Friday, February 16, 2018

RC MTAKA ASITISHA MALIPO YA SHILINGI BILIONI 1.9 KWA WAKANDARASI WALIOSHINDWA KUKAMILISHA MIRADI


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka amesitisha malipo ya shilingi bilioni 1.9   kwa wakandarasi watatu, ambao ni Simiyu Investiment Co. Ltd,  Nselema Associtates Co. Ltd na Great Lakes Construction Co.LTD, wanaotekeleza miradi saba ya maji  wilayani   MEATU ambayo imeshindwa kukamilika tangu mwaka 2014.

Agizo hilo amelitoa wilayani Meatu, mara baada ya kukagua miradi ya maji ya Lubiga, Itinje na Bukundi na kutoridhishwa na kazi iliyofanyika.

“Tunasitisha malipo yote ya wakandarasi  watatu wanatekeleza  miradi saba ya maji ndani ya Wilaya ya Meatu, malipo yafanyike baada ya Wataalam wetu wanasheria, wahandisi wa maji wa Halmashauri ya Meatu, Mhandisi wa Maji Mkoa,  Mwanasheria ya Mkoa na timu ya Mkoa kujiridhisha; ikiwa wanastahili kulipwa watalipwa ikibainika hawana sifa tunavunja mkataba” alisisitiza Mtaka.

Pamoja na kusitisha malipo hayo Mtaka amesema makampuni hayo hayataruhusiwa kufanya kazi za ukandarasi katika miradi yoyote wilayani humo.

Katika hatua nyingine Mtaka amewataka Viongozi wa Kisiasa wilayani Meatu wanaomiliki Makampuni ya Ukandarasi kuacha mara moja kuomba kazi za ujenzi wa miradi mbalimbali katika Halmashauri hiyo badala yake waombe katika Halmashauri jirani Mkoani humo ili kuepuka mgongano wa kimaslahi.

Aidha, amekemea tabia ya baadhi ya viongozi hao wa kisiasa ya kuwapigia simu watumishi wa Halmashauri kwa lengo la kuomba kazi au kudai malipo ya kazi zao na akawahadharisha kuwa endapo hawataacha tabia hii majina yao yatawekwa wazi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu Ndg.Fabian Manoza amesema kuwa wakandarasi hao waliochaguliwa na bodi ya zabuni na kupitishwa katika vikao vya baraza la madiwani kutekeleza miradi hiyo hawana uwezo.

 “Wakandarasi wanaotekeleza miradi hii hawana uwezo wanasubiri walipwe ndiyo kazi ifanyike, pia nikiri kuwa ni kweli kabisa miradi hii inatekelezwa na wanasiasa ndiyo maana hii Halmashauri ya Meatu kuiongoza tunapata shida sana, pale unaposimamia sheria unaitwa kwenye vikao  na kuazimiwa, lakini kama viongozi hasa tulioteuliwa tutasimamia sheria na taratibu” alisema Manoza.

Naye Afisa Ugavi ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya Manunuzi Ndg. Emmanuel Marwa amesema kuwa taratibu za manunuzi hazikufuatwa katika upatikanaji wa wakandarasi hao ikiwa ni pamoja na Kampuni moja kupewa kusaini mkataba wa kazi zaidi ya moja.

Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Mhe.Dkt.Joseph Chilongani, ameunga mkono agizo la Mkuu wa Mkoa la kusitisha malipo na kuangalia namna ya kuvunja mikataba itakapobidi na akabainisha kuwa wamekuwa wakikumbana na changamoto katika utekelezaji wa sheria na maelekezo  mbalimbali kutokana na baadhi ya viongozi kuingilia utekelezaji hivyo ni vema hatua zichukuliwe.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthoy Mtaka akiwa na baadhi ya viongozi wa Mkoa huo na Wilaya ya Meatu wakiondoka eneo la mradi wa maji wa Itinje mara baada ya kukagua mradi huo wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maji wilayani Meatu.


Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Ndg.Fabian Manoza akitoa maelezo juu ya mradi wa Lubiga wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka ya kukagua miradi ya maji wilayani Meatu.


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka akihoji jambo juu ya ujenzi wa tanki(halipo pichani) katika mradi wa Maji wa Itinje wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maji wilayani Meatu.

Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Mhe.Dkt.Joseph Chilongani akifafanua jambo wakati wa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka ya kukagua miradi ya maji wilayani humo

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Mhe.Enock Yakobo akifafanua jambo wakati wa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka ya kukagua miradi ya maji wilayani Meatu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(wa kwanza kulia)  akimsikiliza Katibu wa Jumuiya ya Watumiaji Maji wa Bukundi wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maji wilayani Meatu
Mchungaji Daniel Philimoni Mkandarasi kutoka Kampuni ya Nselema Associtates Co. Ltd anayetekeleza mradi wa Lubiga akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka wakati wa ziara yake   ya kukagua miradi ya maji wilayani Meatu.
Mwanasheria wa Mkoa wa Simiyu, Bi.Mwanahamisi Kawega akifafanua jambo katika kikao cha majumuisho ya ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka baada ya kukagua miradi ya maji wilayani Meatu.
Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Seksheni ya Maji katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, akifafanua jambo katika kikao cha majumuisho ya ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka baada ya kukagua miradi ya maji wilayani Meatu.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Mhe.Pius Machungwa akifafanua jambo katika kikao cha majumuisho ya ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka baada ya kukagua miradi ya maji wilayani humo.
Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, John Lugembe akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka wakati alipokuwa kwenye ziara ya kukagua miradi ya maji wilayani humo.


0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!