Saturday, February 24, 2018

RITA KUANZA USAJILI NA KUTOA VYETI VYA KUZALIWA KWA WATOTO CHINI YA MIAKA MITANO MWEZI MACHI SIMIYU


Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini hapa nchini (RITA) unatarajia kuanza kutekeleza mpango wa kusajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kuanzia mwezi Machi ,  mwaka huu mkoani Simiyu.

Hayo yameelezwa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa RITA, Bi.Emmy Hudson wakati wa Ufunguzi wa semina ya viongozi ngazi ya Mkoa na wilaya iliyofanyika Mjini Bariadi kwa lengo la kuwapa uelewa wa kina viongozi hao juu ya mpango huu utakaotekelezwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Amesema hali ya usajili nchini hairidhishi ambapo amebainisha kuwa, kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 ni asilimia 13.4 tu ya wananchi hapa nchini ndiyo waliosajiliwa na kupewa vyeti vya kuzaliwa.

Ameongeza kuwa ili kuboresha mazingira ya usajili nchini Wakala wa  Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) imeandaa mkakati wa maboresho ya kuhakikisha kuwa kila tukio la uzazi linalotokea nchini linasajiliwa kwa wakati,  ambao pia unalenga makundi matatu la kwanza likiwa ni la watoto chini ya  miaka mitano, kundi la miaka mitano hadi 17 na kundi la miaka 18 na kuendelea.

“Tutakuwa hapa Simiyu kusajili watoto wa umri wa chini ya miaka mitano ambao idadi yao ni 351, 000,  takwimu zinaonesha ni asilimia tano tu ya watoto ndiyo waliosajiliwa, kwa hiyo hali ya usajili na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa Simiyu iko chini na ndiyo maana RITA tumeona tuje ili watoto wote wa Simiyu wapate vyeti vya kuzaliwa na kusajiliwa” alisema Kaimu Mtendaji Mkuu RITA.

Amesema RITA itafanya kampeni kwa muda wa wiki mbili za mwanzo ili kuwaandikisha watoto wote ambao walikuwa hawajaandikishwa na kupewa vyeti vya kuzaliwa, baada ya hapo watoto wote watakaozaliwa baada ya hiyo kampeni wataandikishwa katika Ofisi za Watendaji wa Vijiji, Kata na kwenye vituo vya Tiba ili kusogeza huduma karibu na wananchi.

Aidha, Kaimu mtendaji Mkuu RITA amesema katika kuhakikisha kila mtoto anasajiliwa Serikali imeondoa ada kwa kundi la watoto walio chini ya umri wa miaka mitano hivyo wananchi watapata huduma hii bila malipo yoyote.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amesema watumishi watakaoshiriki zoezi la usajili na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto chini ya miaka mitano hususani Watendaji wa Kata naVijiji wajengewe uwezo na akaziagiza Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya Mkoani humo  kusimamia zoezi hili ili lifanyike kwa ufanisi mkubwa na uzalendo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt.Seif Shekalaghe amesema mpango huu wa usajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto chini ya miaka mitano utawasaidia wananchi kupata huduma karibu na maeneo wanayoishi (Ofisi za Watendaji wa Kata na Vijiji) kwa kuwa awali walikuwa wanalazimika kwenda kwenye Ofisi za Wakuu wa Wilaya ili kupata vyeti hivyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Ndg.Abdallah Malela amesema viongozi wa Wilaya watahakikisha kila mtoto anayezaliwa anaandikishwa kupitia Ofisi za Watendaji wa Kata na Vijiji na kupewa cheti,  jambo litakalowasaidia kupata takwimu zitakazotumika kufanya maoteo ya wanafunzi wanaopaswa kuanza darasa la kwanza na darasa la awali miaka ijayo.

Kikao hiki kiliwahusisha Wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama Mkoa na Wilaya, Makatibu Tawala Wasaidizi wa Sekretarieti ya Mkoa, Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa na Wilaya, Maafisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya, Waganga Wakuu wa Wilaya, Waratibu wa Huduma za Afya ya mama  na mtoto pamoja na watumishi wanaoshughulikia usajili wa vyeti vya kuzaliwa katika Ofisi za Wakuu wa Wilaya.


Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini Tanzania (RITA) Bi.Emmy Hudson akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Simiyu wakati wa ufunguzi wa Semina ya Viongozi hao yenye lengo la kuwapa uelewa wa kina juu ya mpango maboresho ya usajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, iliyofanyika jana Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akifungua Semina ya Viongozi wa Mkoa huo iliyoandaliwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini Tanzania (RITA) kuhusu elimu ya ya mpango wa maboresho ya usajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano, iliyofanyika jana Mjini Bariadi.

Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg. Jumanne Sagini akifafanua jambo katika Semina ya Viongozi wa Mkoa huo iliyoandaliwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini Tanzania (RITA) kwa lengo la kuwapa uelewa wa mpango wa maboresho ya usajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano, iliyofanyika jana Mjini Bariadi.
Baadhi ya Viongozi wa Mkoa wa Simiyu wakiwa katika semina ya kuwapa uelewa wa mpango wa maboresho ya usajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ambayo iliandaliwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini Tanzania (RITA) iliyofanyika jana Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(katikati walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Simiyu na watumishi wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini Tanzania (RITA), mara baada ya kufungua Semina ya Viongozi wa Mkoa huo iliyoandaliwa na RITA Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(katikati walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Simiyu mara baada ya kufungua Semina ya Viongozi hao iliyoandaliwa na RITA Mjini Bariadi.

Friday, February 23, 2018

SIMON GROUP YACHANGIA MILIONI 25 UJENZI WA MIUNDOMBINU YA ELIMU SIMIYU


Kampuni ya Simon Group imechangia kiasi cha Shilingi Milioni 25 kwa ajili ya Ujenzi wa Miundombinu ya Elimu  katika mkoa wa Simiyu.

Akikabidhi hundi hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Simon Group, Ndg. Leonard Kitwala amesema  Kampuni hiyo imetoa fedha hizo ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika maendeleo ya Sekta ya Elimu na kwa kuwa Simiyu ni mahali alipozaliwa Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Ndg. Simon Kisena ameona ni vema  asaidie maendeleo ya elimu nyumbani kwao.

Aidha, Kitwala amesema kama kampuni wameamua kuunga mkono ujenzi wa miundombinu ya Elimu Simiyu kwa kuwa wamependezwa na juhudi za Viongozi wa Mkoa wa Simiyu, wakiongozwa na mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka katika kuwaletea maendeleo wananchi katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu.

Akipokea hundi ya shilingi milioni 25 kwa niaba ya Viongozi na wanafunzi wa  Mkoa wa Simiyu, Mkuu wa Mkoa huo Mhe.Anthony Mtaka amesema anaishukuru Kampuni ya Saimon Group ambayo inaendesha mradi wa Usafrishaji wa Mabasi Dar es Salaam(UDA) kwa kuamua kuchangia ujenzi wa miundombinu ya elimu mkoani humo.

“Nawashukuru sana SAIMON GROUP kwa kuamua kusaidia ujenzi wa miundombinu ya elimu Simiyu, shilingi milioni 25 ni fedha nyingi sana kwenye kufanikisha ujenzi wa mundombinu ya elimu  hasa kwa mkoa kama wa kwetu ambao shughuli nyingi za ujenzi tunatumia “Force Account” , tunatumia nguvu za wananchi na Serikali ina nafasi yake  katika ujenzi wa miradi hiyo” alisema

“ Zaidi sana namshukuru Mkurugenzi wa SIMON GROUP ndugu Robert Kisena ambaye ni  mzaliwa  wa Mkoa huu kwa kuona arudishe sehemu ya faida ya biashara zake nyumbani, kwa niaba ya viongozi wenzangu ninamkikishia kwamba mchango huu utaenda kwenye matokeo yanayoonekana, hata wakati wa uzinduzi wa madarasa yatakayojengwa tutaipa  nafasi Kampuni ya SIMON GROUP kuja kuona alama waliyoweka katika mkoa wetu” alisisitiza Mtaka.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Mhe.Robert Lweyo amesema mchango huo wa SIMON GROUP umekuja katika muda muafaka ambao mkoa huo una uhitaji mkubwa wa vyumba vya madarasa hivyo alimshukuru Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Ndg. Robert Kisena na kuahidi pia kuwa fedha hizo zitafanya kazi iliyokusudiwa..
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(kushoto) akipokea hundi ya shilingi milioni 25 iliyotolewa na Kampuni ya SIMON GROUP kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya elimu kutoka kwa Ndg.Leonald Kitwala ambaye aliyekabidhi kwa niaba ya Mkurugenzi wa Kampun hiyo Ndg.Robert Kisena.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Mhe.Robert Lweyo akitoa shukrani kwa Kampuni ya SIMON GROUP kupitia  kwa Ndg.Leonald Kitwala aliyekabidhi hundi ya Shilingi Milioni 25 kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (hayupo picha) kwa niaba ya Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Ndg.Robert Kisena, kwa ajili ya Ujenzi wa Miundombinu ya Elimu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(kushoto) akipokea hundi ya shilingi milioni 25 iliyotolewa na Kampuni ya SIMON GROUP kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya elimu kutoka kwa Ndg.Leonald Kitwala ambaye aliyekabidhi kwa niaba ya Mkurugenzi wa Kampun hiyo Ndg.Robert Kisena

MAKAMU WA RAIS AKEMEA TABIA YA KUPEANA ZABUNI ZA UJENZI WA MIRADI KINDUGU


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan amekemea tabia ya baadhi ya viongozi kuwapa ndugu au jamaa zao zabuni za ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwepo miradi ya maji kwa kuwa ni kinyume cha taratibu na hali hiyo haiwatendei haki wananchi na Serikali.

