Serikali Mkoani Simiyu imesema
asilimia mbili ya ushuru wa zao la pamba
inayopatikana katika Halmashauri zote za Mkoa wa Simiyu ielekezwe katika ujenzi
wa Miundombinu ya elimu ya msingi na sekondari,hususani vyumba vya madarasa.
Uamuzi huo umefikiwa
kufuatia majadiliano ya pamoja kati ya Uongozi wa Mkoa na Halmashauri zote
katika kikao kilichoongozwa na Mkuu wa
mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony J. Mtaka akiwa na Wakuu wa Wilaya, Wenyeviti wa
Halmashauri, Wakurugenzi wa Halmashauri, Makatibu Tawala Wilaya na Wajumbe wa
Kamati za Fedha za Halmashauri ili kujadili mstakabali wa ujenzi wa vyumba vya
madarasa katika mkoa huo.
Mtaka amewaelekeza
Wakurugezi wote wakafanye uhakiki na kuainisha takwimu sahihi za mahitaji ya vyumba vya madarasa ili kupata
uhakika wa vyumba vinavyohitajika katika mkoa mzima na kupanga mkakati wa namna
vyumba hivyo vitakavyojengwa ikiwa ni pamoja na teknolojia itakayotumika katika
kufyatua matofali pamoja na gharama zake
na kuwasilisha taarifa katika Ofisi yake tarehe 9 Agosti, 2016, ambapo baada ya
kupata taarifa hiyo na kujiridhisha zoezi la ufyatuaji matofali kimkoa
litazinduliwa rasmi Wilayani Maswa tarehe itakayopangwa na mkoa.
“ Sina uhakika sana na
takwimu hizi, niwaagize tena Wakurugenzi wote mkafanye mapitio upya na uhakiki
wa kina katika maeneo yenu juu ya idadi ya vyumba vya madarasa vinavyohitajika
kwa Elimu ya Msingi na Sekondari. Mkae na wataalam wenu wa ujenzi mfanye
tathmini ya namna mtakavyojenga kama mtatumia matofali ya kuchoma, matofali ya
block au matofali yakufungamana (interlocking blocks) yanayofyatuliwa na vijana
waliopewa mafunzo na Shirika la Nyumba la Taifa,ambao wako katika kila halmashauri
pamoja na gharama zitakazotumika”, alisema Mtaka.
Kwa upande wake Katibu
Tawala Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini amewataka Wakurugenzi kufanya utaratibu
wa kubadilisha matumizi ya fedha haraka pale inapobidi kwa kufuata sheria kanuni na
taratibu kufanikisha zoezi la ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kuwatengenezea
wanafunzi mazingira mazuri ya kujifunzia na kuwezesha madawati yaliyotengenezwa
ambayo hayana mahali pa kuwekwa yasiharibike kwa kupigwa na jua na kunyeshewa
na mvua.
Pamoja na kutenga
asilimia mbili ya ushuru wa pamba, Mtaka amesema Mkoa unakusudia kufanya
Harambee kubwa itakayowashirikisha viongozi na wadau wengine muhimu kutoka
ndani na nje ya mkoa ambao watachangia kwa kuunga mkono jitihada za Serikali
Mkoani humo, katika kuondoa tatizo la upungufu wa vyumba vya madarasa kwa Mkoa
wa Simiyu.
Akichangia hoja hiyo ya
harambee Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi , Mhe.Mashimba Ndaki amesema, hiyo
itakuwa ni fursa kwa wenyeji wa Mkoa wa Simiyu walo ndani na nje kuchangia maendeleo ya Mkoa wao na
akasisisitiza fedha zitakazokusanywa zisimamiwe vizuri na viongozi.
Katika hatua nyingine
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu amekabidhi simu tano kwa Wakuu wa Wilaya tano za Mkoa
huo zilizotolewa na idara ya mahakama kwa lengo la kutekeleza mpango wa mapambano dhidi ya rushwa na vitendo vinavyokwenda
kinyume na maadili ya Utumishi wa Umma katika utoaji wa huduma za Mahakama,
ambazo zitagawanywa kwa maafisa wa dawati la malalamiko kwa kila Ofisi ya Mkuu
wa Wilaya na akaelekeza zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa.
Aidha, Mtaka amewataka
Wakuu wa Wilaya kutenga siku maalum ya kusikiliza kero za wananchi ambayo Mkuu
wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri
watakaa kuwasilikiliza wananchi na
kuwapatia ufumbuzi na pale inaposhindikana masuala yao yapelekwe Ofisi ya Mkuu
wa Mkoa kwa ajili ya hatua zaidi.
0 comments:
Post a Comment