Katibu Tawala
wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Miriam Mmbaga amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Busega, Bw. Anderson Njiginya kutoa fedha kwa ajili ya kukamilisha
ujenzi wa majengo ya upasuaji na wodi ya wazazi katika Hospitali ya Wilaya ili
kuboresha hali ya utoaji wa huduma kwa wananchi katika hospitali hiyo.
Mmbaga ametoa agizo hilo Septemba 09,
2020 wakati zoezi la usimamizi shirikishi alipotembelea hospitali hiyo kukagua
maendeleo ya ujenzi wa majengo hayo ambayo yanapaswa kukamilika na kuanza kutoa
huduma ifikapo Septemba 30, 2020.
“Nampongeza Mkurugenzi kwa kujiongeza,
badala ya kusubiri kibali kutoka HAZINA kulipa fedha za kukamilisha ujenzi wa
majengo haya, amejiwekea utaratibu wa kuwalipa mafundi wetu, nimeelekeza kuwa
aongeze kiwango anachotoa kwa kila juma ili kuongeza kasi ya ujenzi na hatimaye
majengo haya yaweze kukamilika na kutumika kwa huduma kusudiwa,” alisema Mmbaga.
Aidha, Mmbaga ameongeza kuwa
ukamilishaji wa majengo hayo uende sambamba na utunzaji wa mazingira ambao
utajumuisha upandaji miti, bustani za maua na utunzaji wa miti asili huku
akitoa pongezi kwa Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri hya Wilaya ya Busega kwa
usimamizi mzuri katika ujenzi wa hospitali hiyo na kumuagiza Mkurugenzi
kumthibitisha katika cheo chake.
Wakati huo huo Mmbaga ameelekeza Timu
ya usimamizi wa afya ngazi ya wilaya (CHMT) kuimarisha usimamizi katika mfuko
wa Afya ya Jamii (CHF) uliboreshwa hususani watoa huduma ngazi ya jamii
wanaohusika katika usajili ili wananchi waweze kupata huduma zilizokusudiwa na serikali.
Katika hatua nyingine Mmbaga
ametembelea kikundi kinachojihusisha kilimo cha umwagiliagi kilichopo kijiji
cha Chamgasa na kuelekeza wataalam wa fedha na uchumi waweze kutoa elimu kwa
wakulima hao juu ya utunzaji na matumizi ya fedha ili wanapopewa mikopo na
wadau waweze kutekeleza miradi ambayo itakuwa endelevu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya
Wilaya ya Busega, Bw. Anderson Njiginya amesema atahakikisha fedha zinatolewa
kwa wakati kwa mafundi wanaoendelea na ujenzi wa majengo ya Upasuaji na wodi ya
wazazi katika hospitali ya wilaya ili shughuli za ujenzi zisikwame.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa
Mkoa wa Simiyu, Dkt. Khamis Kulemba ameipongeza Timu ya usimamizi wa afya ngazi
ya wilaya (CHMT) kwa namna inavyotekeleza majukumu yake huku akisisitiza
watumishi wote wa afya kuendelea kutoa huduma stahiki kwa wananchi.
Nao baadhi
ya watumishi wa afya katika kituo cha afya Lukungu wameomba miundombinu katika
vituo vya kutolea huduma za afya iboreshwe ili kutoa huduma kulingana na hadhi
za vituo hivyo na wananchi wapate huduma wanazotarajia kuzipata katika vituo
husika.
MWISHO.
Katibu tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Miriam Mmbaga
akizungumza na baadhi wajumbe wa Timu ya usimamizi wa masuala ya afya mkoa wa
Simiyu na wilaya ya Busega wakati wa ziara ya Katibu Tawala wa Mkoa iliyolenga kufanya usimamizi
shirikishi katika hospitali hiyo kukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo hayo
ambayo yanapaswa kukamilika na kuanza kutoa huduma ifikapo Septemba 30, 2020.
Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega akitoa
maelezo kwa Katibu tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Miriam Mmbaga katika jengo la
mionzi la Hospitali ya Wilaya hiyo wakati wa ziara ya Katibu Tawala wa Mkoa iliyolenga kufanya usimamizi
shirikishi katika hospitali hiyo kukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo hayo
ambayo yanapaswa kukamilika na kuanza kutoa huduma ifikapo Septemba 30, 2020.
0 comments:
Post a Comment