Na Stella Kalinga
Serikali
Mkoani Simiyu imetoa wito kwa Taasisi zinazoshughulika na Ulinzi na Hifadhi ya
Wanyamapori kuwachukulia hatua askari Wanyamapori wanaojihusisha kwa namna moja
ama nyingine na vitendo vya Ujangili.
Hayo
yamesemwa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Festo Kiswaga ambaye pia ni Mkuu
wa Wilaya ya Bariadi katika Maadhimisho ya Siku ya Wanyamapori duniani, yaliyofanyika
Mjini Bariadi, ambayo yameenda sambamba na zoezi la upandaji miti katika Hospitali
Teule ya Mkoa(Somanda).
Kiswaga
amesema baadhi ya askari wanyamapori wamekuwa wakivujisha siri za kukabiliana
na majangili hali inayosababisha Serikali kupata hasara kutokana na ujangili
kuongezeka na hivyo ameshauri askari hao kuchukuliwa hatua bila kuonewa haya.
“Upo udhaifu kwa baadhi ya walinzi na askari ambao tumewapa dhamana ya
kulinda wanyamapori, nitoe tu wito kwamba viongozi waandamizi wa taasisi hizi kwa
maana ya TANAPA, Vikosi vya kuzuia Ujangili, itakapotokea kiongozi au askari yeyote ana mahusianao na hawa amabao ni majangili
achukuliwe hatua” amesema.
Ameongeza
kuwa pamoja na Serikali kuwawezesha askari wanyamapori kwa silaha za kivita ili
kupambana na majangili, upo umuhimu wa
kuwaongezea mafunzo na kuona namna ya kuongeza vikosi vya Intelejensia
vitakavyosaidia kuwakamata majangili kabla hawajafanya uharibifu katika hifadhi.
Aidha,
Kiswaga ameomba Mashirika yasiyo ya Kiserikali kusaidia vikundi na taasisi
zinazijitolea kuelimisha jamii kuondokana na ujangili ili elimu hii iwafikie wananchi
wote kwa ajili ya kuwasaidia kuona
umuhimu wa kulinda wanyamapori kwa manufaa yao na Taifa wa ujumla.
Vile
vile Kiswaga amewashauri wakazi wa Mkoa wa Simiyu kutumia vizuri fursa ya kuwa
karibu na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa kujenga hoteli za kitalii, kufanya
kazi za sanaa zitazonunuliwa na watalii pamoja na kuanzisha vilabu vya kupinga
masuala ya ujangili kwa ajili ya kujiletea maendeleo yao na ya mkoa kwa ujumla.
Sambamba
na hilo amesisitiza wananchi kuendelea kupanda miti ili kukabiliana na hali ya
jangwa na mabadiliko ya Tabia nchi na kuiomba Taasisi ya RAFIKI Wildlife
Foundation kuona namna ya kuongeza idadi ya miti katika maadhimisho yajayo.
Naye
Mkuu wa Kanda ya Serengeti kutoka Kikosi cha Kuzui Ujangili, Ndg. Said Hassan
Mkeni amesema Maadhimisho ya Siku ya wanyamapori imeenda sambamba na upandaji
miti kwa sababu miti ni chakula cha wanyamapori, vile vile inasaidia kupata
mvua na kuhifadhi mazingira.
Kauli
mbiu ya Siku ya Wanyamapori Duniani Mwaka 2017 ambayo yamefanyika Mkoani Simiyu
kwa Ufadhili wa Shirika lisilo la Kiserikali la RAFIKI Wildlife Foundation ni “
SIKILIZA SAUTI YA VIJANA KWA UHIFADHI”
0 comments:
Post a Comment