Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mhe. Festo Kiswaga amemuagiza
Meneja wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) wa Halmashauri ya
Wilaya ya Bariadi kumtafuta mkandarasi
wa Kampuni ya LNGA na kumpeleka Polisi ili akatoe maelezo ya sababu za kutelekeza
kazi ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 28 na kukiuka masharti ya
mkataba.
Kiswaga alitoa
agizo hilo wakati wa zoezi la kutia saini mikataba 16 ya ujenzi wa barabara na
madaraja kati ya Wakandarasi na Mameneja wa Wakala wa Barabara Vijijini
na Mijini (TARURA) wa Halmashauri za Mkoa
wa Simiyu., ambapo alishuhudia zoezi hilo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe.Anthony Mtaka.
Kiswaga amesema amekuwa akimtafuta
mkandarasi huyo ili wakae pamoja kujua sababu za kutelekeza na kuchelewesha
ukamilishaji wa mradi huo lakini amekuwa akikaidi wito na maagizo ya Serikali , hivyo ipo
haja afikishwe katika jeshi hilo ili aweze kutoa maelezo.
“Mhandisi alinieleza mwenendo wa kazi
yake nikamwita Ofisini tukamwonya, nilienda kutembelea mradi sikumkuta nikampigia
simu hapokei, hii wiki ya tatu hapokei simu yangu wala ya Mhandisi, naagiza
huyu mkandarasi LNGA atafutwe apelekwe polisi ili atueleze anatekeleza mradi wa
Serikali au barabara ya nyumbani kwake” alisema Kiswaga.
Meneja wa
TARURA wa Halmashauri ya Bariadi Vijijini Mhandisi. Masatu Ndango amesema
amepokea maelekezo ya Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga ya
kumtafuta mkandarasi LNGA, anayefanya kazi ya matengenezo ya barabara ya Mbiti-Sakwe-Itubukilo
(KM 17), Sakwe-Mbiti(KM 4), Sakwe-Pugu (KM 3) na Ngulyati-Mwanzoya (KM 4)
ambaye kwa mujibu wa mkataba alipaswa kukamilisha kazi Desemba 2017.
Ndango amesema Mkandarasi
huyo amekuwa akikaidi maelekezo kila anapoelezwa na ameshindwa kukamilisha mradi kwa wakati, hivyo kwa mujibu wa mkataba ameanza kukatwa Fedha
ambazo ni adhabu ya ucheleweshwaji wa mradi(Liquidated damage).
Kutokana na hali hiyo Mkuu wa Wilaya, Mhe.Festo
Kiswaga amesema Wakandarasi wa aina hiyo hawana na nafasi katika Mkoa wa Simiyu
na kamwe wasifikirie kuwa mkoa huo ni mahali pa kujifunzia, hivyo akawataka
Wakandarasi wote 16 waliosaini mikataba ya ujenzi wa barabara na madaraja
kupitia TARURA kuheshimu kazi wanazopewa na Serikali.
Aidha, amewataka Mameneja wa TARURA
mkoani Simiyu kuhakikisha wanajiridhisha na uwezo wa wakandarasi wote
watakaotekeleza miradi mkoani humo, ili miradi yote itekelezwe kwa wakati na
ubora unaotakiwa.
Akiwasilisha taarifa kwa niaba ya
Mratibu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Simiyu,
Meneja wa TARURA Halmashauri ya Mji Bariadi Mhandisi.Mathias Mugolozi amesema jumla ya mikataba itakayotekelezwa
ni 16 ikiwa na thamani ya shilingi 1, 830, 524,724.91, ambapo Halmashauri ya Mji
ina mikataba miwili(02), Bariadi Vijijini miwili(02), Itilima miwili(02), Busega
miwili(02), Meatu miwili(02) na Maswa mikataba sita(06).
Kwa upande wake Mratibu wa TARURA
Mkoa wa Simiyu, Mhandisi.Peter Mosha amesema TARURA mkoa pamoja na Mameneja wa TARURA wa Halmashauri
wamejipanga na watahakikisha wanatembelea miradi yote mara kwa mara na kufanya
vikao vya ndani kwa lengo la kufanya tathmini ya maendeleo ya miradi hiyo.
Naye Mkandarasi Fahmy Hemed
kutoka Kampuni ya Hemed Holdings Ltd ya Mkoani Shinyanga amesema watahakikisha
wanafanya kazi katika viwango vya ubora vinavyohitajika, kukamilisha kwa
wakati na kuheshimu mikataba.
Miradi hii 16 ni ya kwanza
kutekelezwa Mkoani Simiyu chini ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini
(TARURA), tangu kuanzishwa kwa Wakala
huo kupitia Tangazo la Serikali la tarehe 12/05/2017 na kuzinduliwa rasmi
tarehe 02/07/2017.
Mkuu
wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga akishuhudia zoezi la kutia saini
mikataba 16 ya ujenzi wa barabara
na madaraja kati ya Wakandarasi na Mameneja wa Wakala wa Barabara
Vijijini na Mijini(TARURA) wa Halmashauri za Mkoa wa Simiyu lililofanyika jana
mjini Bariadi
Mratibu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini(TARURA)
Mkoa wa Simiyu, Mhandisi.Peter Mosha akizungumza na wakandarasi wa makampuni ya
ujenzi(hawapo pichani) kabla ya zoezi zoezi la kutia saini
mikataba 16 ya ujenzi wa barabara
na madaraja kati ya Wakandarasi hao na Mameneja wa Wakala wa TARURA wa
Halmashauri za Mkoa wa Simiyu lililofanyika jana mjini Bariadi
Mkuu wa Wilaya ya
Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga akizungumza
na wakandarasi wa makampuni ya ujenzi(hawapo pichani) kabla ya zoezi zoezi
la kutia saini mikataba 16 ya
ujenzi wa barabara na madaraja kati ya Wakandarasi hao na Mameneja wa
Wakala wa TARURA wa Halmashauri za Mkoa wa Simiyu lililofanyika jana mjini
Bariadi
Meneja wa TARURA Halmashauri ya Mji wa Bariadi,
Mhandisi.Mathias Mugolozi akifafanua jambo kabla ya zoezi zoezi la kutia saini mikataba 16 ya ujenzi wa barabara na madaraja kati
ya Wakandarasi hao na Mameneja wa Wakala wa TARURA wa Halmashauri za Mkoa
wa Simiyu lililofanyika jana mjini Bariadi
Mwanasheria kutoka Wakala wa Barabara Vijijini na
Mijini(TARURA), Bw.Speratus Boniphace akifafanua jambo, kabla ya
zoezi
la kutia saini mikataba 16 ya
ujenzi wa barabara na madaraja kati ya Wakandarasi na Mameneja wa Wakala
wa Barabara Vijijini na Mijini(TARURA) wa Halmashauri za Mkoa wa Simiyu
lililofanyika jana mjini Bariadi
Baadhi ya Wakandarasi wa Makampuni ya ujenzi wakifuatilia
maelekezo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga aliyotoa kwa
niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka, kabla ya zoezi la kutia saini
mikataba 16 ya ujenzi wa barabara
na madaraja kati ya Wakandarasi na Mameneja wa Wakala wa Barabara
Vijijini na Mijini(TARURA) wa Halmashauri za Mkoa wa Simiyu lililofanyika jana
mjini Bariadi
0 comments:
Post a Comment