Katibu Tawala Mkoa wa
Simiyu, Ndg. Jumanne Sagini ametoa wito kwa viongozi na watumishi mkoani humo
kushirikiana na wadau mbalimbali wenye nia njema ya kuunga mkono juhudi za Serikali
katika uboreshaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Sagini ameyasema hayo
leo katika ufunguzi wa kikao cha kuutambulisha Mradi wa USAID Boresha Afya, kilichofanyika
katika Ukumbi wa Kanisa Katoliki Mjini Bariadi.
Amesema Simiyu ni miongoni
mwa mikoa saba ambayo Mradi wa USAID Boresha Afya utatekelezwa kwa kipindi cha
miaka mitano (2017-2022), hivyo akawataka viongozi na wataalam kushirikiana na
wadau hao kuhakikisha mradi huu unasaidia kubadilisha mfumo wa utoaji huduma za
afya katika maeneo yaliyobainishwa.
Aidha, ameongeza kuwa
ujio wa Mradi huu katika Halmashauri zote za Mkoa wa Simiyu uwe ni chachu ya
kuhakikisha huduma za Afya zinapatikana kirahisi kwa wananchi wa Mkoa huo.
“Ndugu washiriki nichukue
nafasi hii kushukuru mashirika na wadau mbalimbali wanaounga mkono juhudi za
Serikali, natoa wito kwa Idara ya Afya Mkoa na wilaya kutoa ushirikiano wa
karibu kuhakikisha mradi huu unafanikiwa na unatoa matunda tarajiwa”
Sagini amesema Serikali
inafanya juhudi za kukabiliana na viashiria visivyoridhisha katika utoaji
huduma za afya ikiwemo kupunguza vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi ambavyo
vinafikia 556 kwa kila vizazi hai 100,000 kwa sasa.
“Vifo hivi vinachangiwa
na mambo mengi, ikiwemo mahudhurio hafifu ya wajawazito kliniki katika theluthi
ya kwanza ya mimba kwa asilimia 24 na wajawazito wanaohudhuria kliniki kwa
mahudhurio manne au zaidi kwa asilimia 51” amesema Sagini.
Sagini amesisitiza kuwa
mafanikio katika suala la kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi halitatatuliwa na
sekta ya Afya pekee bali kwa ushirikiano wa sekta zote za maendeleo.
Kwa upande wake Mganga
Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Simiyu, Dkt.Fredrick Mlekwa amesema Mradi huu
umekuja katika wakati muafaka ambao mkoa unafanya jitihada mbalimbali za
kukabiliana na vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto
wadogo chini ya miaka mitano.
Naye Dkt.Joseph Masenga
kutoka USAID Boresha Afya amesema mradi huo katika mkoa wa Simiyu utajikita
kuunga mkono juhudi za Serikali katika huduma za uzazi wa mpango, Malaria,
Huduma za Afya ya Mtoto, huduma za Uzazi, Lishe na maeneo mengine mtambuka ikiwemo
jinsia, heshima na ushirikishwaji wa jamii katika huduma za Afya (ngazi ya
jamii).
Kwa upande wake Mratibu
wa Mradi wa USAID Boresha Afya wa Mkoa wa Simiyu , Dkt. Charles Suka amesema
utambulisho wa mradi huo umefanyika kwa viongozi na watendaji wa mkoa huo ili
wawe na uelewa wa pamoja ili waweze kutoa mchango katika utengenezaji wa mpango
mkakati wa kupunguza vifo vya mama na mtoto na kuweka mpango wa utekelzaji
wa wa mradi kwa miaka mitano.
Mradi wa USAID Boresha
Afya Mkoani Simiyu, unatekelezwa kwa ubia wa mashirika ya Jhpiego,
Engenderhealth katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na Magharibi ambayo ni Simiyu,
Mara,Kagera, Kigoma, Shinyanga, Geita na Mwanza katika kipindi cha miaka
mitano(2017-2022).
0 comments:
Post a Comment