Mhe.Makamu wa Rais aliyasema hayo jana katika kikao cha majumuisho alichokifanya mara baada ya kuhitimisha ziara yake ya siku nne mkoani humo ambayo aliianza tarehe 19/02/2018.

Amesema miradi mingi hususani miradi ya maji katika maeneo mengi mkoani humo haitekelezwi kwa wakati na katika kiwango cha ubora unaotakiwa kwa kuwa baadhi ya viongozi wamekuwa wakipeana miradi hiyo kwa kuzingatia undugu/ ukaribu wao badala ya kuangalia sifa zinazotakiwa.

“Miradi mingi ya maji imeshindwa kwenye baadhi ya maeneo kwa sababu mmepeana kindugu ndugu, mnashindwa kukemeana mnashindwa kusimamiana miradi haiendi, msiwadhulumu wananchi haki yao; mlizoea huko nyuma mnachukua fedha za miradi na hamfanyi lakini siyo sasa hivi” alisema.

Mhe.Makamu wa Rais aliwaagiza Wakuu wa Wilaya kuwasilisha taarifa yenye orodha ya  miradi inayotekelezwa katika maeneo yao, mtu anayetekeleza, hatua iliyofikia, tarehe ya kumaliza mradi na ikiwa haijamalizika ioneshwe sababu za kutokamilisha miradi hiyo kwa wakati, lengo likiwa ni kutoa nafasi kwa vyombo vya dola kufanya kazi yake.

Aidha, amevitaka vyombo  vya dola ikiwemo Taasisi ya Kuzui na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) kufuatilia Miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri zote mkoani humo.

Sanjali na hilo Mhe.Makamu wa Rais amewataka viongozi mkoani Simiyu kufanya kazi kwa kushirikiana ili kuwaletea wananchi maendeleo katika maeneo yao.

Wakati huo Mhe.Makamu wa Rais amewapongea viongozi na wananchi Mkoani Simiyu kwa kufanya vizuri katika sekta ya Kilimo hususani Kilimo cha zao la pamba na akaahidi kuwa Serikali itahakikisha wakulima wanapata dawa za kuuwa wadudu waharibifu ili malengo ya kuongeza mavuno mwaka huu kufikia kilo milioni 300 yaweze kutimia.

Vile vile amewapongeza kwa kutekeleza Sera ya Tanzania ya Viwanda kwa kuanzisha viwanda katika maeneo mbalimbali kupitia Mkakati wa “Wilaya moja Bidhaa moja” ambapo amesema Serikali inakusudia kujenga Kiwanda cha Bidhaa za Afya zitokanazo na pamba (Bariadi) na Maji wanayotundikiwa wagonjwa(IV Fluid/Drip) katika wilaya ya Busega.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amehitimisha ziara yake jana Mkoani Simiyu ambapo alikuwa Mgeni Rasmi katika mahafali ya 34 ya Chuo kikuu Huria cha Tanzania yaliyofanyika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Simiyu katika kikao cha majumuisho ya ziara yake ya siku nne aliyoianza tarehe 19/02/2018 hadi 22/02/2018 mkoani humo
Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Simiyu(waliokaa mbele) pamoja na viongzoi wengine wakimsikiliza Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan (hayupo pichani)katika kikao cha majumuisho ya ziara yake ya siku nne aliyoianza tarehe 19/02/2018 hadi 22/02/2018 mkoani humo
Baadhi ya Viongozi wa Chama Tawala na Serikali mkoani Simiyu wakimsikiliza Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan(hayupo pichani) katika kikao cha majumuisho ya ziara yake ya siku nne aliyoianza tarehe 19/02/2018 hadi 22/02/2018 mkoani humo
Baadhi ya Viongozi na Watumishi wa Serikali Mkoani Simiyu wakimsikiliza Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan(hayupo pichani) katika kikao cha majumuisho ya ziara yake ya siku nne aliyoianza tarehe 19/02/2018 hadi 22/02/2018 mkoani humo
Baadhi ya Viongozi na Watumishi wa Serikali Mkoani Simiyu wakimsikiliza Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan(hayupo pichani) katika kikao cha majumuisho ya ziara yake ya siku nne aliyoianza tarehe 19/02/2018 hadi 22/02/2018 mkoani humo

MAKAMU WA RAIS AKITAKA CHUO KIKUU HURIA KUONGEZA UDAHILI KUSAIDIA TANZANIA KUFIKIA UCHUMI WA KATI


Makamu wa Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amekitaka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kuongeza  ubora na kupanua wigo wa udahili wa wanafunzi  kwenye programu za sasa ili kuendana na Sera Tanzania ya viwanda na kufikia Uchumi wa kati ifikapo 2025.
Ushauri huo ameutoa katika mahafali ya 34 ya Chuo Kikuu Huria cha TANZANIA  yaliyofanyika katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu.

