Na Stella Kalinga
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka
amesema Serikali mkoani humo haitawasimamisha kazi walimu wakuu na wakuu wa
shule kutokana na matokeo mabaya ya shule zao, isipokuwa kwa uthibitisho wa
taarifa za wadhibiti ubora wa elimu kuwa hawafai kushika nyadhifa hizo.
Mtaka ameyasema hayo leo ktk ufunguzi wa
mafunzo ya siku mbili ya kuboresha utendaji kwa wajumbe wa kamati za Shule za
Msingi mkoani humo ktk ukumbi wa Kanisa Katoliki mjini Bariadi
Amesema suala la matokeo ya mitihani ya
kitaifa kuwa mabaya lawama hazipaswi kwenda kwa walimu pekee kwa kuwa wazazi,
kamati za shule, walimu na wanafunzi kila mmoja ana wajibu wake.
"Kuna wanafunzi wameshindikana
hawawatii walimu, wazazi nao wanatetea ubovu wa watoto wao, halafu wakifeli
mwalimu asimamishwe, hii haitawezekana kabisa; kwa nini kamati za shule
zisiwajibishwe" alihoji Mtaka.
Amesema ikiwa taarifa za wadhibiti ubora
wa elimu zitaonesha kuwa mwalimu Mkuu au Mkuu wa shule amefanya kazi ktk
kiwango kinachomfanya apoteze sifa za kuwa katika nafasi yake,
Wakurugenzi wa Halmashauri ambao ndio mamlaka yao ya nidhamu watawachukulia
hatua kwa mujibu wa sheria za utumishi wa Umma.
Ameongeza kuwa Wakurugenzi wa
Halmashauri wanapaswa kuwawezesha wadhibiti ubora kupita na kukagua shule zote,
ili taarifa zao ziwe kichocheo cha kuchukua hatua kwa walimu wakuu,wakuu wa
shule na kamati za shule.
Wakati huo huo Mtaka ameishauri Wizara
yenye dhamana na Elimu kuacha utaratibu wa kufanya mabadiliko ya mara kwa mara
ya mitaala ya Elimu ili kudhibiti ubora wa elimu hapa nchini.
Kwa upande wake Mkufunzi wa mafunzo hayo
kutoka Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu(ADEM) Ndg.Adam Mnyavanu amesema
mafunzo hayo yatasaidia kutatua changamoto ya wazazi kutotambua nafasi
yao katika elimu na kupitia kamati za shule wazazi watatambua wajibu wao katika
maendeleo ya elimu.
Vile vile Mnyavanu ametoa wito kwa
Wakurugenzi wa Halmashauri kutenga fedha za kuwawezesha wadhibiti ubora
kutekeleza majukumu yao ipasavyo katika bajeti za Halmashauri na kuhakikisha
fedha hizo zinatumika kama ilivyokusudiwa kwa lengo la kuinua ubora wa elimu.
Mafunzo kwa wajumbe wa kamati za shule
yaliyofadhiliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la EQUIP Tanzania, yamehusisha
pia wataalam wa elimu ngazi ya Mkoa na wilaya na yamelenga kuwaelimisha wajumbe
hao juu ya muundo wa kamati za shule, majukumu yake, namna wajumbe
wanavyopatikana na umuhimu wa kamati hizo katika Maendeleo ya Elimu.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu,
Mhe.Anthony Mtaka akifungua mafunzo ya kuboresha utendaji wa Wajumbe wa Kamati
za Shule za Msingi Mkoani humo ambayo yamefanyika leo Mjini Bariadi .
0 comments:
Post a Comment