Na
Stella Kalinga
Serikali Mkoani Simiyu
imesema haiko tayari kuwavumilia na kuwaacha katika vyeo na majukumu waliyonayo
watendaji wanaotoa takwimu zisizo za kweli.
Kauli hiyo imetolewa na
Mkuu wa mkoa huo, Mhe. Anthony Mtaka wakati wa ufunguzi wa mafunzo elekezi
yaliyotolewa kwa Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala Wilaya na Wakurugenzi wa
Halmashauri za Mkoa huo, yaliyofanyika jana Mjini Bariadi, kwa lengo la kuwajengea
uwezo wa kiutendaji, kwa kuwa baadhi ya viongozi hao wametoka katika sekta
binafsi ambazo zina mifumo tofauti ya kitendaji na mfumo wa Serikali.
“Tunawezaje kukaa na Mtendaji
ambaye ukimwomba taarifa za upungufu wa madawati anadanganya, idadi ya wanafunzi
anadanganya, walimu anadaganya tutamchukulia hatua tu. Lazima tupeleke ujumbe
kwamba taarifa za uongo hazina nafasi tena katika Mkoa wa Simiyu. Namwagiza Katibu
Tawala Mkoa, aanze kuchukua hatua stahiki dhidi ya watendaji wote waliotoa
taarifa zisizo za kweli hususani katika
takwimu za wanafunzi, walimu, madawati na vyumba vya madarasa”, alisema Mtaka.
Mtaka amesema azma ya
Serikali Mkoani humo ni kuhakikisha Nafasi za watendaji wasio waadlifu
zinajazwa na watumishi waadilifu, wenye sifa na elimu ya kutosha waliopo katika
Halmashauri za Mkoa huo.
Aidha, Mkuu huyo wa
Mkoa amewataka viongozi hao wa Wilaya kubaini watumishi wenye sifa na uwezo wa
kutekeleza majukumu ya Serikali katika maeneo yao na wawape fursa watumie
talanta zao kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Pamoja na kubaini
watumishi wenye sifa, viongozi hao wameelekezwa kuwachukulia hatua watumishi
wanaopenda kufanya kazi kwa mazoea, ikiwa ni pamoja na kuwapangia majukumu
yanayoendana na uwezo wao wa kufanya kazi.
Katika kuboresha ukusanyaji
wa mapato, Mtaka ametoa wito kwa viongozi hao kuibua vyanzo vipya vya mapato na
kusimamia ukusanyaji wa Mapato hayo kwa kuzingatia maagizo ya Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ya kutowabugudhi wananchi wanyonge
na akawataka Wakurugenzi wa Halmashauri
kuhakikisha wanatenga asilimia 10 ya mapato yao ya ndani kwa ajili ya
kuimarisha vikundi vya uzalishaji vya vijana na wanawake.
Sanjari na hilo Mtaka
amewataka Viongozi hao wa Wilaya kutambua fursa za maendeleo katika maeneo yao
na kuzitekelezafursa hizo kwa manufaa ya Wananchi walio katika maeneo yao.
Akizungumza baada ya
mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe, Tano Mwera alisema mafunzo hayo
yamemsaidia kumpa mwanga na dira ya
utendaji katika nafasi yake hasa katika utaratibu wa mawasiliano na mahusiano
kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kwa Mujibu wa Sheria, Kanuni na
Taratibu za Nchi, Nafasi yake kama Kiongozi wa Serikali Wilayani pamoja na
Sheria na Miongozo ya Vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Mafunzo hayo ya siku
moja kwa Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri ambayo
yaliongozwa na Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini. yaliendeshwa na
Makatibu Tawala Wasaidizi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Vyombo vya
Ulinzi na
Usalama wa Mkoa huo.
0 comments:
Post a Comment