Makamu wa Rais amesema kuwa ili kuweza kufikia TANZANIA ya viwanda na kufikia uchumi wa kati 2025 lazima udahili wa wanafunzi katika vyuo vikuu ufikie kiwango cha angalau  asilimia 23.
“Naungana na Mhe.Rais kuwaomba muisaidie nchi yetu kuongeza kiwango cha udahili wa wananchi wake kwa haraka na kwa kasi itakayotuwezesha kufikia lengo la kuwa nchi ya Uchumi wa kati ifikapo 2025” alisema

“Kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia kiwango kidogo cha udahili katika elimu ya juu ni sifa ya msingi ya Uchumi wa chini na wa kimaskini, Uchumi wa kati na wa Viwanda hauwezi kufikiwa na kuwa endelevu pasipokuwa na kiwango cha udahili katika elimu ya juu  cha angalau asilimia 23” alisema Makamu wa Rais.

Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe.William Ole Nasha amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania katika maendeleo ya sekta ya elimu nchini kwa kuwa kimekuwa mtekelezaji mkuu wa malengo na mikakati ya Serikali kwa upande wa ujifunzaji kwa njia za masafa.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Profesa Elifas Bisanda amesema tangu Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kianzishwe idadi ya wahitimu imefikia 38, 993 baada ya mahafali ya 34 idadi hiyo imeongezeka kufikia 39,934, jambo ambalo limechangia  kukuza rasilimali watu hapa nchini.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu amesema kufanyika kwa  mahafali ya 34 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania mkoani humo kutakuwa chachu na kutaleta mwamko mpya wa elimu kwa wananchi Mkoani humo.

“Tuliona tuwaalike wanafunzi ili kujenga hamasa kwao, tulialika kamati zetu za shule, madiwani, walimu na wananchi wote wa Simiyu ili washuhudie tukio hili tukiamini kuwa kwa kuona tukio hili kila mmoja atatamani kuwa hivyo kesho,  kama siyo yeye basi awe  mwanaye au ndugu yake” alisema Mtaka.

Jumla ya wahitimu 941 kutoka Tanzania bara na Zanzibar na nchi jirani  walihudhurishwa mbele ya Mkuu wa Chuo Kikuu Huria  Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda na kutunukiwa  Astashaha, stashahada, shahada, shahada za uzamili , ambapo miongoni mwa hao 941 wahitimu saba walitunukiwa  shahada ya uzamivu(PhD).


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akishiriki matembezi ya mahafali ya 34 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania pamoja na Mkuu wa chuo hicho Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda (kulia) kuelekea  Uwanja wa Halmashauri ya  Mji wa Bariadi kwenye sherehe za mahafali hayo zilizofanyika Mjini Bariadi Mkoa  wa Simiyu.(Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Huria Tanzania Profesa Rwekaza Mukandala wakati wa mahafali ya 34 ya chuo hicho yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu. .(Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Baadhi ya Wahitimu waliohitimu katika Mahafali ya 34 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyofanyika katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu. .(Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)

Baadhi ya Wahitimu waliohitimu katika Mahafali ya 34 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyofanyika katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu. .(Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Wahitimu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na wananchi wa Mkoa wa Simiyu katika Mahafali ya 34 ya Chuo hicho yaliyofanyika katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani humo.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na Wahitimu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na wananchi wa Mkoa huo katika Mahafali ya 34 ya Chuo hicho yaliyofanyika katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani humo.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof.Elifas Bisanda akizungumza na Wahitimu wa Chuo hicho na wananchi wa Mkoa wa Simiyu katika Mahafali ya 34 ya Chuo hicho yaliyofanyika katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani humo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan(kulia),  Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof.Elifas Bisanda(kushoto) Mkuu wa chuo hicho Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda (katikati) wakishangilia jambo katika Mahafali ya 34 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyofanyika katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan( wa nne kulia),  akiwa katika Picha ya pamoja na Viongozi wa Chuo Kikuu huria cha Tanzania na Viongozi wa Mkoa wa Simiyu mara baada ya Mahafali ya 34 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, yaliyofanyika katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu(kulia) Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka.

