Na
Stella Kalinga
Zaidi ya Vijiji 63 vya
wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu vinatarajia kupata umeme kupitia Wakala wa
Umeme Vijijini (REA) Awamu ya III inayoanza mwishoni mwa Mwezi Septemba, 2016.
Hayo yamesemwa na Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Mhe.
Dkt. Merdard Kalemani alipozungumza na wananchi wa maeneo
tofauti ya wilaya ya Itilima wakati wa Ziara yake ya kukagua miradi ya Wakala wa
Umeme Vijijini (REA) Awamu ya II Mkoani Simiyu.
Pamoja na kupeleka huduma ya umeme kwa wananchi kutoka
katika vijiji hivyo 63 Dkt. Kalemani amesema Serikali imedhamiria kupeleka
huduma ya umeme katika Taasisi za Serikali zikiwemo shule za Msingi na
Sekondari Ofisi za Serikali, Vituo Vya
Afya na Zahanati na katika maeneo ya miradi ya maji.
Dkt. Kalemani ameelekeza Serikali za vijiji kwa
kushirikana na Shirika la Ugavi wa Umeme (TANESCO) kuainisha wananchi
wanaohitaji huduma ya umeme ili mradi utakapoanza kutekelezwa waanze kupata
huduma hiyo mara moja.
Wakati Serikali ikiweka mikakati ya kujenga Ofisi za
TANESCO Wilaya, Naibu Waziri Nishati na Madini amemuagiza Meneja wa TANESCO
Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Rehema Mashinji kuteua maafisa watatu kutoka katika
Ofisi yake watakaowafuata wananchi vijijini badala ya wananchi kuifuata huduma
maofisini.
Aidha, Dkt Kalemani amelitaka Shirika la Umeme TANESCO
kuainisha wataalam wake wanaohusika na REA, kupeleka Orodha yao katika Ofisi za Vijiji na
kutoa elimu juu ya gharama na taratibu za kuunganisha umeme ili wananchi
wasidanganywe.
“Ili kudhibiti ulaghai wa kuongeza gharama ambazo
hazipo kila mtaalam awe na muhuri na majina yote ya wataalam wa TANESCO
yapelekwe katika Ofisi za Vijiji tuweze kuwatambua vishoka. Kuna watu wanaweza
kuwaongezea wanachi gharama wakati gharama halisi ni shilingi 27,000/= kwa yule
ambaye ameshasuka nyaya kwenye nyumba yake, na fomu anachukua bure.” Alisema
Kalemani.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Itilima, Mhe. Njalu
Silanga amesema anaishukuru Serikali kwa kuwaweka katika mpango wa kupata umeme
wananchi wa Wilaya ya Itilima na akawataka Wenyeviti wa Serikali za Vijiji kupita
katika kaya zote na kusaidia kubaini kaya zisizona umeme katika maeneo yao.
Wakati huo huo Mhe. Dkt. Kalemani amekitambulisha
kifaa cha kuweka umeme bila kusuka nyaya
ndani ya nyumba kiitwacho UMETA kinachotumika
kuunganisha umeme kwa gharama isiyozidi 36,000/=,ambapo amesema kifaa
hicho kinaweza kuwasaidia wananchi wasio na uwezo wa kusuka nyaya katika nyumba
zao.
Akizungumza mara baada ya hotuba ya Naibu Waziri,
Bibi.Milembe Katani mkazi wa Kijiji cha Nanga Kata ya Chinamili amesema
anaishukuru Serikali kwa kuweka mikakati ya kuwapelekea umeme kwa kuwa
utasaidia vijana wao kujiajri katika saluni, kuchomelea vyuma, na kuwekeza
katika Mashine za kukamua alizeti na kukoboa mpunga.
Naibu Waziri Dkt. Kalemani yuko Mkoani Simiyu kwa ajili
ya ziara ya Siku tatu ambapo amekagua miradi mbalimbali ya Wakala wa Umeme
Vijijini (REA) katika Wilaya za Busega, Bariadi na Itilima.
0 comments:
Post a Comment