Monday, February 19, 2018

MAKAMU WA RAIS AWAHAKIKISHIA WANANCHI UPATIKANAJI WA DAWA ZA KUUWA WADUDU WAHARIBIFU WA PAMBA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan amewahakikishia wananchi wa Mkoa wa Simiyu kuwa Serikali itamaliza kabisa tatizo la uhaba wa dawa za kuuwa wadudu waharibifu wa zao la pamba.


Mhe. Makamu wa Rais ameyasema hayo leo wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Busega kwenye Mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Lamadi wakati akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake Mkoani Simiyu.

Amesema awamu ya kwanza ya dawa zimeshafika Simiyu kwa ajili ya kuwagawia wakulima wa pamba na akaahidi kuwa awamu ya pili ya kuleta dawa hizo inamalizika katika wiki inayoanza leo tarehe 19/02/2018, hivyo tatizo hilo litakuwa limekwisha.

“Ninajua kuna kiasi kikubwa cha dawa kinakuja Simiyu dawa itakuwa nyingi na wakulima wote watapata, hatuwezi kuacha nguvu zenu zipotee bure na kwa kuwa Simiyu ni mkoa wa Viwanda na ndiyo unazalisha pamba kwa wingi tutajenga viwanda vinavyotumia pamba, kwa maana hiyo hatuwezi kuiacha pamba iharibike” alisema.

Katika hatua nyingine Mhe.Makamu wa Rais wakati akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Masanzakona baada kuweka  jiwe la msingi mradi wa maji wa Kiloleli amewahimiza wananchi kuchangia huduma za maji ili miradi ya maji iwe endelevu.

Amesema Serikali imedhamiria kumaliza kabisa tatizo la maji hapa nchini kwa kujenga miradi ya maji  hivyo ni vema wananchi wakaunga mkono juhudi za Serikali kwa kuchangia huduma za maji ili kusaidia miradi hiyo kujiendesha.

Akiwasilisha taarifa ya mradi wa Kiloleli kwa Makamu wa Rais, Mhandisi wa Maji Wilaya ya Busega, Mohammed Said amesema mradi huo utagharimu jumla ya shilingi bilioni 1.6 mpaka kukamilika kwake mwezi Machi 2018  na utawahudumia wananchi wa vijiji vitatu vya Yitwimila B, Ihale na Ijitu.

 Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Busega, Mbunge wa Busega Mhe. Raphael Chegeni amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli kwa kutekeleza ahadi aliyoitoa kwa wananchi wakati wa ziara yake Mkoani Simiyu ya kuwapelekea mradi wa Maji wananchi wa kata ya Kiloleli.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameanza ziara ya kikazi ya siku nne(04) mkoani Simiyu, ambapo amepata fursa ya kuzungumza na wananchi pamoja na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika Wilaya ya Busega na Bariadi.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe.Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Masanzakona leo wilayani Busega wakati wa ziara  yake wilayani humo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe.Samia Suluhu Hassan (mwenye ushungi) akiweka jiwe la msingi mradi wa maji wa Kiloleli wilayani Busega wakati wa ziara yake wilayani humo leo,(kushoto) Mbunge wa Busega, Mhe.Dkt.Raphael Chegeni.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan akiweka jiwe la msingi Nyumba za Viongozi wa Mkoa katika eneo la Nyaumata mjini Bariadi, wakati wa ziara yake wilayani humo, (kulia) Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe.Samia Suluhu Hassan (mwenye ushungi)  akikagua mradi wa maji wa Kiloleli wilayani Busega mara baada ya kuuwekea jiwe la msingi wakati wa ziara yake wilayani humo leo.

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe.Samia Suluhu Hassan (kulia) akipewa maelezo na Meneja wa TBA Mkoa wa Simiyu, Mhandisi.Likimaitare Naunga kuhusu Mradi wa Ujenzi wa Nyumba za Viongozi wa Mkoa huo mara baada ya kuuwekea jiwe la msingi leo Mjini Bariadi.



Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka (kushoto) akizungumza jambo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe.Samia Suluhu Hassan,  (kulia) Mbunge wa Busega, Dkt.Raphel Chegeni, Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Mhe.Enock Yakobo wakati wa ziara yake mkoani Simiyu.

 Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe.Tano Mwera akiwasilisha taarifa ya wilaya kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe.Samia Suluhu Hassan (hayupo pichani) katika Mkutano wa Hadhara uliofanyika kata ya Lamadi.


0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!