Thursday, February 22, 2018

SHIRIKA LA MAENDELEO LA UINGEREZA LATOA SHILINGI BILIONI 1.7 UJENZI WA MIUNDOMBINU YA ELIMU SIMIYU

Shirika la Mendeleo la Uingereza (DFID) kupitia Mpango wa Kuboresha Elimu Tanzania(EQUIP-T) limetoa jumla ya shilingi bilioni 1.7  kwa ajili ya ujenzi wa Miundombinu ya Elimu katika Halmashauri zote za mkoa wa Simiyu.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka wakati wa hafla fupi ya makabidhiano na vyerehani 50 kutoka Ubalozi wa China, kusaini hati ya makubaliano ya ujenzi wa Bweni la Wasichana Shule ya Sekondari Nkoma Itilima, Makabidhiano ya. Hundi ya Shilingi Milioni 178 kwa ajili ya ujenzi wa bweni hilo zilizotolewa na Balozi wa China, na uwasilishwaji wa Taarifa za mashirika wadau wa Maendeleo mkoani Simiyu(DFID, AMREF na UNFPA), ambayo ilishuhudiwa na Makamu wa Rais wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan.

Mtaka amesema fedha hizo zimeshapokelewa katika Akaunti za Halmashauri zote za Mkoa huo na wiki ya kuanzia tarehe 26/02/2018 Halmashauri hizo zinaanza kujenga miundombinu ya Elimu.
Mtaka ametoa shukrani zake kwa Shirika hilo ambalo amesema limechangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko katika Elimu na kuufanya mkoa wa Simiyu kutoka kwenye nafasi za mwisho kwenye ufaulu mpaka kufikia nafasi ya 11 kwa mwaka 2017.

“ Tunawashukuru sana DFID kwa namna wanavyotusaidia katika Sekta ya Elimu kwenye mkoa wetu,  DFID kupitia EQUIP wametoa IPAD(Vishikwambi) kwa kila Mkuu wa Shule ndani ya mkoa Simiyu, Kila Mratibu wa Elimu wa Elimu Kata amepewa  pikipiki na anapewa posho ya shilingi 206,000/=  kila mwezi kwa ajili ya kununua mafuta ya kuwawezesha  kutembelea  shule zao,  sisi kama mkoa tunawashukuru sana” alisema Mtaka.

Akitoa taarifa ya utendaji kazi wa Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID) Bi. Elizabeth Arthy amesema Shirika hilo litaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali  na kuhakikisha wanashiriki katika kuinua ubora wa elimu kwa watoto wa Mkoa wa Simiyu.

Naye Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke aliyekabidhi vyerehani 50 kwa ajili ya Kikundi cha Wanawake Mjini Bariadi  amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka kwa jinsi anavyojishughulisha katika kuwaletea wananchi wa Mkoa wa Simiyu maendeleo na akaahidi kuendelea kushirikiana na mkoa huo katika nyanja mbalimbali.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Shirika lilaloshughulikia Idadi ya Watu Duniani(UNFPA), Bi. Jacqueline Mahon amewapongeza viongozi wa mkoa wa Simiyu wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka na akaahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za maendeleo mkoani humo kupitia huduma za afya ya uzazi kwa wananwake na vijana.

