Monday, February 26, 2018

RC MTAKA: FEDHA ZA WADAU WA AFYA ZILENGE KUJIBU MAHITAJI YA WANANCHI


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amewataka wadau na mashirika mbalimbali wanaofanya kazi na Mkoa huo  katika sekta ya Afya kuelekeza fedha zao zaidi katika masuala yanayojibu mahitaji ya wananchi wa Mkoa huo kwenye Afya badala ya kujikita zaidi katika kugharamia mafunzo na semina kwa watumishi.

Mtaka ameyasema hayo katika kikao kilichofanyika Februari 26, Mjini Bariadi kwa lengo la kufanya tathmini ya mchango wa fedha za wahisani na wadau mbalimbali wa sekta ya Afya mkoani Simiyu  na matokeo yake katika mahitaji halisi ya Kiafya kwa wananchi.

Amesema mkoa huo una wadau wengi wanaounga mkono juhudi za Serikali katika sekta Afya na wanatoa fedha nyingi ambazo zikiwekwa pamoja na fedha zinazotengwa na Serikali kupitia bajeti za Halmashauri zinaweza kujibu mahitaji ya mkoa huo ambayo  ni pamoja na upungufu wa zahanati na vituo vya Afya .

“ Msingi mkubwa wa kikao hiki ni kutaka tufanye tathmini ya fedha zinazotolewa na wadau ndani ya mkoa wetu,  kwa mwaka huu kwenye Halmashauri zetu tumetenga Bilioni 33.4  na tuna shilingi bilioni 11 kutoka kwa wadau  kwa ajili ya sekta ya afya, hivi ‘impact’(matokeo) ya hizi bilioni 11 iko wapi? Natamani hapa kila mwenye fedha yake atuambie mwaka huu atafanya nini” alisema Mtaka.

“Nashukuru TAMISEMI mko hapa hili ni la kuliangalia , kama tunaingia mikataba ya shilingi bilioni 11 kwa mwaka na mashirika yanayofanya kazi za Afya ndani ya Mkoa kwa ajili ya kuwajengea uwezo watumishi, uhamasishaji na semina,  wakati tukiwa kwenye mazingira ambayo hatuna hata nusu ya idadi ya zahanati na vituo vya afya vinavyohitajika ni lazima tutafakari wote”  alisisitiza Mtaka.

Wakati huo huo Mtaka ametoa wito kwa wataalam wa Afya kuendelea kutoa elimu na kuwahamasisha wananchi kuzingatia uzazi wa mpango na akasisitiza umuhimu wa kutoa elimu kwa wazazi watarajiwa (vijana) ili waanze kufanya maandalizi mapema juu ya maamuzi ya idadi ya watoto watakaoweza kuwahudumia baadaye.

Naye Katibu Tawala Mkoa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini amesema malengo waliyojiwekea katika kikao hicho ni pamoja na kuhakikisha kazi zinazofanywa na wadau wa Afya mkoani humo zinajibu matatizo ya Wanasimiyu  na namna ya kuwa na uratibu mzuri  wa shughuli zao, mambo ambayo yamepokelewa na wadau hao na kuahidi kuweka uratibu mzuri ili kuimariasha afya za wananchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirikala Cuso International Tanzania, Ndg.Romanus Mtung’e amesema wadau wa Afya Mkoani humo watashirikiana na Viongozi na Wataalam wa Afya katika kuweka mipango ya baadaye na watazingatia vipaumbele ambavyo vitaleta matokeo chanya yanayoonekana kwa wananchi mkoani humo.

Kikao cha wadau wa Afya na Viongozi Mkoa Simiyu kimewahusisha Viongozi na Wataalam wa Afya ngazi ya Mkoa na Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Makatibu Tawala wa Wilaya, Viongozi wa Dini pamoja na wadau(mashirika) wa Afya wanaofanya kazi na mkoa wa Simiyu wakiwemo AMREF, AGPAHI, CUAMM, UNFPA, Mkapa Foundation, AMERICARE, PSI,Red Cross, ICAP, TAMA, INTRAHELTH, WORD VISION, BORESHA AFYA, CHAI, MARIESTOPES na BRIDGE2 AID.

MWISHO

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na viongozi, watendaji katika Sekta ya Afya pamoja na wadau mbalimbali wa Afya mkoani humo katika kikao maalum kilichofanyika kwa lengo la kutathmini  mchango wa wadau wa Afya(mashirika mbalimbali yanayofanya kazi na mkoa huo)  ambacho kilichofanyika Mjini Bariadi.
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini akifafanua jambo katika kikao kati ya Viongozi wa Mkoa huo , watendaji wa Sekta ya Afya ngazi ya mkoa na Wilaya na wadau mbalimbali wa Sekta ya Afya kilichofanyika Mjini Bariadi.
 Mratibu wa Mpango wa Kudhibiti UKIMWI Mkoa wa Simiyu, Dkt.Khamisi Kulemba akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mpango huo Mkoani humo katika kikao  kati ya Viongozi wa Mkoa huo , watendaji wa Sekta ya Afya ngazi ya mkoa na Wilaya na wadau mbalimbali wa Sekta ya Afya kilichofanyika Mjini Bariadi.
Baadhi ya Viongozi wa Mkoa wa Simiyu , watendaji wa Sekta ya Afya na wadau mbalimbali wa Sekta ya Afya Mkoani humo wakifuatilia mada mbalimbali katika kikao cha tathmini ya mchango wa wadau mbalimbali wa Afya Mkoani Simiyu kilichofanyika Mjini Bariadi.
Mwakilishi Mkazi Msaidizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu (UNFPA), Bi. Christine Mwanukuzi Kwayu  akichangia jambo katika kikao kati ya Viongozi wa Mkoa wa Simiyu , watendaji wa Sekta ya Afya na wadau mbalimbali wa Sekta ya Afya kilichofanyika Mjini Bariadi.
Mkurugenzi Mkazi wa Shirikala Cuso International Tanzania, Ndg.Romanus Mtung’e akichangia jambo katika kikao kati ya Viongozi wa Mkoa wa Simiyu , watendaji wa Sekta ya Afya na wadau mbalimbali wa Sekta ya Afya kilichofanyika Mjini Bariadi.
Baadhi ya Viongozi wa Mkoa wa Simiyu , watendaji wa Sekta ya Afya na wadau mbalimbali wa Sekta ya Afya Mkoani humo wakifuatilia mada mbalimbali katika kikao cha tathmini ya mchango wa wadau mbalimbali wa Afya Mkoani Simiyu kilichofanyika Mjini Bariadi.
Shekhe wa Mkoa wa Simiyu, Mahamoud Kalokola akichangia jambo katika kikao kati ya Viongozi wa Mkoa wa Simiyu , watendaji wa Sekta ya Afya na wadau mbalimbali wa Sekta ya Afya kilichofanyika Mjini Bariadi.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Mkoa wa Simiyu (CCT), Mchungaji Martine Samson Nketo akichangia jambo katika kikao kati ya Viongozi wa Mkoa wa Simiyu , watendaji wa Sekta ya Afya na wadau mbalimbali wa Sekta ya Afya kilichofanyika Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (katikati walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Viongozi wa Mkoa wa Simiyu , watendaji wa Sekta ya Afya na wadau (mashirika) mbalimbali wa Sekta ya Afya wanaofanya kazi na Mkoa huo mara baada ya kufungua kikao kilichofanyika Mjini Bariadi.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!