Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amewataka
vijana wa Mkoa huo na Tanzania kwa ujumla kutambua na kuchangamkia fursa za uchumi
na maendeleo badala ya kujiingiza katika masuala ya siasa zisizo na tija.
Mkuu huyo wa Mkoa
amesema hayo katika ufunguzi wa semina ya Vijana Wajasiriamali iliyolenga
kuwasaidia kutambua fursa za biashara na uchumi inayondeshwa na CLUODS Media
Group kwa kushirikiana na Wataalam mbalimbali, ikiwa na Kauli Mbiu ya “FURSA
2016-Ongeza Thamani” ambayo imeshirikisha vikundi vya vijana kutoka wilaya zote
tano za mkoa huo.
Mtaka
amesema Serikali Mkoani humo itawachukulia hatua Wanasiasa wote watakaotaka
kuwafanya vijana wa Mkoa huo kuandamana Septemba Mosi, 2016 na badala yake
Serikali inawataka vijana hao kujikita katika fursa zilizopo Mkoani humo, kwa kuwa inayo dira na
malengo ya kuwasaidia vijana kujikwamua kutoka katika umaskini.
“ Ni vizuri uwaache wanasiasa wanaotaka
kufanya majaribio na Serikali watoke wao na familia zao, kwa sababu hizo nyumba
wanazokaa za viyoyozi hukai wewe, kwenye magari ya viyoyozi wanayotembelea
hutembelei wewe, usiwe fursa ya Wanasiasa waganga njaa”, alisema Mtaka.
Mtaka
amesema azma ya Serikali katika Mkoa wa Simiyu ni kuwa kila wilaya izalishe zao
moja ambalo litaitambulisha wilaya husika yaani (one product one district) ambapo
alieleza kuwa, Wizara yenye dhamana na Vijana imeshatoa zaidi ya shilingi 69,000,000
kwa ajili ya Vijana wa Meatu na Maswa, hivyo akawataka kabla ya tarehe 14 Oktoba, 2016 Vijana wa Wilaya ya
Meatu waanze kuzalisha maziwa ya ng’ombe
asilia, Vijana wa wilaya ya Maswa waanze kuzalisha chaki ambazo zitatumika
katika shule za Mkoa huo mikoa mingine nchini.
Katika
Tanzania ya Viwanda Serikali mkoani Simiyu imedhamiria Mkoa huo kwenye sekta ya
Viwanda uwe Mkoa unaozalisha mahitaji madogo mdogo ya wananchi kama vile pamba
inyotumika hospitali kufungia na kusafishia vidonda, pamba za masikioni badala
ya kuagiza vitu hivyo kutoka nje ya nchi, kwa kuwa Mkoa wa Simiyu unazalisha
takribani asilimia 55 ya pamba nchini
Aidha,
Mtaka amesema Serikali imejipanga kuongeza uzalishaji wa pamba bora kutoka tani
milioni 70 mwaka 2015/2016 hadi kufikia tani 200 mwaka 2017/2018 kwa kuwa imeweka mipango ya
kuwawezesha Maafisa Ugani ngazi zote ili wawape msaada wa kitaalam wakulima
walime kilimo bora chenye tija.
Akizungumza
katika semina hiyo mmoja wa wawezesheshaji, Charles Ndugu amesema ili
wafanyabiashara na wajasiriamali waweze kuzitangaza bidhaa na huduma
wanazozitoa wajikite katika kutoa huduma bora kwa wateja,udhibiti ubora wa
huduma/bidhaa, biashara zao ziwe na mwendelezo katika utoaji wa huduma na pia
bidha zao ziwe na muonekano mzuri kwa wateja.
Nae
Hassan Ngoma amewataka vijana wajasiriamali kutofanya biashara kwa mazoea na
badala yake watafute taarifa na maarifa sahihi juu ya fursa mbalimbali za biashara
wanazozifanya.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Vipindi wa Clouds, Ruge Mtahaba amesema wao kama Clouds
wamenzisha semina za namna hii wakishirikiana na Wataalam mbalimbali, kwa lengo
la kuwasaidia vijana na wananchi wote kwa ujumla katika kuanzisha mawazo,
kuyalea, kuyakuza na kufika mahali pa kupanuka kuwa biashara na akatoawito kwa
vijana kuachana na dhana ya kusoma kwa lengo la kutaka kuajiriwa badala yake
wasome wakiwa na malengo ya kujiajiri.
CLOUDS
Media Group kupitia “FURSA 2016-Ongeza
Thamani” itatembelea mikoa 22 na Simiyu ni Mkoa wa tatu tangu ilipoanza kwa
mwaka 2016.
0 comments:
Post a Comment