Akitoa shukrani kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Simiyu,  Mbunge wa Jimbo la Bariadi Mhe.Andrew Chenge, aliyashukuru mashirika hayo na Balozi wa China ambao ni wadau wakubwa wa maendeleo mkoani humo katika Sekta ya elimu, afya na viwanda na kubainisha kuwa mkoa huo una kiu ya maendeleo ni hivyo umejipanga kwenda kwa kukimbia wakati wengine wanatembea.
MWISHO
Kutoka kushoto (wanaoandika) Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima wakisaini hati ya makubaliano ya Ujenzi wa Bweni la Wasichana katika Shule ya Sekondari Nkoma wilayani Itilima, fedha ambazo zimetolewa na Balozi wa China hapa nchini, Mhe.Wang Ke., zoezi ambalo lilishuhudiwa pia na Makamu wa Rais wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan Jana Mjini Bariadi..
Mwakilishi wa Shirika laUingereza la ( DFID) Bi. Elizabeth Arthy akiwasilisha taarifa ya namna Shirika hilo linavyofanya kazi na mkoa wa Simiyu mbele ya viongozi wa Kitaifa na Mkoa wa Simiyu, katika hafla iliyofanyika jana Viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mjini Bariadi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima(mwenye miwani) na Balozi wa China hapa nchini, Mhe.Wang Ke wakisaini hati ya makubaliano ya ujenzi wa Bweni la Wasichana katika Shule ya Sekondari Nkoma wilayani Itilima, fedha ambazo zimetolewa na Balozi huyo , zoezi ambalo lilishuhudiwa pia na Makamu wa Rais wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka na viongozi wengine wa Kitaifa na Mkoa mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akimshukuru Balozi wa China hapa Nchini, Mhe.Wang Ke mara baada ya kusaini hati ya makubaliano ya ujenzi wa Bweni la Wasichana katika Shule ya Sekondari Nkoma wilayani Itilima, fedha ambazo zimetolewa na Balozi huyo , zoezi ambalo lilishuhudiwa pia na Makamu wa Rais wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan(katikati) na viongozi wengine wa Kitaifa mjini Bariadi.
Balozi wa China hapa Nchini, Mhe.Wang Ke akimkabidhi  Makamu wa Rais wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan Hundi ya Shilingi milioni 178 kwa ajili ya ujenzi wa Bweni la Wasichana katika Shule ya Sekondari Nkoma wilayani Itilima, fedha ambazo zimetolewa na Balozi huyo kwa Serikali mkoani Simiyu.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akionesha Hundi ya Shilingi milioni 178 iliyotolewa na Balozi wa China hapa nchini, Mhe.Wang Ke kwa ajili ya ujenzi wa Bweni la Wasichana katika Shule ya Sekondari Nkoma wilayani Itilima zoezi lililofanyika jana Mjini Bariadi.
Balozi wa China hapa nchini, Mhe.Wang Ke akitoa maelezo kwa  Makamu wa Rais wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan(wa pili kulia) kabla ya kumkabidhi vyerehani 50 kwa ajili ya kikundi cha wanawake wa Mjini Bariadi zoezi lililofanyika jana Mjini Bariadi.
Makamu wa Rais wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan na viongozi wa Mkoa wa Simiyu pamoja na Halmashauri ya Mji wa Bariadi wakipokea cherehani kama ishara ya makabidhiano ya vyerehani 50 kutoka kwa Balozi wa China hapa nchini, Mhe.Wang Ke, zoezi lililofanyika jana mjini Bariadi.
Mwakilishi Mkaazi wa Shilika la umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu Duniani(UFPA) Bi. Jacqueline Mahon akiwasilisha taarifa ya namna Shirika hilo linavyofanya kazi na Mkoa wa Simiyu katika kikao kilichofanyika jana Mjini Bariadi.
Kiongozi wa AMREF Tanzania, Bi. Florence Temu akiwasilisha taarifa ya namna Shirika hilo linavyofanya kazi na Mkoa wa Simiyu kwa Viongozi wa Kitaifa na Mkoa katika Hafla  iliyofanyika jana Mjini Bariadi.

Mbunge wa Jimbo la Bariadi, akitoa shukrani kwa wadau wote wanaounga mkono juhudi za Serikali katika kuwaletea maendeleo wakati wa uwasilishwaji wa taarifa za wadau hao kwa viongozi wa Kitafa na Mkoa katika hafla iliyofanyika jana Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akiteta jambo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa makabidhiano ya hundi ya shilingi milioni 178 za ujenzi wa Bweni Itilima, Vyerehani 50 viliyotolewa na Balozi wa China hapa nchini Mhe.Wang Ke kwa  kikundi cha wanawake Bariadi Mjini na uwasilishwaji wa taarifa za mashirika wadau wa maendeleo mkoa wa Simiyu jana jioni.

MAKAMU WA RAIS: ELIMU YA JUU NI NGUZO MUHIMU KATIKA KUFIKIA TANZANIA YA VIWANDA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Elimu hususani ya juu ni nguzo Muhimu ya kufikia Agenda ya Serikali ya kuwa na Tanzania ya Viwanda na kufikia Uchumi wa Kati ifikapo 2025.


Makamu wa Rais wa amesema hayo ,wakati wa akifungua kongamano la elimu ya juu na Tanzania ya viwanda lililofanyika mjini Bariadi, lililokuwa limeandaliwa na Chuo kikuu huria Tanzania kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.

Amesema kutokana na umuhimu huo Serikali imeamua kuwekeza katika Elimu na Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2025 imeweka elimu kuwa kipaumbele cha juu kwa kuwa ndiyo kitovu cha  kuleta mabadiliko ya kiuchumi katika jamii.

“Ninyi ni mashahidi kuwa Serikali imeweka mkazo kwenye elimu, tumeanza na shule za msingi, sekondari lakini pia tumeongeza bajeti kubwa kwenye mikopo ya Elimu ya Juu na tutakwenda polepole mpaka tuhakikishe Watanzania wanapata elimu ya kutosha ili kuendana na uchumi wa Viwanda” alisema.

