Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amemsimamisha kazi kwa muda wa mwezi mmoja Mwenyekiti
wa Kijiji cha Lamadi Wilayani Busega Mhe.Nzala Hezron pamoja na Wajumbe wa
Serikali ya Kijiji hicho, ili kupisha uchunguzi kufuatia tuhuma mbalimbali
zinazowakabili.
Uamuzi
huo umekuja kufuatia malalamiko yaliyotolewa na wananchi wa Lamadi dhidi ya
Mwenyeiti huyo kwa Mkuu Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka katika
Mkutano wa hadhara uliofanyika jana Lamadi, kuhusu tuhuma mbalimbali ikiwemo matumizi
mabaya ya fedha za michango ya wananchi katika Ujenzi wa Shule ya Sekondari
Lukungu pamoja na kutosoma mapato na matumizi ya fedha za michango mbalimbali
ya wananchi.
“Ili tuweze
kutenda haki ya uchunguzi na ukaguzi tumeona ni busara Mwenyekiti asiwe Ofisini
na wajumbe wanaounda Serikali ya Kijiji
wasiwe ofisini ili uchunguzi na ukaguzi wa akaunti uweze kufanyika kwa
haki” alisema Mtaka.
Mtaka amesema
Mkaguzi wa Ndani kutoka katika Ofisi yake atakayeshirikiana na Mkaguzi wa ndani
wa Wilaya ya Busega kufanya ukaguzi katika Akaunti ya Shule kujua namna fedha
zilizochangwa na wananchi na zilizotolewa na Halmashauri zilivyofanya kazi ya
Ujenzi wa Vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo katika Shule ya Sekondari
Lukungu.
Ameongeza kuwa kutokana
na malalamilo ya baadhi ya wadau pamoja na wananchi uchunguzi na ukaguzi huo
pia utahusisha pia Akaunti ya Kijiji cha Lamadi kwa kuwa Kijiji hicho kina hali
nzuri kimapato na kimekuwa kikichangiwa na wadau mbalimbali wa maendeleo, hivyo
ni vema ikabainishwa wadau wanaokichangia, wanachangia kitu gani na namna
michango hiyo inavyotumika.
Aidha, Mtaka
amesema ukaguzi huo pia utafanywa kwenye kamati iliyohusika katika upimaji
viwanja katika Mji Mdogo wa Lamadi kwa sababu nayo imekuwa ikilalamikiwa na
baadhi ya wananchi kuwa haikuwatendea haki.
Mkuu wa Mkoa
huyo amesema uchunguzi na ukaguzi katika maeneo hayo matatu utaanza tarehe
10/01/2018 na taarifa rasmi ya zoezi hilo itatolewa tarehe 10/02/2018 kwa
wananchi kupitia Mkutano wa hadhara, itakapobainika kuwa tuhuma zilizotolewa
dhidi ya watu hao ni za kweli Serikali itachukua hatua.
Wakati huo huo
Mtaka amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega kumuondoa Afisa
Mtendaji wa Kata ya Lamadi Bw.Furaha Magese Ng’onela na kuhakikisha kuwa ifikapo tarehe 10/01/2018
Kijiji cha Lamadi kinapata Mtendaji wa Kijiji kwa kuwa aliyepo sasa anakaimu na
Kata ya Lamadi ipangiwe Afisa Mtendaji mwingine.
Vile vile Mtaka
ameahidi kuchangia mifuko 100 ya saruji katika Ujenzi wa Shule ya Sekondari
Lukungu ambayo sasa imepewe jina lake(Mtaka Sekondari) na wananchi hao, Mkuu wa
Wilaya ya Busega,Mhe.Tano Mwera ameahidi kuchangia mifuko 40 na Mbunge wa Jimbo
la Busega, Mhe.Dkt.Raphael Chegeni ameahidi kutoa vifaa vya ujenzi vyenye
thamani ya shilingi milioni 10 kufanikisha ujenzi huo.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Kijiji cha Lamadi, Mhe.Nzala
Hezron amesema kuhusu suala la ujenzi wa
Shule yeye pamoja na Serikali yake ya Kijiji haikushirikishwa kikamilifu na
Kamati ya Maendeleo ya Kata(WADC).
Naye Mhe.Chegeni
amemhakikishia Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka kuwa michango ya
viongozi, wadau wa mendeleo na wananchi wa Lamadi inayotolewa sasa itatumika
kama ilivyokusudiwa na ikiwa kuna atakayebainika kutumia tofauti na utararibu
atachukuliwa hatua.
Mkuu wa Wilaya
ya Busega, Mhe.Tano mwera ametoa wito kwa wananchi wa Lamadi kuunga mkono juhudi
za Serikali kwa kuchangia shilingi 10,000 kwa kaya ili kufikia Februari 15,
2018 vyumba vinne vya madarasa viwe vimekamilika katika Shule ya Sekondari
Lukungu(imebadilishiwa jina na wananchi na kuitwa Mtaka Sekondari), ambayo hadi
sasa ina madarasa manne na matundu ya vyoo 16 yanayoendelea kukamilishwa ili
wanafunzi waanze masomo.
Nao wananchi wa
Vijiji vinavyounda Kata ya Lamadi wamesema wamejipanga kuhakikisha vyumba vya
madarasa vinajengwa na kukamilika katika
shule hiyo kabla ya Februari 15, 2018 ambapo kila Kitongoji kimejipanga kuanza na ujenzi wa
chumba kimoja cha darasa na vitongoji vyenye watu wachache vitaungana viwili
kujenga chumba kimoja cha darasa, ambapo kamati za ujenzi zitachaguliwa na wananchi
wenyewe.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Lamadi Wilayani
Busega, Mhe. Nzala Hezron akizungumza na wananchi katika Mkutano wa Hadhara ulioitishwa
na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka kwa lengo la kusikiliza kero
mbalimbali za wananchi na kuzitolea ufumbuzi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu
akizungumza na wananchi wa Kata ya Lamadi katika mkutano wa Hadhara uliofanyika
Lamadi wiayani Busega.
Diwani wa Kata ya Lamadi Mhe.Bija
Laurent Bija akizungumza na wananchi wa kata hiyo katika Mkutano wa Hadhara ulioitishwa na Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka kwa lengo la kusikiliza kero mbalimbali za
wananchi na kuzitolea ufumbuzi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe.Anthony Mtaka (kushoto) na Mbunge wa Jimbo la Busega Mhe.Dkt. Raphael
Chegeni wakifurahia jambo wakiwa kwenye Mkutano wa Hadhara uliofanyika katika
Kata ya Lamadi wilayani Busega.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.
Anthony Maka(kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe.Tano Mwera wakiwa kwenye
Mkutano wa Hadhara uliofanyika katika Kata ya Lamadi wilayani Busega.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Simiyu, Boniventure Mushongi akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali katika
Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Lamadi wilayani Busega.
Ngolo Masunga mkazi
wa Kijiji cha Lamadi akiwasilisha malalamiko yake kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe.Anthony Mtaka(hayupo pichani) katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika
Kata ya Lamadi wilayani Busega.
Afisa Mtendaji
wa Kata ya Lamadi Bw.Furaha Magese Ng’onela akifafanua jambo katika Mkutano wa
Hadhara uliofanyika katika Kata hiyo wilayani Busega.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Ndg.Anderson Njiginya akifafanua
jambo katika Mkutano wa Hadhara uliofanyika katika Kata ya Lamadi wilayani humo.
0 comments:
Post a Comment