Halmashauri ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu
imeshauriwa kuwekeza katika kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi ikiwemo
viatu, mikoba na mikanda kinachomilikiwa na kikundi cha Usindikaji Ngozi
Senani kilicho kata ya Senani wilayani Maswa, ili kuongeza thamani ya ngozi
zitokanazo na mifugo.
Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka wakati wa ziara yake ya kutembelea viwanda vidogo
katika wilaya MASWA.
Mtaka amesema katika kutekeleza Sera ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Tanzania
ya Viwanda , Halmashauri ya Maswa inapaswa kuwekeza katika viwanda vinavyoanzishwa
na vikundi ili kuviwezesha katika upatikanaji wa malighafi ya kutosha, kuongeza
thamani ya mazao ya mifugo pamoja na kilimo ili viwanda hivyo viweze kuzalisha
kwa tija.
“Tungehitaji kuwa mkoa ambao utawekeza sana katika viwanda vidogo na ndiyo
maana tulianza dhana ya Wilaya moja bidhaa moja kiwanda kimoja na sasa
tunakwenda kwenye Kijiji Kimoja Bidhaa Moja Kiwanda kimoja; tunataka kupunguza
uagizwaji wa bidhaa kutoka nje ya Mkoa” alisema Mtaka.
Aidha, ameitaka Halmashauri hiyo kuwasaidia wanakikundi kuweka mifumo
mizuri ya kutengeneza soko la bidhaa zinazozalishwa katika kiwanda hicho ikiwa
ni pamoja na kuuza katika minada yote ya wilaya hiyo na kuimarisha soko la nje.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa,
Dkt.Fredrick Sagamiko amesema Halmashauri itahakikisha kiwanda hicho
kinapata malighafi ya kutosha ambapo
amebainisha kuwa Halmashauri imeingia mkataba na Chuo cha DIT Mwanza kuhakikisha
kuwa inazalisha malighafi(ngozi) kwa wakati kwa ajili ya kiwanda hicho.
Akiwa Malampaka ambapo alitembelea Mradi wa Ghala na Mashine ya
kukoboa mpunga na kupanga madaraja, Mtaka amekipongeza Chama cha Ushirika Bumala
AMCOS kwa kuanzisha kiwanda, huku akiwataka wananchi wa eneo hilo kujiandaa kiushindani katika biashara,
kwa kuwa hivi karibuni Serikali inatarajia kuanza ujenzi wa bandari ya nchi
kavu itakayoenda sambamba na ujenzi wa Reli ya Kisasa(Standard Gauge).
“Ni lazima mjiandae kiushindani katika biashara, miaka mitatu ijayo katika
Mipango ya Serikali Malampaka haitakuwa kama ilivyo, hapa ni mahali ambapo
Standard Gauge ikianza bidhaa zitakuwa zikisafirishwa kwa wingi; nimeshaongea
na Mkurugenzi kuwa eneo hili lipimwe na Halmashauri imiliki eneo la uwekezaji”
alisisitiza Mtaka.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka alitembelea
eneo la ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza
ungalishe katika Kijiji cha Njiapanda, ambacho kitamilikiwa na shule 30 za Halmashauri
ya Wilaya ya Maswa, kinachoanzishwa kwa lengo la kuongeza kipato cha shule na
halmashauri, kutoa ajira kwa wananchi na kuboresha lishe za watu.
Akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu, Afisa Elimu Msingi Wilaya ya Maswa, Mwl. Mabeyo Bujimu amesema shule za
msingi 30 wilayani humo zitanufaika kwa kulima viazi lishe na kukiuzia kiwanda
hicho kama malighafi pamoja na kuuza bidhaa zitakazozalishwa na kiwanda.
Huu ni mwanzo wa ziara ya Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka ambayo amepanga
kutembelea viwanda vidogo vilivyopo katika wilaya zote za mkoa huo.
0 comments:
Post a Comment