Friday, March 2, 2018

HATUJAWAKATAA WADAU WA AFYA TUNATAMBUA MCHANGO WAO, TUNAOMBA WAZINGATIE VIPAUMBELE VYA KITAIFA-RC MTAKA


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amesema Serikali Mkoani humo haijawakataa wadau wa Afya kutoka katika Mashirika mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa wanaofanya kazi mbalimbali  katika  kuunga mkono juhudi za Serikali kwenye Sekta ya Afya , bali inatambua mchango wao na inawaomba kufanya kazi kwa kuzingatia vipaumbele vya Kitaifa na Mkoa kwenye Sekta ya Afya.

Mtaka ameyasema hayo katika mazungumzo maalum na waandishi wa Habari wakati alipokuwa akifafanua kauli aliyoitoa katika kikao kilichofanyika Februari 25 na 26 Mjini Bariadi kati ya Viongozi wa Mkoa huo na Wadau Afya mkoani humo ya kuwataka kuelekeza zaidi fedha zao katika kujibu mahitaji ya wananchi kwenye Afya badala ya semina na mafunzo kwa watumishi.

Amesema Serikali inatambua mchango wa Mashirika na wadau wa Afya Mkoani humo kutokana na mambo waliyoyafanya kuunga mkono Serikali kutatatua changamoto mbalimbali za Sekta ya Afya, ikiwa ni pamoja na kutoa magari, kujenga majengo ya upasuaji katika baadhi ya Vituo vya Afya na kuwajengea uwezo watumishi wa afya.

Ameongeza kuwa pamoja na michango hiyo Mashirika mengi yanayofanya kazi Mkoani Simiyu katika Sekta ya Afya yameonekana kujikita zaidi katika kutoa fedha nyingi kwa ajili ya semina na mafunzo kwa watumishi wa Afya , badala ya kusaidia katika kutatua changamoto ambazo ni vipaumbele vya Kitaifa na Mkoa pia katika Sekta ya Afya.

Aidha. Mtaka amebainisha kuwa Vipaumbele vya Kitaifa na Mkoa  katika Sekta ya Afya ni pamoja na Ujenzi wa Miundombinu ya Afya ambayo ni majengo ya zahanati, vituo vya afya, vyumba vya upasuaji, hospitali), Vifaa pamoja na vifaa tiba,  ambapo alieleza kuwa Mkoa huo una upungufu wa Hospitali ya Mkoa, Hospitali mbili za Wilaya, Vituo vya Afya 112 na Zahanati 291.

“Tumepitia bajeti za mashirika haya 11 kwa ujumla wake mwaka 2018 yatatumia zaidi ya shilingi bilioni 21, hizi ni fedha nyingi ambazo kama zitafanya kazi inayoonekana huduma za Afya ndani ya mkoa zitaimarika, changamoto kubwa ambayo mimi kama mkuu wa mkoa na viongozi wenzangu tumeiona ni fedha nyingi kati ya hizo kuelekezwa kwenye mafunzo ya watumishi wa afya” alisema.

“Kwanza nimeyaomba mashirika yanayofanya kazi za Sekta ya Afya ndani ya Mkoa  kila moja kuonesha kazi wanazofanya, pili natoa wito kwa mashirika haya kuelekeza fedha nyingi kwenye kuongeza idadi ya vituo vya afya, zahanati, vifaa na vifaa tiba ili tunapojenga uwezo kwa watumishi wetu wa Afya wawe na mahali pa kwenda kufanyia kazi mafunzo wanayopata” alisisitiza Mtaka

Ameongeza kuwa Ofisi yake imeandika barua Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ili Viongozi kutoka Wizara hizo mbili wakutanishwe pamoja na Viongozi wa Wizara ya Afya na Viongozi wa Mkoa wa Simiyu kwa lengo la kujadili na kuchambua tija ya fedha za wadau/mashirika hayo kwenye Sekta ya  Afya.

Mmoja wa wadau hao  Mwakilishi kutoka Shirika la Mkapa Foundation Bi.Adeline Saguti akichangia hoja katika kikao chao na Viongozi wa Mkoa wa Simiyu alisema Wadau wa Afya Mkoani humo wameahidi kushirikiana na Mkoa huo  kufanyia kazi maeneo yenye uhitaji katika Sekta ya Afya.

Wadau wa Afya (mashirika ya ndani na nje ya nchi) wanaofanya kazi na mkoa wa Simiyu ni pamoja na AMREF, AGPAHI, CUAMM, UNFPA, Mkapa Foundation, AMERICARE, Red Cross, ICAP, TAMA, INTRAHELTH, WORD VISION na BORESHA AFYA.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) ofisini kwake Machi O2, 2018 Mjini Bariadi

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!