Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe. Anthony J. Mtaka ameviagiza Vyombo vya Ulinzi na Usalama, kumkamata na
kumchunguza Meneja wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Wilayani Maswa
(MAUWASA) Mhandisi. Lema Jeremia.
Mtaka ametoa agizo hilo
kufuatia taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mhe. Rosemary Kirigini
kuwa Meneja huyo anatuhumiwa kushindwa kusimamia Mamlaka hiyo na kutoa taarifa
za uongo kuhusu mwenendo mzima wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa chujio la
maji, katika Bwawa la New Sola lililopo katika Kijiji cha Zanzui kwa Kamati ya
Ulinzi na Usalama ya Wilaya.
Aidha, Bi.Rosemary
Kirigini amesema Meneja huyo anapaswa kuchukuliwa hatua kwa kuwa utekelezaji wa mradi huo ulikuwa ukifanyika
bila uwepo wa Bodi ya Mamlaka ya Maji. “Mhe. Mkuu wa Mkoa kwa maneno ya
Mwenyekiti wa Bodi, anasema bodi hii imeanza kazi hivi karibuni kwa maana hiyo haikuwepo,
mimi nasema akamatwe na afikishwe
mahakamani” alisema Kirigini.
Mtaka amesema pamoja na
mradi wa ujenzi wa chujio, Mamlaka hiyo imekuwa ikisambaza maji kwa wananchi bila
kuweka dawa, hali ambayo inaweza kusababisha magonjwa ya mlipuko kama kuhara na
kipindupindu.
“Unakusanya fedha
kutoka kwa wananchi kila mwezi, lakini unawapatia maji yasiyo na dawa na unaona hilo ni jambo la kawaida tu.
Unakusanya shilingi milioni 20 kwa mwezi kutokana na kuwauzia maji wananchi
ambao ni wateja wa mamlaka yako , lakini unashindwa kutoa shilingi milioni
1.7 kununua dawa kwa ajili ya kutibu
maji, kwa nini usishukuliwe hatua?”, alihoji Mtaka.
Wakati huo huo Mhe.
Mtaka amefuta maadhimisho ya kilele cha wiki ya maji kilichopangwa
kufanyika kimkoa wilayani Meatu na
ameelekeza fedha zilizokuwa zimepangwa kufanikisha maadhimisho hayo zitumike
kununua madawati.
“Nimefuta maadhimisho
ya kilele cha wiki ya maji kwa sababu hatuwezi tukawa tunafanya sherehe kuadhimisha wiki ya maji wakati watu
wanakunywa maji ya tope” alisema Mtaka.
0 comments:
Post a Comment