Thursday, February 15, 2018

SIMIYU KUVUNA PAMBA KILO MILIONI 300 MWAKA 2018


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amesema mkoa huo unatarajia kuvuna kilo milioni 300 za zao la pamba katika msimu wa mwaka 2017/2018

Mtaka aliyasema hayo jana wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa Bariadi Mjini kwenye Mkutano wa Hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Mnada wa Kidinda.

 “ Matarajio yetu mwaka huu kama mkoa ni kuvuna pamba ambayo haijawahi kutokea tangu tumepata Uhuru, ndiyo maana  tunafuata vinyunyizi(dawa za kuuwa wadudu) chupa milioni mbili, tunatarajia kuvuna zaidi ya kilo milioni 300 za pamba” alisema Mtaka.

Amesema kutokana ongezeko hilo la mavuno matarajio ya Mkoa ni kuongezeka kwa mzunguko wa fedha ndani ya mkoa ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa vibarua na wafanyakazi katika Viwanda vya kuchambua pamba(ginneries).

Aliongeza kuwa Serikali ina mpango wa kujenga Kiwanda cha bidhaa za Afya zitokanazo na zao la pamba katika Mkoa wa Simiyu ambacho kitaajiri zaidi ya watu 3000 hivyo akawataka wananchi kuzitumia fursa hizo vizuri.

Aidha, Mtaka alisema Mkoa unaandaa utaratibu wa kuwawezesha wafanyabiashara hasa katika siku za Minada ya Bariadi mjini(Kidinda) na Dutwa (Jumanne na Alhamisi) kufanya biashara kwa masaa sita zaidi, kuanzia saa 12:00 jioni hadi saa 06:00 usiku katika moja ya barabara za Mjini Bariadi.

Alisema barabara hizo zitawekewa taa na Uongozi wa Mkoa na Wilaya utazungumza na Jeshi la polisi namna ya kufanya Doria ili kuwahakikishia  wafanyabiashara hao usalama wao na mali zao.


Wakati huo huo Mtaka amewaeleza wananchi wa Wilaya ya Bariadi kuwa Mkoa wa Simiyu umepata Kanda ya Simiyu ya Maonesho ya Sikukuu ya Wakulima Nane nane itakayojumuisha mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga , ambapo Uwanja wa Maonesho unatarajiwa kujengwa katika Mtaa wa Nayakabindi Halmashauri ya Mji wa Bariadi 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mhe.Robert Lweyo alimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Simiyu kwa jitihada anazofanya katika kuwaletea maendeleo wananchi, ikiwa ni pamoja na kusimamia suala la Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda ambapo alimshukuru kwa kutafuta vyerehani 50 ambavyo vitatumika kuanzisha kiwanda cha ushonaji.

Katika Mkutano huo wa Hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Mnada wa Kidinda wananchi walitoa kero zao ambazo zote zilipatiwa majawabu na viongozi na Wataalam ngazi ya Wilaya ya Mkoa.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu akizungumza na wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi kwenye Mkutano wa Hadhara uliofanyika jana katika Uwanja wa Mnada wa Kidinda
Bw. Shimbi Yuda akitoa malalamiko yake kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (hayupo pichani) kwenye Mkutano wa Hadhara uliofanyika jana katika Uwanja wa Mnada wa Kidinda Mjini Bariadi.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi kwenye Mkutano wa Hadhara uliofanyika jana katika Uwanja wa Mnada wa Kidinda.
Mkurugenzi wa Mji wa Bariadi,Ndg.Melkizedeck Humbe akitoa ufafanuzi kuhusu kero na malalamiko mbalimbali yaliyowasilishwa na wananchi kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka wakati wa Mkutano wa Hadhara uliofanyika jana katika Uwanja wa Mnada wa Kidinda Mjini Bariadi. 
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(kulia) na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Mhe.Robert Lweyo wakifurahia jambo jana kwenye Mkutano wa Hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Mnada wa Kidinda Mjini Bariadi.
Bw. Saguda Maduhu Mkazi wa Bariadi akitoa malalamiko yake kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (hayupo pichani) kwenye Mkutano wa Hadhara uliofanyika jana katika Uwanja wa Mnada wa Kidinda Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (wa tano kulia), baadhi ya viongozi wa Wilaya ya Bariadi na Mkoa wa Simiyu wakicheza wimbo wa Kabila la Kisukuma na Msanii Elizabeth Maliganya (mwenye sketi ya rangi za bendera ya Taifa) kwenye Mkutano wa Hadhara uliofanyika jana katika Uwanja wa Mnada wa Kidinda Mjini Bariadi.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!