Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Elimu hususani ya juu ni nguzo Muhimu
ya kufikia Agenda ya Serikali ya kuwa na Tanzania ya Viwanda na kufikia Uchumi
wa Kati ifikapo 2025.
Makamu wa Rais wa amesema hayo ,wakati
wa akifungua kongamano la elimu ya juu na Tanzania ya viwanda lililofanyika mjini
Bariadi, lililokuwa limeandaliwa na Chuo kikuu huria Tanzania kwa kushirikiana
na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.
Amesema kutokana na umuhimu huo Serikali
imeamua kuwekeza katika Elimu na Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2025 imeweka elimu
kuwa kipaumbele cha juu kwa kuwa ndiyo kitovu cha kuleta mabadiliko ya kiuchumi katika jamii.
“Ninyi ni mashahidi kuwa Serikali
imeweka mkazo kwenye elimu, tumeanza na shule za msingi, sekondari lakini pia tumeongeza
bajeti kubwa kwenye mikopo ya Elimu ya Juu na tutakwenda polepole mpaka
tuhakikishe Watanzania wanapata elimu ya kutosha ili kuendana na uchumi wa
Viwanda” alisema.
Ameongeza kuwa lengo kuu la ni Serikali kuongeza kipato cha
wananchi kupitia viwanda ambavyo vitaongeza thamani ya mazao yanayozalishwa katika
maeneo mbalimbali hapa nchini.
Aidha, amewataka washiriki wa Kongamano
hilo kuja na majibu ya ni kwa namna gani
wahitimu wa Vyuo Vikuu walivyojipanga katika suala la uzalishaji viwandani na
kubainisha ikiwa fani, stadi na mafunzo
waliyosomea yatakidhi mahitaji ya viwanda vinavyotakiwa kujengwa hapa nchini.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha
Tanzania, Prof.Elifas Bisanda amesema nchi zote zilizoendelea katika Sekta ya
Viwanda zina msukumo mkubwa na udahili mkubwa wa Wanafunzi wa Elimu ya Juu,
hivyo upo umuhimu wa kujadili Mchango wa
Elimu ya Juu katika Tanzania ya Viwanda.
Aidha, Prof.Bisanda ametoa wito kwa
wananchi wa Mkoa wa Simiyu kutumia fursa ya uwepo wa Chuo Kikuu Huria cha
Tanzania kwa ajili ya kujiendeleza katika masomo ya elimu ya juu.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe.Anthony Mtaka amewataka waajiri wote mkoani humo kuwaruhusu watumishi
kwenda kusoma kwa ajili ya kuwaandaa watumishi hao kuwa na maarifa ya kutosha.
“ Tuna shida kwenye ofisi zetu tena wakati mwingine ni roho mbaya tu, mtumishi anaomba kwenda
kusoma Mkurugenzi anamkatalia, tukitaka nchi yetu iende mbele turuhusu watu
wasome, miaka ijayo tunataka mkoa wetu
ushindane hatuwezi kushindana kama hatutawekeza kwenye maarifa” alisisitiza
Mtaka.
Wasomi waliowasilisha mada mbalimbali
katika Kongamo hilo la Elimu ya Juu na Tanzania ya Viwanda ni pamoja na Prof.
Rwekaza Mukandala, Prof.Elifas Bisanda , Prof.Uswege Minga, Dkt. Adolf
Rutayuga, Dkt. George Mgode, Balozi Nicholas Kuhanga na Mhe.Anthony Diallo.
Kongamano hili lililokuwa na Mada kuu
isemayo: “Mustakabali wa Elimu ya Juu
kuelekea Tanzania ya Viwanda” limehudhuriwa na wanafunzi wa shule za
sekondari, walimu, Wanafunzi wa Vyuo Vikuu kutoka Mwanza pamoja na viongozi wa
Serikali.
MWISHO
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan aifungua Kongamano la Elimu ya Juu na Tanzania ya Viwanda lililofanyika Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na Washiriki wa Kongamano la Elimu ya Juu lililofanyika Mjini
Bariadi.
Baadhi ya Washiriki wa
Kongamano la Elimu ya Juu na Tanzania ya Viwanda kutoka ndani na nje ya Mkoa wa
Simiyu wakifuatilia ufunguzi wa Kongamano hilo uliofanywa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan mjini Bariadi.
Makamu Mkuu wa Chuo
Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Elifas Bisanda akizungumza na Washiriki wa
Kongamano la Elimu ya Juu lililofanyika Mjini Bariadi(hawapo pichani)
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan(wa pili
kushoto) akifurahia jambo na viongozi wa Mkoa wa Simiyu wakati wa Kongamano la
Elimu ya Juu na Tanzania ya Viwanda lililofanyika Mjini Bariadi.
Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan(katikati walioketi )
akiwa katika picha ya pamoja na wawasilishaji wa mada wa Kongamano la Elimu ya Juu na Tanzania ya Viwanda
lililofanyika Mjini Bariadi.(waliosimama mstari wa nyuma) na viongozi wengine
kutoka ndani na nje ya mkoa wa Simiyu.
0 comments:
Post a Comment