Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Samia Suluhu Hassan amewahakikishia wananchi wa Itilima
ujenzi wa hospitali ya wilaya itakayowawezesha kupata huduma bora zaidi za Afya
wilayani humo.
Mhe.Makamu wa Rais ameyasema alipowasalimia wananchi
wa makao makuu ya wilaya ya Itilima Lagangabilili mara baada ya kufungua Jengo
la Utawala la Halmashauri ya Wilaya Itilima.
Amewapongeza viongozi wilayani humo kwa kutatua changamoto mbalimbali za
wananchi katika sekta za elimu, maji, kilimo na sekta nyingine huku akiahidi
kushughulikia suala la ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ambayo ndiyo changamoto
kubwa ya afya wilayani humo.
“Niwapongeze kwa mambo mbalimbali
mliyopata kwenye elimu, maji, umeme na kuhusu changamoto ya afya niwaahidi tu kuwa, hiyo ndiyo sekta
ninayoisimamia mimi kama mama nitahakikisha Hospitali ya Wilaya inajengwa hapa
Itilima” alisema
Aidha, akizungumza mara baada ya
kufungua jengo la utawala la halmashauri
ya ITILIMA ameupongeza uongozi wa wilaya
ya Itilima kwa usimamizi mzuri wa Jengo na kuhakikisha linajengwa kwa gharama
nafuu, huku akiwataka watendaji walitumie kuwatumikia wananchi katika kutatua
kero zao.
Amesema Serikali imeboresha mazingira ya
kazi kwa watumishi wilayani humo kwa kuwajengea jengo la kufanyia kazi na
nyumba za kuishi hivyo wanapaswa kuwatumikia wananchi na watakaoshindwa kutekeleza
majukumu yao ipasavyo hawatavumiliwa.
Wakati huo huo amewataka wananchi wa
wilaya hiyo kulitumia jengo hilo kwa kupeleka masuala yao yanayopaswa kufanyiwa
kazi na Serikali kabla ya kwenda
Serikali Kuu na akaahidi kuwa Serikali
itaendelea kuwapelekea watumishi wanaohitahijika.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Itilima,
Mbunge wa Jimbo la Itilima Mhe. Njalu Silanga ameishukuru
Serikali kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani humo.
“Mhe.Makamu wa Rais tunaishukuru
Serikali ya awamu ya tano kwa jinsi
inavyotekeleza miradi mbalimbali, hapa tulipo tunalo tenki lenye ujazo wa lita
250,000 lenye thamani ya shilingi milioni 910, tunayo mabwawa manane kati ya
hayo Bwawa la Habiya lililojengwa na Kampuni ya Serikali ya DDCA limeshaisha na
tayari kwenye bajeti ya mwaka huu kuna usanifu unaendelea vijiji vinne vitapata
maji “ alisema Njalu.
Akiwasilisha taarifa ya Ujenzi wa Jengo
hilo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Ndg. Mariano Mwanyigu amesema jengo hilo lenye
vyumba 45 lililojengwa na wakala wa majengo nchini TBA , limegharimu kiasi
shilingi milioni 621.
MWISHO
Makamu
wa Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan(wa pili kushoto) akikata utepe kufungua jengo
la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Itilima wakati wa Ziara yake Mkoani
Simiyu, (kushoto) Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka
Mbunge wa Jimbo la
Itilima, Mhe.Njalu Silanga akizungumza na wananchi wa Lagangabili mara baada ya
Makamu wa Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan kufungua jengo la Utawala la Halmashauri
ya Wilaya ya Itilima wakati wa Ziara yake Mkoani Simiyu, (kushoto) Mkuu wa Mkoa
huo, Mhe.Anthony Mtaka.
Makamu wa Rais
Mhe.Samia Suluhu Hassan(kushoto) akizungumza jambo na viongozi wa Mkoa wa
Simiyu na Wilaya ya Itilima kabla ya kufungua Jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya
Itilima wakati wa Ziara yake Mkoani Simiyu.
Makamu wa Rais
Mhe.Samia Suluhu Hassan akizungumza na Wananchi wa Lagangabili Wilayani ya
Itilima mara baada ya kufungua Jengo la
Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Itilima wakati wa Ziara yake Mkoani Simiyu.
Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan akipata maelezo juu ya
Ujenzi wa Jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Itilima kutoka kwa
Meneja wa TBA Mkoa wa Simiyu, Mhandisi. Likimaitare Naunga wakati wa Ziara yake
Mkoani humo.
0 comments:
Post a Comment