Wednesday, August 10, 2016

NAIBU WAZIRI AAGIZA UTORO MASHULENI UDHIBITIWE KUPUNGUZA IDADI YA WASIOJUA KUSOMA NA KUANDIKA



Na Stella Kalinga
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mhandisi Stella Manyanya ameutaka Uongozi wa Mkoa kudhibiti utoro wa wanafunzi ili kupunguza idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika katika nchi hii.

Naibu Waziri amesema hayo  wakati alipozungumza na Viongozi wa Mkoa na Maafisa Elimu wa Halmashauri zote 6 za Mkoa wa Simiyu, wakati wa ziara yake Mkoani humo ambayo ilikuwa na lengo la kuona eneo la ujenzi wa Chuo cha Elimu ya  Mafunzo Stadi (VETA), kinachotarajiwa kujengwa Mtaa wa Bunamhala, Mjini Bariadi na kupata taarifa juu ya masuala mbalimbali katika sekata ya elimu.

Mhandisi Manyanya amesema hadi sasa takribani asilimia 29 ya Watanzania hawajui kusoma na kuandika, hivyo zinahitajika jitihada za dhati katika kukabiliana na ongezeko la watu wasiojua kusoma na kuandika kwa kuendeleza elimu ya watu wazima, kuhakikisha madarsa ya MEMKWA yanafundishwa na walimu (wenye sifa) wanaofundisha madarasa mengine na kuwaweka wanafunzi wa Madarasa hayo katika Mpango wa Elimu ya Bila malipo, ambapo alieleza kuwa taasisi za elimu zitumike kama vituo vya elimu ya watu wazima. 

“Tusipowekeza katika elimu hatuwezi kufikia kwenye uchumi wa kati kwa haraka, tunataka tufike mahali mtu apate taarifa za afya, masoko na mambo mengine kupitia simu yake ya kiganjani, sasa kama mtu hawezi kujua kusoma na kuandika itakuwa vigumu sana”, alisema Manyanya.

Aidha, Mhandisi Manyanya ilisema ili  kufikia uchumi wa kati ipo haja ya kuwa na vyuo vya mafunzo ya ufundi na ujuzi mbalimbali, hivyo kulingana na umuhimu wa mafunzo hayo Serikali imekusudia kujenga vyuo vya Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) katika kila mkoa, ambapo  katika bajeti ya mwaka fedha 2016/2017 imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Vyuo hivyo kwa mikoa minne ukiwepo Mkoa wa Simiyu, ambao umetenga eneo lenye ukubwa wa jumla ya ekari 81 kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho.

Akizungumza na Naibu Waziri wakati alipotembelea eneo liltotengwa kwa ajli ya ujenzi wa chuo cha VETA Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka amesema Mkoa utahakikisha miundombinu muhimu inapatikana katika eneo hilo ili Chuo kitakapojengwa wanafunzi wapate huduma zote muhimu.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa huo ametoa wito kwa Wizara kuijengea uwezo Idara ya Ukaguzi ili iweze kutekeleza majukumu yake sawa sawa hususani kuwapatia vyombo vya usafiri badala ya kuiacha idara hii iwe tegemezi kwa Wakurugenzi wa Halmashauri.

Akitoa ufafanuzi juu ya suala hilo Naibu Waziri amesema Wizara itaiwezesha idara hii na imeanza kwa kutoa magari 40 katika wilaya 40 ili iweze kufanya kazi ya udhibiti ubora katika sekta ya elimu kwa kuhakikisha shule zina mahitaji na miundombinu muhimu ya kuwawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira mazuri ikiwa ni pamoja na uwepo wa matundu ya vyoo ya kutosha.

Mhandisi Manyanya amesema kulingana na umuhimu wa elimu katika nchi hii, jumla ya shilingi bilioni 4.3 zimetengwa kwa ajili ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, katika mwaka wa fedha 2016/2017.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Emmanuel Mgongo, akiwasilihsa taarifa ya ujenzi wa  Chuo Cha Mafunzo ya ufundi Stadi (VETA) cha Mkoa wa Simiyu kinachotarajiwa kujengwa Mtaa wa Bunamhala, Mjini Bariadi kwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mhandisi Stella Manyanya, wakati alipokuwa katika ziara ya siku moja mkoani humo. (Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu)

: Afisa Mipango Miji wa Halmashauri ya Mji Bariadi, Bw. Dennis Rashid (aliyenyoosha mkono) akimuonesha Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mhandisi Stella Manyanya (wa pili kushoto) Eneo la Chuo Cha Mafunzo ya ufundi Stadi (VETA) cha Mkoa wa Simiyu kinachotarajiwa kujengwa Mtaa wa Bunamhala, (kutoka kulia)Afisa Elimu Mko, Julius Nestory, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, (kulia) ni Mkurugenzi wa VETA Kitengo cha Masoko, Ajira  na Mipango Enock Kibendera. (Picha Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.)

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mhandisi Stella Manyanya akizungumza na Viongozi wa Mkoa na Maafisa Elimu kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Simiyu (baadhi hawapo pichani) katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wakati wa ziara yake Mkoani humo. (Picha Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.

Baadhi ya Maafisa Elimu wa Halmashauri za Mkoa wa Simiyu wakimsikiliza Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mhandisi Stella Manyanya (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao juu ya masauala mbalimbali yanayohusu sekta ya elimu wakati wa ziara yake mkoani humo. (Picha Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.)

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, (kulia) akimsikiliza  Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mhandisi Stella Manyanya akizungumza na Viongozi wa Mkoa na Maafisa Elimu kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Simiyu  (hawapo pichani), katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wakati wa ziara yake Mkoani humo. (Picha Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.


Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mhandisi Stella Manyanya (wa pili kulia) akipata maelezo ya Mchoro wa Chuo Cha Mafunzo ya ufundi Stadi (VETA) cha Mkoa wa Simiyu kinachotarajiwa kujengwa Mtaa wa Bunamhala, Mjini Bariadi kutoka kwa Afisa mipango Miji wa Halmashauri ya Mji Bariadi, Bw. Dennis Rashid (wa pili kushoto), kulia Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka. (Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu)

  

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!