Serikali imewahakikishia wakulima wa pamba Mkoani Simiyu kuwa itatoa chupa 2,000,000 za dawa ya kuuwa wadudu wanaoshambulia
zao la Pamba ili kuwasaidia katika kukabiliana na wadudu hao.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mhandisi Mathew Mtigumwe
jana alipofanya ziara katika Wilaya ya Bariadi, Itilima na Maswa Mkoani Simiyu kwa ajili ya kukagua mashamba ya pamba na
kujionea changamoto zinazowakabili wakulima wa pamba.
Mhandisi Mtigumwe
amesema lengo la Serikali lilikuwa ni kutoa chupa za dawa 1,800,000 lakini
kutokana kuongezeka kwa wakulima wa zao hilo, Serikali kupitia Bodi ya Pamba imeamua kutoa
chupa 2,000,000 .
“Awali tulipanga kusambaza chupa 1,800,000 lakini mahitaji yamekuwa makubwa,
kwa hiyo tutaongeza na kufikia chupa 2,000,000 na kufikia mwishoni mwa mwezi
Februari chupa 1,000,000 zitakuwa zimeshafika Simiyu” alisistiza Mhandisi Mtigumwe.
Aidha, Mtigumwe alisisitiza viongozi na wataalam wa
Kilimo mkoani Simiyu kusimamia ugawaji wa dawa hizo kwa wakulima na kuhakikisha
zinatumika vizuri.
Aliongeza
kuwa Wizara imetoa wataalam wake wasiopungua 60 kutoka makao makuu ya Wizara,
Kituo cha Utafiti cha Ukirigulu na Chuo cha Kilimo Ukirigulu na kuwapeleka katika
mikoa yote inayolima pamba, lengo likiwa ni kutoa elimu kwa wakulima na Maafisa
Ugani juu ya matumizi sahihi ya dawa za kuua wadudu(viuadudu).
Masanja Mabula mkulima wa Pamba kutoka Kijiji cha Mbiti Wilayani Bariadi alisema katika
msimu wa mwaka 2017/2018 wakulima wamehamasika kulima pamba hivyo wanaomba
Serikali iwasaidie wapate dawa ili wadhibiti wadudu waharibifu.
Awali akiwasilisha taarifa
ya Mkoa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini alisema Mkoa huo unahitaji chupa za dawa 1,810,839 kwa
ajili ya wakulima wa pamba 309,511 ambao wamelima ekari 602,409 zikitarajiwa
kuzalisha tani 421,686.3 za pamba kwa wastani wa kilo 700 kwa ekari moja.
Hadi kufikia Januari 31, 2018 Mkoa wa Simiyu umelima jumla ya hekta 241,445.2 sawa na ekari 603,613, ambazo ni
asilimia 85.1 ya lengo la kulima ekari 709,296.5
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi
Mathew Mtigumwe (mwenye miwani katikati) akipewa maelezo na mkaguzi wa pamba wilaya ya Bariadi Alfred
Chagula juu ya mmea wa zao la pamba ulioshambuliwa na wadudu wakati wa ziara
yake jana katika mashamba ya wakulima wilayani humo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi
Mathew Mtigumwe (wa pili kushoto), Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.Jumanne
Sagini wakiangalia shamba la pamba Mkulima Emmanuel Masuke wakati
walipotembelea mashamba ya wakulima jana katika Wilaya ya Bariadi, Iilima na
Maswa mkoani Simiyu.
Katibu Mkuu wizara ya Kilimo Mathew Mtigumwe (mwenye miwani)
akimsikiliza mkulima wa pamba Tindigwe Masuke(hayupo pichani) wa kijiji cha
Mbiti wilayani Bariadi alipokuwa akiongelea juu ya uhitaji wa dawa, wakati wa
ziara yake jana mkoani Simiyu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi
Mathew Mtigumwe (mwenye miwani wa pili kushoto), akikagua shamba la pamba la Mkulima
Emmanuel Masuke wakati wa ziara yake jana katika Wilaya ya Bariadi, Iilima na
Maswa mkoani Simiyu.
0 comments:
Post a Comment