Balozi wa Ireland nchini Tanzania Mhe.
Paul Sherlock amemuahidi Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Anthony Mtaka kuendeleza
ushirikiano na Mkoa wa Simiyu ili kuboresha sekta ya Afya kupitia Irish Aid.
Balozi huyo ameyasema hayo wakati wa
mazungumzo ya pamoja na Mhe Mtaka ambapo tayari kwa pamoja wamekubaliana kuanza
kutekelezwa wa kusudio hilo tarehe 6 Februari 2018 kwa kuanza na timu ya
wataalamu kufika Mkoani humo ili kuanza haraka shughuli hiyo.
Balozi Mhe. Paul Sherlock amemuahidi Mhe
Mtaka kuwa tayari nchi yake ya Ireland imekusudia kwa dhati kushirikiana vyema
na Mkoa huo huku akisisitiza kuendelea kushirikiana zaidi pia katika
utekelezaji wa miradi ya Maendeleo kwenye sekta ya Mifugo, Kilimo na Utalii.
Balozi wa Ireland nchini Tanzania Mhe.
Paul Sherlock ametoa kauli hiyo ya kuunga mkono juhudi za Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu Mhe. Antony Mtaka za katika kuboresha sekta mbalimbali ikiwemo uwekezaji
wakati alipokutana na kufanya mazungumzo leo 2 Februari 2018 katika.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Anthony
Mtaka amemshukuru Balozi Sherlock kwa ubalozi wa Ireland kukubali kuwezesha
safari ya mafunzo kwa wataalamu wawili kutoka Mkoani Simiyu kwenda nchini
Ireland kuanzia Februari 12 mpaka 16 Machi 2018 kwa ajili ya kupata mafunzo ya
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) hasa kwenye upande wa uhifadhi wa
Data za Mkoa.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa
wa Simiyu Mhe Mtaka alikutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkaazi wa
shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na Idadi ya watu duniani (UNFPA) Bi
Jacqurline Mahon ambapo pamoja na mambo mengine Shirika hilo limetoa zaidi
Bilioni 3 kwa ajili ya kukarabati vituo vya afya na upasuaji ndani ya
Halmashauri zote za Mkoa wa Simiyu.
Pia UNFPA imeahidi kutoa magari kwa
Halmashauri 6 za Mkoa wa Simiyu kwa ajili ya kuboresha huduma za afya, ambapo
tayari UNFPA wameamua kujenga ofisi yao ndogo ndani ya Mkoa wa Simiyu
itakayoratibu shughuli mbalimbali za shirika hilo kwa mikoa yote ya kanda ya
ziwa.
Wakati huo huo Mhe Mtaka amekutana na
Balozi wa Indonesia nchini Tanzania Prof Ratlan Pardede ambaye pamoja na
mambo mengine amekubali kutembelea Mkoa wa Simiyu mwezi Machi mwaka huu 2018
huku akiwaalika wataalamu wa Mkoa wa Simiyu nchini Indonesia mwezi Aprili mwaka
huu.
Aidha, Balozi huyo Prof Pardede alisema
kuwa pia sekta rasmi ya Indonesia itazuru Mkoani Simiyu ili kuona uwezekano wa
kujenga kiwanda kitakachosaidia kuongeza thamani ya zao la pamba, kuboresha
mkoa dada wa Indonesia na Simiyu katika mazao ya Mpunga na pamba pamoja na
kualika wawekezaji wa Indonesia kuwekeza Mkoani Simiyu kwa kuzingatia Mwongozo
wa uwekezaji wa Mkoa wa Mkoa huo (Simiyu Investment Guide).
Balozi Prof Pardede ameusifia Mwongozo
wa Uwekezaji wa Mkoa wa Simiyu kwamba ni wa kipekee na alipouona mwongozo huo
kupitia mtandao wa Youtube aliona ukiwa umeitangaza sana Tanzania na
wafanyabiashara wa Indonesia walihamasika sana kuuona na kuusoma katika Tovuti
hiyo.
:- Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Anthony Mtaka
(Kulia) akisalimiana na Balozi wa Ireland nchini Tanzania Mhe. Paul Sherlock
ofisini kwake Jijini Dar es salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Anthony Mtaka (Kushoto) akimkabidhi Balozi wa Indonesia nchini
Tanzania, Mhe. Prof Ratlan Pardede Mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa wa Simiyu.
Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu Mhe Anthony Mtaka (Kulia) akifurahia jambo na Mwakilishi Mkaazi wa Shirika
la Umoja wa Mataifa linalohusika na Idadi ya watu duniani (UNFPA) Bi. Jacqurline
Mahon.
0 comments:
Post a Comment