Ameongeza kuwa  lengo kuu la ni Serikali kuongeza kipato cha wananchi kupitia viwanda ambavyo vitaongeza thamani ya mazao yanayozalishwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Aidha, amewataka washiriki wa Kongamano hilo kuja na majibu ya ni kwa  namna gani wahitimu wa Vyuo Vikuu walivyojipanga katika suala la uzalishaji viwandani na kubainisha  ikiwa fani, stadi na mafunzo waliyosomea yatakidhi mahitaji ya  viwanda vinavyotakiwa kujengwa hapa nchini.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof.Elifas Bisanda amesema nchi zote zilizoendelea katika Sekta ya Viwanda zina msukumo mkubwa na udahili mkubwa wa Wanafunzi wa Elimu ya Juu, hivyo  upo umuhimu wa kujadili Mchango wa Elimu ya Juu katika Tanzania ya Viwanda.

Aidha, Prof.Bisanda ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Simiyu kutumia fursa ya uwepo wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kwa ajili ya kujiendeleza katika masomo ya elimu ya juu.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amewataka waajiri wote mkoani humo kuwaruhusu watumishi kwenda kusoma kwa ajili ya kuwaandaa watumishi hao kuwa na maarifa ya kutosha.

 Tuna shida kwenye ofisi zetu  tena wakati mwingine  ni roho mbaya tu, mtumishi anaomba kwenda kusoma Mkurugenzi anamkatalia, tukitaka nchi yetu iende mbele turuhusu watu wasome,  miaka ijayo tunataka mkoa wetu ushindane hatuwezi kushindana kama hatutawekeza kwenye maarifa” alisisitiza Mtaka.

Wasomi waliowasilisha mada mbalimbali katika Kongamo hilo la Elimu ya Juu na Tanzania ya Viwanda ni pamoja na Prof. Rwekaza Mukandala, Prof.Elifas Bisanda , Prof.Uswege Minga, Dkt. Adolf Rutayuga, Dkt. George Mgode, Balozi Nicholas Kuhanga na Mhe.Anthony Diallo.

Kongamano hili lililokuwa na Mada kuu isemayo: “Mustakabali wa Elimu ya Juu kuelekea Tanzania ya Viwanda” limehudhuriwa na wanafunzi wa shule za sekondari, walimu, Wanafunzi wa Vyuo Vikuu kutoka Mwanza pamoja na viongozi wa Serikali.
MWISHO


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan aifungua Kongamano la Elimu ya Juu na Tanzania ya Viwanda lililofanyika Mjini Bariadi.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na Washiriki wa Kongamano la Elimu ya Juu lililofanyika Mjini Bariadi.
Baadhi ya Washiriki wa Kongamano la Elimu ya Juu na Tanzania ya Viwanda kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Simiyu wakifuatilia ufunguzi wa Kongamano hilo uliofanywa na  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan mjini Bariadi.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Elifas Bisanda akizungumza na Washiriki wa Kongamano la Elimu ya Juu lililofanyika Mjini Bariadi(hawapo pichani)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan(wa pili kushoto) akifurahia jambo na viongozi wa Mkoa wa Simiyu wakati wa Kongamano la Elimu ya Juu na Tanzania ya Viwanda lililofanyika Mjini Bariadi.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan(katikati walioketi ) akiwa katika picha ya pamoja na wawasilishaji wa mada  wa Kongamano la Elimu ya Juu na Tanzania ya Viwanda lililofanyika Mjini Bariadi.(waliosimama mstari wa nyuma) na viongozi wengine kutoka ndani na nje ya mkoa wa Simiyu.

MAKAMU WA RAIS AWATAKA WANANCHI KUCHANGIA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA ELIMU

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi mkoani Simiyu kuchangia ujenzi wa miundombinu ya elimu ili kuunga mkono jitihada za Serikali katika maendeleo ya Sekta ya Elimu.

Mhe.Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati  akizungumza na Wananchi wa Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu kwenye  Mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Nguzo Nane wakati wa ziara yake mkoani humo.

Amesema Serikali imeamua kutoa elimu bila malipo na kuwapunguzia wazazi mzigo wa kulipia gharama za karo na michango mbalimbali ya uendeshaji wa shule lakini suala la kuchangia ujenzi wa miundombinu ya elimu wananchi wanapaswa kuunga kuchangia ili kuunga mkono juhudi hizo.

“ Tunapeleka fedha katika shule zote za Msingi na Sekondari ili wanafunzi waweze kusoma vizuri lakini kwenye suala la ujenzi wa matundu ya vyoo, madarasa, maabara pamoja na kwamba Serikali ina wajibu wa kufanya hayo na ninyi wananchi mnao wajibu wa kusaidia kufanya hayo” alisema Mhe. Makamu wa Rais.

