Wakala wa Usajili, Ufilisi na
Udhamini hapa nchini (RITA) unatarajia kuanza kutekeleza mpango wa kusajili na
kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kuanzia
mwezi Machi , mwaka huu mkoani Simiyu.
Hayo yameelezwa na Kaimu Mtendaji
Mkuu wa RITA, Bi.Emmy Hudson wakati wa Ufunguzi wa semina ya viongozi ngazi ya
Mkoa na wilaya iliyofanyika Mjini Bariadi kwa lengo la kuwapa uelewa wa kina
viongozi hao juu ya mpango huu utakaotekelezwa katika maeneo mbalimbali hapa
nchini.
Amesema hali ya usajili nchini
hairidhishi ambapo amebainisha kuwa, kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya
mwaka 2012 ni asilimia 13.4 tu ya wananchi hapa nchini ndiyo waliosajiliwa na
kupewa vyeti vya kuzaliwa.
Ameongeza kuwa ili kuboresha
mazingira ya usajili nchini Wakala wa Usajili,
Ufilisi na Udhamini (RITA) imeandaa mkakati wa maboresho ya kuhakikisha kuwa
kila tukio la uzazi linalotokea nchini linasajiliwa kwa wakati, ambao pia unalenga makundi matatu la kwanza
likiwa ni la watoto chini ya miaka
mitano, kundi la miaka mitano hadi 17 na kundi la miaka 18 na kuendelea.
“Tutakuwa hapa Simiyu kusajili
watoto wa umri wa chini ya miaka mitano ambao idadi yao ni 351, 000, takwimu zinaonesha ni asilimia tano tu ya
watoto ndiyo waliosajiliwa, kwa hiyo hali ya usajili na utoaji wa vyeti vya
kuzaliwa Simiyu iko chini na ndiyo maana RITA tumeona tuje ili watoto wote wa
Simiyu wapate vyeti vya kuzaliwa na kusajiliwa” alisema Kaimu Mtendaji Mkuu
RITA.
Amesema RITA itafanya kampeni kwa
muda wa wiki mbili za mwanzo ili kuwaandikisha watoto wote ambao walikuwa
hawajaandikishwa na kupewa vyeti vya kuzaliwa, baada ya hapo watoto wote
watakaozaliwa baada ya hiyo kampeni wataandikishwa katika Ofisi za Watendaji wa
Vijiji, Kata na kwenye vituo vya Tiba ili kusogeza huduma karibu na wananchi.
Aidha, Kaimu mtendaji Mkuu RITA
amesema katika kuhakikisha kila mtoto anasajiliwa Serikali imeondoa ada kwa
kundi la watoto walio chini ya umri wa miaka mitano hivyo wananchi watapata
huduma hii bila malipo yoyote.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe.Anthony Mtaka amesema watumishi watakaoshiriki zoezi la usajili na utoaji
wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto chini ya miaka mitano hususani Watendaji wa Kata
naVijiji wajengewe uwezo na akaziagiza Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya
Mkoani humo kusimamia zoezi hili ili
lifanyike kwa ufanisi mkubwa na uzalendo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Maswa,
Dkt.Seif Shekalaghe amesema mpango huu wa usajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa
kwa watoto chini ya miaka mitano utawasaidia wananchi kupata huduma karibu na
maeneo wanayoishi (Ofisi za Watendaji wa Kata na Vijiji) kwa kuwa awali
walikuwa wanalazimika kwenda kwenye Ofisi za Wakuu wa Wilaya ili kupata vyeti hivyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji
wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Ndg.Abdallah Malela amesema viongozi wa
Wilaya watahakikisha kila mtoto anayezaliwa anaandikishwa kupitia Ofisi za
Watendaji wa Kata na Vijiji na kupewa cheti, jambo litakalowasaidia kupata takwimu
zitakazotumika kufanya maoteo ya wanafunzi wanaopaswa kuanza darasa la kwanza
na darasa la awali miaka ijayo.
Kikao hiki kiliwahusisha Wajumbe
wa Kamati za Ulinzi na Usalama Mkoa na Wilaya, Makatibu Tawala Wasaidizi wa
Sekretarieti ya Mkoa, Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa na Wilaya, Maafisa
Ustawi wa Jamii wa Wilaya, Waganga Wakuu wa Wilaya, Waratibu wa Huduma za Afya
ya mama na mtoto pamoja na watumishi
wanaoshughulikia usajili wa vyeti vya kuzaliwa katika Ofisi za Wakuu wa Wilaya.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa
Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini Tanzania (RITA) Bi.Emmy Hudson
akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Simiyu wakati wa ufunguzi wa Semina ya
Viongozi hao yenye lengo la kuwapa uelewa wa kina juu ya mpango maboresho ya
usajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano,
iliyofanyika jana Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe.Anthony Mtaka akifungua Semina ya Viongozi wa Mkoa huo iliyoandaliwa na Wakala
wa Usajili, Ufilisi na Udhamini Tanzania (RITA) kuhusu elimu ya ya mpango wa maboresho
ya usajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri chini ya miaka
mitano, iliyofanyika jana Mjini Bariadi.
Katibu Tawala Mkoa wa
Simiyu, Ndg. Jumanne Sagini akifafanua jambo katika Semina ya Viongozi wa Mkoa
huo iliyoandaliwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini Tanzania (RITA) kwa
lengo la kuwapa uelewa wa mpango wa maboresho ya usajili na kutoa vyeti vya
kuzaliwa kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano, iliyofanyika jana Mjini
Bariadi.
Baadhi ya Viongozi wa
Mkoa wa Simiyu wakiwa katika semina ya kuwapa uelewa wa mpango wa maboresho ya
usajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano
ambayo iliandaliwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini Tanzania (RITA) iliyofanyika
jana Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe.Anthony Mtaka(katikati walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya
viongozi wa Mkoa wa Simiyu na watumishi wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na
Udhamini Tanzania (RITA), mara baada ya kufungua Semina ya Viongozi wa Mkoa huo
iliyoandaliwa na RITA Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe.Anthony Mtaka(katikati walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya
viongozi wa Mkoa wa Simiyu mara baada ya kufungua Semina ya Viongozi hao
iliyoandaliwa na RITA Mjini Bariadi.
0 comments:
Post a Comment