Walimu
wa Shule za Msingi Mkoani Simiyu wameiomba Serikali kushughulikia changamoto ya
ukosefu wa vitabu vya darasa la nne ili waweze kutimiza wajibu wao vema wa kuwafundisha wanafunzi
jambo ambalo Serikali ya Mkoa imelipatia majibu.
Ombi
hilo limetolewa kwa Serikali wakati wa kikao kati ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe.Anthony Mtaka na walimu wa Shule ya
msingi Somanda A na Somanda B ambacho kimefanyika katika Shule ya Msingi Somanda
A Mjini Bariadi.
Wakiongea katika
kikao hicho wamesema kutokana na kutokuwepo kwa vitabu vya mtaala ulioboreshwa
wamekuwa wakitumia vitabu vya mtaala wa zamani katika kuwafundisha
wanafunzi, hivyo wanaomba serikali
iwaletee vitabu vipya ili waweze kuendana na mahitaji ya mtaala uliboreshwa.
“Wakati mwingine
tunalazimika kuwafundisha watoto kwa kutumia vitabu vya mtaala wa zamani,
badala ya kuwapa watoto kile wanachostahili tunawapa kilichopitwa na wakati,
tunaomba tupate vitabu vya vipya ili kuendana na mtaala uliopo katika kuwapa
watoto kile wanachostahili” alisisitiza Mwl.Francis Paulo kutoka Shule ya
Msingi Somanda A.
Kwa upande wao
wadhiti Wakuu wa Ubora wa Shule, Hellen Jackson kutoka Halmashauri ya Mji wa
Bariadi na Fabian Machunde kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi wamekiri
kuwepo kwa tatizo la upungufu wa vitabu vya darasa la nne jambo ambalo lina
athari kwa wanafunzi hususani katika ujifunzaji .
“Ni kweli
kukosekana kwa vitabu shuleni kuna athari kubwa kitaaluma mwalimu anahitaji
vitabu na mwanafunzi pia anahitaji vitabu anapofundishwa darasani na kujisomea ili kuongeza maarifa zaidi ya
yale aliyojifunza darasani” alisema Hellen Jackson.
Naye Mkoa wa
Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka baada ya kuwasikiliza walimu pamoja na wadhibiti
Ubora Mkuu hao, amesema Taasisi ya Elimu Ukuzaji Mitaala inapaswa kutimiza
wajibu wake katika kuhakikisha inaleta vitabu hivyo katika Mkoa huo, ili walimu
na wanafunzi wapate vitabu na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
“Kama Taasisi ya
Ukuzaji Mitaala Tanzania imeshindwa kuleta vitabu vya darasa la nne kwa miezi
tisa sasa hawana uhalali wa kuwepo, huyo Mkurugenzi wa Taasisi anaingia Ofisini
kufanya kazi gani kama anajua nchi nzima
haina vitabu vya darasa la nne, atafutwe mtu mwingine atakayekuja na maarifa
mapya akubali maoni ya mikoani” alisema Mtaka.
Ameongeza kuwa
ili walimu waweze kupimwa utendaji wao wa kazi ni lazima wawe na vitabu vya
kufundishia na ili wanafunzi waweze kupimwa kiwango chao cha ufaulu ni lazima
wawe na vitabu vya kujifunzia, hivyo ikiwa Taasisi hiyo haina uwezo wa kuchapicha
vitabu hivyo kwa sasa iupelekee mkoa wa Simiyu nakala zilizohaririwa na mkoa
utaweka utaratibu wa kuchapisha vitabu
hivyo.
Aidha, Mtaka
amesema walimu, viongozi pamoja na wadau mbalimbali wa elimu mkoani Simiyu
wamefanya jitihada kubwa katika kuboresha elimu jambo ambalo limeutoa mkoa huo kufanya
vibaya katika mitihani ya Kitaifa ukiwepo wa darasa la nne, hivyo ni vema
jitihada hizo zisirudhishwe nyuma kwa namna yoyote.
Afisa Elimu Mkoa
wa Simiyu amesema pamoja na kuwepo kwa ukosefu wa vitabu vya darasa la nne Serikali imetoa vitabu kwa
madarasa mengine ikiwemo vitabu vya najifunza kusoma (darasa la kwanza) lakini mgawanyo wa vitabu
hivyo haukuwa mzuri, akaomba ufanyike utaratibu kila mkoa upate nakala chache.
Mkoa wa Simiyu
kwa sasa unahitaji vitabu zaidi ya 50,000 kwa ajili ya kufundishia na
kujifunzia kwa wanafunzi wa darasa la nne.
0 comments:
Post a Comment