Wakati huo huo Mhe.Makamu wa Rais ameipongeza Wilaya ya Maswa kwa kuongeza ufaulu kutoka asilimia 45 hadi asilimia 75 kwa mwaka 2017 na akakemea vikali tabia ya wanaume wanaoua ndoto za watoto wa kike kwa kuwapa mimba , ambapo amesema jicho la Serikali liko kwa watoto wa kike na itawachukulia hatua kali wote watakaobainika kufanya hivyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt.Seif Shekalaghe amesema watoto wa kike 28 wameripotiwa kuwa na mimba katika kipindi cha mwezi Desemba 2017 hadi sasa na Serikali ya Wilaya kupitia Operesheni tokomeza Mimba imefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 15 na kati ya hao wawili wamehukumiwa miaka 30 jela kila mmoja.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki ambaye pia ni Naibu Waziri wa Madini , Mhe.Stanslaus Nyogo amewashukuru viongozi wa Wilaya kuleta mafanikio katika elimu ikiwa ni pamoja na ongezeko la ufaulu.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan mara baada ya kufungua Jengo la Upasuaji la Upasuaji Hospitali ya Wilaya ya Maswa ambalo limepewa jina lake “SAMIA SULUHU HASSAN OPERATING THEATER” amewataka Watumishi wa Afya kufanya kazi kwa bidii

Aidha, amesema Serikali itahakikisha inaboresha huduma za afya ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vituo vya Afya katika kila kata na kuboresha huduma za Afya ya Mama na Mtoto ili kupunguza Vifo vya mama na mtoto.

Naye Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe.Josephat Kandege amesema Serikali imekusudia kujenga vituo vya Afya 286 kufikia  mwisho mwa mwaka 2017/2018  lengo likiwa ni kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa kupunguza mrundikano wa wagonjwa katika Hospitali za Wilaya.
Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, Mhe.Mashimba Ndaki amesema pamoja na kuendelea kuboresha sekta ya Afya kwa kujenga miundombinu, ni vema Serikali ikaajiri watumishi wa Idara ya Afya kukabiliana na upungufu uliopo.

Mhe.Makamu wa Rais amemaliza Ziara yake Wilayani Maswa ambapo amefungua Jengo la Upasuaji la Upasuaji Hospitali ya Wilaya ya Maswa ambalo limepewa jina lake “SAMIA SULUHU HASSAN OPERATING THEATER” na kuzungumza na wananchi katika Uwanja wa Nguzo Nane.
MWISHO

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan akimwagilia mti wa mwembe alioupanda mara baada ya kufungua Jengo la Upasuaji la Hospitali ya Wilaya ya Maswa ambalo limepewa jina lake “SAMIA SULUHU HASSAN OPERATING THEATER” wakati wa ziara yake Mkoani Simiyu.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Maswa kwenye mkutano wa Hadhara uliofanyika katika uwanja wa Nguzo nane Mjini Maswa, wakati wa ziara yake wilayani humo.
Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki, Mhe.Stanslaus Nyogo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Madini akitoa maelezo kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan wakati alipokuwa akikagua Jengo la Upasuaji la Hospitali ya Wilaya ya Maswa ambalo limepewa jina lake “SAMIA SULUHU HASSAN OPERATING THEATER” mara baada ya kulifungua wilayani humo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan akikagua Hospitali ya Wilaya ya Maswa mara baada ya kufungua Jengo la Upasuaji la Hospitali ya Wilaya ya Maswa ambalo limepewa jina lake “SAMIA SULUHU HASSAN OPERATING THEATER” wakati wa ziara yake Mkoani Simiyu, (kulia mwenye miwani) Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt.Seif Shekalaghe akimuongoza.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan(katikati) akia katika picha ya pamoja na viongozi wa Chama na Serikali wa Wilaya ya maswa na Mkoa wa Simiyu mara baada ya kufungua Jengo la Upasuaji la Hospitali ya Wilaya ya Maswa ambalo limepewa jina lake “SAMIA SULUHU HASSAN OPERATING THEATER” wakati wa ziara yake wilayani Maswa.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan akiagana na wananchi wa Wilaya ya Maswa mara baada ya mkutano wa Hadhara uliofanyika Uwanja wa Nguzo Nane mjini Maswa.
Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki ambaye pia ni Naibu Waziri wa Madini , Mhe.Stanslaus Nyogo, akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Maswa kwenye mkutano wa Hadhara uliofanyika katika uwanja wa Nguzo nane Mjini Maswa, wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan wilayani humo
Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, Mhe.Mashimba Ndaki, akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Maswa kwenye mkutano wa Hadhara uliofanyika katika uwanja wa Nguzo nane Mjini Maswa, wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan wilayani humo.

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!