Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka wa Viwanja
vya Ndege nchini (TAA), Richard
Mayongela ameiomba serikali kutoa kiupaumbele cha ujenzi wa Viwanja vya Ndege kwa
mikoa ya Simiyu na Lindi katika bajeti ya mwaka 2018/2019 ili kuongeza fursa za
uwekezaji na utalii.
Mayongele ametoa ombi hilo leo katika
kijiji cha IGEGU kata ya Sapiwi wilayani BARIADI katika eneo linalotarajiwa kujengwa Uwanja
wa Ndege wa Mkoa wa Simiyu, wakati wa ziara ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa mkoani
Simiyu.
Amesema hatua za awali za maandalizi ya ujenzi wa Uwanja
huo zimekamilika ambapo usanifu na upembuzi yakinifu vimeshafanyika na makadirio
ya awali yanaonesha kuwa mradi huo utagharimu takribani shilingi bilioni 95.56
na utakapokamilika utawezesha ndege zenye uwezo wa kubeba kuanzia watu 75 na kuendelea kutua.
Ameongeza kuwa Ujenzi wa Uwanja huo utakapokamilika utakuwa ni chachu ya
maendeleo kwa Mkoa huo katika nyanja za uchumi na utalii na utachangia kuufungua mkoa wa Simiyu
kiuchumi pamoja na mikoa mingine ya kanda ya Ziwa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony
Mtaka amesema kukamilika kwa Uwanja huo itakuwa ni faida kubwa kwa kuwa utakuwa
Uwanja pekee wa Serikali hapa nchini
ambao Watalii watautumia kuifikia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa urahisi
kuliko viwanja vingine.
“Tunajenga Uwanja ambao kimkakati unakaa
mpakani mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, karibu na uwanja huu kuna hii
barabara ya inayotunganisha na Mkoa wa Shinyanga kupitia Malampaka ambako kutajengwa
Reli ya Kisasa, hapa jirani tuna eneo
ambalo tutajenga Kiwanda cha Vifaa tiba, mbele yeke tunaanzisha Kanda ya
Nanenane ...tunaamini kukamilika kwa mradi huu kutakuwa na faida sana kwa Serikali na wananchi” alisema Mtaka
Waziri wa Ujenzi , Uchukuzi na Mawasiliano
Prof. Makame Mbarawa amewahikikishia viongozi wa Mkoa wa Simiyu juu ya ujenzi
wa uwanja wa ndege Simiyu, lakini akatoa angalizo kuwa wakati kufanya tathmini
ya fidia ya eneo la ujenzi, gharama ya
fidia isiwe kubwa vinginevyo Uwanja huo
hautaweza kujengwa.
“Wale watakaokuja kufanya tathmini
wahakikishe gharama ya fidia inakuwa chini sana na ifanywe kwa mujibu wa
sheria, hatutaweza kuwadhulumu watu lakini tuhakikishe tathmini inafanyika kwa
mujibu wa sheria” alisisitiza Waziri Mbarawa.
Akizungumza kwa niaba ya Wananchi wa Kijiji
cha Igegu mahali unapotarajiwa kujengwa uwanja huo, Diwani wa Kata ya Sapiwi,
Mhe.Kibuga Gamalieli amesema wananchi wanasubiria kwa shauku kubwa kuona Uwanja
huo unakamilika na akamuhakikishia
Waziri Mbarawa kuwa wananchi hawatadai fidia kubwa katika eneo hilo kwa kuwa
wanataka maendeleo.
Waziri Mbarawa yuko
Mkoani Simiyu kwa ziara ya siku mbili ambapo leo pamoja na kutembelea eneo la
ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mkoa Simiyu amezungumza na watumishi wa Taasisi
zote zilizo chini ya Wizara yake, amekagua Ujenzi wa Hospitali ya Mkoa na
Nyumba za Viongozi wa Mkoa na kutembelea
Kambi ya Mkandarasi wa Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Bariadi-Maswa kata ya
Luguru wilayani Itilima
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya
Ndege Nchini, Richard Mayongele (kulia)
akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame
Mbarawa(mwenye kofia) kuhusu Uwanja wa
Ndege wa mkoa wa Simiyu unaotarajiwa kujengwa Kijiji cha Igegu wilayani Bariadi
wakati wa ziara ya Waziri huyo leo Mkoani Simiyu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (kushoto) akieleza
juu ya umuhimu wa Uwanja wa Ndege wa mkoa unaotarajiwa kujengwa Kijiji cha Igegu
wilayani Bariadi wakati wa ziara ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,Mhe.
Prof. Makame Mbarawa leo Mkoani humo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano,Mhe. Prof. Makame Mbarawa akizungumza na Viongozi wa Mkoa wa Simiyu
wakati alipotembelea eneo la Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mkoa wa Simiyu, unaotarajiwa
kujengwa Kijiji cha Igegu wilayani Bariadi wakati wa ziara yake leo Mkoani humo.
Mkurugenzi Mtendaji
wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi,
Ndg.Abdallah Malela akiwasilisha taarifa ya eneo la Igegu wilayani Bariadi linalotarajiwa
kujengwa Uwanja wa Ndege Mkoani Simiyu kwa
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,Mhe. Prof. Makame Mbarawa alipokuwa
kwenye ziara mkoani humo leo.
Diwani wa Kata ya Sapiwi wilayani Bariadi,
Mhe.Kibuga Gamalieli( kulia) akimweleza jambo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,Mhe.
Prof. Makame Mbarawa(kushoto) alipotembelea eneo linalotarajiwa kujengwa Uwanja
wa Ndege Mkoani Simiyu, wakati alipokuwa katika ziara Mkoani humo leo .
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano,Mhe. Prof. Makame Mbarawa(mwenye kofia) akisalimiana na
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa
Bariadi, Ndg.Melkizedeck Humbe mara baada ya kuwasili wilayani Bariadi kwa ajili
ya kuanza ziara ya siku mbili mkoani Simiyu.
0 comments:
Post a Comment