand kwa nchi; Alphonce
ameibrand nchi na Kauli mbiu ya Mhe. Rais”, alisema Mtaka.
Kwa upande wake Katibu
wa Chama cha Riadha Mkoa wa Simiyu na Katibu wa Vyama vya Riadha Kanda ya Ziwa,
Yohana Msese amempongeza Mwanariadha Alphonce na kuiomba Serikali kutilia mkazo
suala la michezo mashuleni ili kuweza kuwatambua watoto wenye vipaji katika
michezo mbalimbali na kuwawezesha katika kuviendeleza vipaji hivyo ili
kuwajengea mazingira mazuri ya kuwa wachezaji wazuri kwa siku za usoni.
Alphonce Felix Simbu
ameshika nafasi ya tano katika mashindano ya Olimpiki ya Mbio za Marathoni za
Kilomita 42
Mwanariadha Mtanzania, Alphonce Sembu aliyeshika nafasi ya tano katika mbio za kilomita 42, kwenye Mashindano ya Olimpiki ya Marathoni yaliyofanyika Jijini Rio de Janeiro nchini Brazili. |
0 comments:
Post a Comment